Nenda kwa yaliyomo

Panya-nyika

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Otomys)
Panya-nyika
Panya-nyika wa Mlima Kenya (Otomys orestes)
Panya-nyika wa Mlima Kenya (Otomys orestes)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Rodentia (Wanyama wagugunaji)
Nusuoda: Myomorpha (Wanyama kama panya)
Familia: Muridae (Wanyama walio na mnasaba na panya)
Nusufamilia: Murinae (Wanyama wanaofanan na vipanya-miiba)
Jenasi: Otomys
F. Cuvier, 1824
Ngazi za chini

Spishi 21:

Panya-nyika ni wanyama wagugunaji wa jenasi Otomys katika nusufamilia Murinae ya familia Muridae ambao wanatokea Afrika kusini kwa Sahara katika nyika nyevu mpaka nyanda za juu na vinamasi vya milimani.

Panya-nyika ni wagugunaji imara wenye uelekeo wa kuwa na uso mfupi na miguu mifupi kuliko spishi nyingine za panya. Mwili wao una urefu wa sm 12-22 na uzito wa g 90-260. Mkia pia ni mfupi kuliko panya wengi sana, kwa kawaida kati ya moja na mbili ya tatu ya urefu wa mwili. Rangi ya manyoya inatofautiana kulingana na spishi, lakini kwa ujumla huwa na manyoya kahawia hadi kijivu ambayo ni kawaida kwa panya na wagugunaji wengine wadogo wa porini, ingawa rangi ya upande wa chini ni hafifu zaidi. Spishi zinazoishi katika maeneo yenye joto kubwa au ya wastani huwa na masikio makubwa sana miongoni mwa panya, huku baadhi ya spishi za milimani zikiwa na masikio madogo zaidi. Vidole vyao vyote vina kucha ndefu na kucha za nyuma ni ndefu kuliko kucha za mbele.

Spishi nyingi sana huishi kwenye maeneo manyevu, nyika na makazi yalandanayo na hula mimea ya maeneo hayo, wakiiongezea mara kwa mara mizizi na mbegu. Hizo ni spishi za ardhini ambazo hukaa juu ya ardhi katika viota wazi vilivyo na umbo la bakuli na vilivyotengenezwa na nyasi zilizokatwa-katwa karibu na maeneo yenye mabwawa na uoto mzito.

Mwenendo

[hariri | hariri chanzo]

Panya-nyika hukiakia wakati wa alasiri na alfajiri. Wengi sana hushughulika mchana, ingawa panya-nyika wengine huonyesha shughuli za usiku. Wanaunda na kugawana njia za kukimbia na spishi nyingine zilizopo pamoja nao kupitia uoto wakati wanajilisha kwa mimea kijani.

Panya hao ni walamani thabiti na sehemu kubwa ya mchakato wa kumeng'enya hufanyika katika sikamu kwa msaada wa vijidudu. Vidonge vya kinyesi mara nyingi hunyweshwa tena ili kupata zaidi kutoka kwa chakula duni kwa virutubisho. Chakula chao kina mashina na majani ya nyasi, mimea na vichaka, na mbegu za nyasi. Walakini, sio wachaguzi wa chakula na watakula karibu spishi zote za mimea kijani katika makazi yao. Spishi fulani pia zinaweza kuguguna gome la misonobari kwenye migunda wakiharibu miti hii. Wametoholewa kuwa na kiwango cha uvumilivu wa hali ya juu kwa mimea yenye sumu.

Kwa kawaida huishi peke yao na kugombana na wana wengine wa spishi yao. Madume wapevu hutunza mara nyingi eneo dogo la kinyumba karibu na mahali pa kiota. Wanawasiliana kupitia ishara za kunusa kwa kutopoa eneo lao kwa vinyaa vya tezi za mkundu. Wakati wanyama wenye cheo sawa wanapokutana huanza kupigana na kufukuzana hadi mnyama mmoja atakapokimbia au kuonyesha tabia ya unyenyekevu. Tabia za kunyenyekea ni pamoja na kukaa wima na kufunua tumbo wakitatarika. Mapigano hayo mara nyingi husababisha majeraha, makubwa pengine.