Nenda kwa yaliyomo

Bunzi-karatasi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Polistes)
Bunzi-karatasi
Bunzi-karatasi (Belonogaster juncea) kwenye sega lake
Bunzi-karatasi (Belonogaster juncea) kwenye sega lake
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Hymenoptera (Wadudu wenye mabawa mangavu)
Nusuoda: Apocrita (Hymenoptera wenye kiuno chembamba)
Familia ya juu: Vespoidea
Familia: Vespidae
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Jenasi 26, 4 katika Afrika ya Mashariki:

Bunzi-karatasi (kutoka Kiing. paper wasps) ni nyigu wakubwa na warefu wenye kiuno chembamba na mara nyingi kirefu sana. Ni wana wa nusufamilia Polistinae katika familia Vespidae ya order Hymenoptera. Hujenga masega yao kwa aina ya karatasi wanayotengeneza kwa kutafuna fumwele za mbao na kuchanganya na mate yao. Wanatokea duniani kote isipokuwa Antakitiki. Kuna spishi takriban 1100 ambapo 48 zinatokea Afrika ya Mashariki.

Nyigu hao wana saizi ya kati au kubwa wenye urefu wa mm 10-33. Baadhi ya spishi ni nyeusi yenye mng'ao nyekundu au nyekundu iliyoiva sana. Nyingine ni nyeusi, nyekundu iliyoiva au kahawianyekundu pamoja na idadi tofauti ya miila au mabaka njano. Pingili ya kwanza ya fumbatio ni nyembamba sana na inaweza kuwa ndefu sana, kama ilivyo katika jenasi Belonogaster. Wana miguu mirefu na mandibulo kubwa.

Biolojia

[hariri | hariri chanzo]
Bunzi-karatasi njano wenye sega lao

Spishi zote za bunzi-karatasi za Afrika ya Mashariki hujenga masega ya dutu nyeupe inayofanana na karatasi wanayotengeneza kwa kutafuna fumwele za mbao na kuzichanganya na mate. Masega hayafunikwi kaa matope au nyenzo nyingine, kwa hivyo zinaonekana kwa urahisi. Kila sega lina kikonyo kinacholiunganisha kwenye tawi au muundo wa mbao au wa metali. Nyigu hao hutoa kemikali inayofukuza sisimizi, ambayo hueneza pande zote za kikonyo ili kuzuia kupoteza mayai au majana.

Bunzi-karatasi huonyesha viwango mbalimbali vya ujamii. Katika spishi za kijamii kidogo, majike kadhaa wanaweza kujenga sega moja pamoja na kushiriki majukumu ya utagaji wa mayai, kutunza mayai na majana ya kila mmoja, na ulinzi wa sega. Katika spishi za kijamii zaidi, utagaji wa mayai huwekwa kwa jike mmoja (malkia) na uzao wake hukuwa wafanyakazi waliobobea katika utafutaji wa chakula, ujenzi na ulinzi. Majike wowote wanaoshirikiana huachwa kwa tabaka la wafanyakazi baada ya kupigania utawala. Mshindi anakuwa malkia na hudumisha utawala wake kwa tabia na ishara za kemikali.

Mzunguko wa maisha wa koloni la bunzi-karatasi huanza wakati jike mmoja au kadhaa, ambao wamepandana, huanza kujenga sega. Ikiwa kuna majike kadhaa, wote hutaga mayai au wanapigania utawala. Ikiwa majike wote hutaga mayai, wote wanayatunza pamoja mayai na majana wanaoibuka. Majike wapya wapevu hupandana na kujiunga na mama wao katika utagaji wa mayai na utunzaji wa majana. Madume hukua katika mayai yasiyorutubishwa ambayo yanatagwa kwenye kona tofauti ya sega. Katika maeleo yenye majira ya baridi kali, majike wachanga zaidi hujifichia baridi na kuibuka katika majira ya kuchipua ili kuasisi makoloni mapya. Wanapewa chakula cha ziada kama majana. Katika maeneo yenye joto zaidi, kama vile Afrika ya Mashariki, makoloni polepole hupoteza mshikamano kwa sababu fulani na majike waliosalia huenda na kuasisi makoloni mengine.

Katika bunzi-karatasi za kijamii zaidi, ni jike mmoja tu anayetaga mayai yote. Yeye hutoa chakula kwa majana hadi majike wapya waibuka, ambao huchukua majukumu yake. Majike hawa wanaweza kutaga mayai, lakini maendeleo ya ovari zao yanakandamizwa na uwepo wa malkia. Kwa kawaida hufa wakati majana zimekuwa mabundo. Kwa hivyo kuna kizazi kimoja tu cha wafanyakazi waliopo wakati wowote. Kuelekea mwisho wa msimu, chakula cha ziada hutolewa kwa majana fulani, ambao kisha huendelea kuwa majike wa uzazi. Wanapandana kabla ya kupata mahali pa kujifichia baridi au joto. Wakati msimu mzuri unapofika, wanaibuka kuasisi makoloni mapya.

Spishi nne za Polistes ni vidusia wa lazima wa kijamii, na wamepoteza uwezo wa kujenga masega yao yenyewe. Wakati mwingine hujulikana kama "bunzi-karatasi kekeo". Tatu kati yao hutokea Ulaya na moja Kaskazini-magharibi mwa Afrika (Polistes maroccanus). Kwa kuwa hawajengi masega, majike wa spishi hizi huchukua masega ya spishi zinazohusiana kwa nguvu[7]. Kwa kutoa feromoni ya mwenyeji, huwahadaa wafanyakazi wake kuchunga mayai yao. Kwa hiyo, hawana haja ya wafanyakazi wao wenyewe.

Spishi za Afrika ya Mashariki

[hariri | hariri chanzo]
  • Belonogaster brachystoma
  • Belonogaster brevitarsus
  • Belonogaster brunnea
  • Belonogaster brunnescens
  • Belonogaster clypeata
  • Belonogaster dubia
  • Belonogaster facialis
  • Belonogaster filiventris
  • Belonogaster flava
  • Belonogaster freyi
  • Belonogaster grisea
  • Belonogaster hirsuta
  • Belonogaster juncea
  • Belonogaster kohli
  • Belonogaster lateritia
  • Belonogaster leonhardii
  • Belonogaster leonina
  • Belonogaster levior
  • Belonogaster longitarsus
  • Belonogaster maculata
  • Belonogaster multipunctata
  • Belonogaster neavei
  • Belonogaster pennata
  • Belonogaster pileata
  • Belonogaster punctilla
  • Belonogaster pusilloides
  • Belonogaster saeva
  • Belonogaster somereni
  • Belonogaster tarsata
  • Belonogaster ugandae
  • Belonogaster vasseae
  • Polistes africanus
  • Polistes badius
  • Polistes defectivus
  • Polistes fastidiosus
  • Polistes loveridgei
  • Polistes madiburensis
  • Polistes marginalis
  • Polistes ornatus
  • Polistes smithii
  • Polistes tristis
  • Polybioides melainus
  • Polybioides tabidus
  • Ropalidia cincta
  • Ropalidia distigma
  • Ropalidia guttatipennis
  • Ropalidia nobilis
  • Ropalidia tomentosa