Nenda kwa yaliyomo

Mtoro Bakari

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mtoro bin Mwinyi Bakari)
Saini ya Mtoro Bakari, 1906

Mtoro bin Mwinyi Bakari (Dunda karibu na Bagamoyo, leo nchini Tanzania, 3 Oktoba 1869 [1] - Berlin, Ujerumani, 14 Julai 1927) alikuwa mwandishi wa Afrika Mashariki na mhadhiri wa Kiswahili. Alikusanya habari za utamaduni wa watu wa pwani akaendelea kufundisha Kiswahili katika chuo kikuu Ujerumani. Ndoa yake na Mjerumani mnamo 1904 ilisababisha mtafaruku wa umma na kuchangia mazungumzo ya kisiasa katika Dola la Ujerumani, ambayo mwishowe yalisababisha kupigwa marufuku kwa ndoa za mchanganyiko wa kimbari katika makoloni ya Ujerumani. [2]

Bakari kuhusu Wazaramo (1901)
Bakari kuhusu Wazaramo (Kijerumani), 1901

Mtoro Bakari alizaliwa katika kijiji cha Dunda katika familia ya Wazaramo[3]. Alipokuwa kijana alihamia mji wa karibu wa pwani wa Bagamoyo. [4] Jina lake Mtoro bin Mwinyi Bakari linaonyesha alikuwa mtoto wa mmiliki wa ardhi aliyeitwa Bakari. Huko Ujerumani alitumia sana jina la baba yake kama jina la familia akijiita Mtoro Bakari kwa kifupi. Alizaliwa katika familia ya Waislamu akasoma madrasa alipojifunza Kurani na elimu ya Kiislamu, pamoja na Kiarabu.

Mnamo 1888, alipokuwa bado kijana, Bagamoyo ilikuwa makao makuu ya Shirika kwa Ukoloni wa Kijerumani iliyoweka msingi kwa koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Bagamoyo ikawa mji mkuu wa kwanza wa koloni hilo hadi mwaka 1891. Katikati ya miaka ya 1890, alioa Mamboni binti Amiri Majiru, ambaye alikuwa na binti naye. [5] Bakari alijaribu kujiunga na biashara ya misafara akashindwa. Akiwa msomi, alipata ajira ya mtoza ushuru kwa mamlaka ya kikoloni ya Ujerumani mnamo 1898.

Bakari na Velten

[hariri | hariri chanzo]

Hata kabla ya ajira yake, Mtoro Bakari alikuwa mmojawapo wa Waswahili walioombwa na mkalimani mkuu wa serikali ya kikoloni Carl Velten kuandika habari za utamaduni wa watu wa pwani. Velten alirudi Ujerumani mwaka 1896 kuwa profesa kwenye Chuo Kikuu cha Berlin alipofundisha lugha za Kiafrika, elimu iliyotafutwa sana Ujerumani hasa kwa kuandaa maafisa Wajerumani walioelekea makoloni mapya ya nchi hiyo.

Chuo Kikuu cha Berlin

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1900 Velten alimwalika Bakari kwenda Berlin akawa mhadhiri wa Kiswahili katika taasisi ya Velten kwenye Chuo Kikuu. [6] [7] Bakari, ambaye "alikuwa akihesabiwa kati ya Waswahili waliosoma sana na wenye ujuzi" [8], sio tu kwamba alitoa masomo ya lugha na mazungumzo huko katika miaka michache ijayo, lakini pia aliandika maandishi yake ya kitamaduni na kihistoria, ambayo Carl Velten alichapisha. [9]

Talaka na ndoa na Bertha

[hariri | hariri chanzo]

Bakari alipanga nyumba na familia ya Kijerumani alipoanzisha uhusiano na binti wa familia, Bertha Hilske. Mnamo Desemba 1903 Mtoro Bakari alimwandikia mkwewe Bagamoyo akamtaliki mkewe kulingana na sheria ya Kiislamu kwa sababu alitaka kumuoa Bertha. Carl Velten na mkurugenzi wa semina hiyo Eduard Sachau walizungumza kwa nguvu dhidi ya ndoa hiyo. Waliona haiwezekani Mwafrika kutoka koloni amwoe Mjerumani, pia waliona anataka kumwoa mke wa pili ambayo ni marufuku Ujerumani.

Afisa mmoja katika Wizara ya Mambo ya Nje alimsaida kwa kuuliza serikali ya kikoloni ya Dar es Salaam kama kulikuwa na vizuizi kwa ndoa jibu lilikuwa kufuatana na utaratibu wa Kiislamu uliokubaliwa katika koloni talaka ilikuwa halali, hivyo hapakuwa na vizuizi vya ndoa. Hivyo Bakari na Bertha walifunga ndoa pale Berlin-Charlottenburg katika Oktoba 1904.

Kuacha kazi chuoni na kurudi Afrika

[hariri | hariri chanzo]

Uhusiano kati ya Bakari na wakubwa wake ulikuwa mgumu tangu wakati huo. Bakari alikosolewa mara kwa mara kibaguzi na wanafunzi wake aliomba wakuu wake wamsaidie lakini hawakumlinda tena.

Kwa hivyo Bakari alisitisha ajira yake mapema Mei 1905. Jina lake halijatajwa tena kwenye machapisho ya semina tangu wakati huo, ingawa muswada alizowahi kutunga bado zilitumika. [6] [10]

Mnamo Agosti 1905 Mtoro Bakari ambaye hakuwa na kazi tena alipewa tiketi ya meli na wizara aweze kurudi akasafiri kwenda Afrika Mashariki pamoja na mkewe. Walipofika Tanga kwenye mwezi Septemba 1905 wakati wa Vita ya Majimaji, mkuu Mjerumani wa wilaya aliingia katika meli akamwambia haruhusiwi kutoka. Baada ya kuwasili Dar es Salaam tukio lilirudiwa. Mkuu wa Wilaya alifika kwenye meli akamwambia mke haruhusiwi kutoka. Bakari alitishiwa akionekana na mke wake atadhibiwa kwa kupigwa viboko 25 [6] . Hata hivyo walitembea mjini ambako umati kubwa ya wakazi Waafrika iliwafuata wakishangaa kumwona Mwafrika na mwanamke Mzungu. Polisi iliwarudisha kwenye meli. Siku iliyofuata, Bertha alikwenda peke yake akapeleka malalamiko kwa ofisi ya koloni. Hapo alipewa hati ya kufukuzwa katika koloni na serikali iliwapa tiketi. Akina Bakari walipaswa kurudi Ujerumani.

Taarifa ya Gazeti la Kijerumani la Afrika ya Mashariki (Deutsch-Ostafrikanische Zeitung) ilibeba taarifa juu ya tukio hilo na kusifu serikali, ikieleza hofu kwamba mke Mzungu wa Mwafrika angeharibu sifa za Wazungu wote machoni pa wenyeji, hali iliyotazamiwa kuwa hatari hasa katika hali ya vita iliyoendelea wakati ule.

Baadaye Gavana Gustav Adolf von Götzen alitangaza amri ya kupiga marufuku ndoa zote kati ya wenyeji na Wajerumani, ambazo zilikuwa halali ndani ya Ujerumani lakini aliweza kutumia mamlaka yake ya pekee ya kutoa sheria kwa koloni lake.

Kurudi Ujerumani

[hariri | hariri chanzo]

Oktoba 1905, wenza hao walirudi Berlin, ambapo Bakari alidai fidia kutoka kwa serikali kwa dhuluma waliyokuwa wakipata. Mnamo Januari 1906 alimwandikia Kaisari Wilhelm II. barua alimoelezea uharamu wa hatua zilizochukuliwa dhidi yake, alielezea hali yake ya kiuchumi akaomba nafasi mpya katika utumishi wa umma - iwe Ujerumani au Afrika Mashariki. Mnamo Februari 1906, hata hivyo, alipokea uamuzi kutoka kwa idara ya kikoloni katika Ofisi ya Mambo ya nje iliyokataa. [10] Bakari alizingira mlango wa ofisi hiyo kwa wiki kadhaa akijaribu kuzungumza na afisa aliyehusika. [11] Mnamo Desemba 1906 mwishowe alimwandikia mkurugenzi wa idara ya kikoloni Bernhard Dernburg:

“Kutokana na kufunga ndoa halali chini ya sheria ya Ujerumani, nilifukuzwa kutoka nyumbani kwangu huko Afrika Mashariki ya Ujerumani na vyombo vya serikali ya Ujerumani nikakosa ajira hapa Ujerumani. Kwa hivyo ninaomba kwamba Mheshimiwa atakuwa mwema wa kutosha kunisafirisha kurudi nyumbani pamoja na mke wangu na kuniacha niishi huko, au kupata kazi hapa Berlin ambapo naweza kupata riziki yangu kwa njia halali. ”

Ili kuzuia majadiliano ya umma, Ofisi ya Kikoloni iliamua mwaka 1907 kutafuta kazi mpya kwa Bakari. Bakari alikataa nafasi ya mfanyakazi msaidizi katika duka la vitabu la kikoloni kama haitoshi. [6] [10]

Mhadhiri wa Kiswahili Hamburg

[hariri | hariri chanzo]

Hapo alipata usaidizi na mchungaji aliyewahi kuwa misionari Carl Meinhof, aliyefundisha pia lugha za Kiafrika kwenye Chuo Kikuu aliyemsaidia kupata wanafunzi wa Kiswahili kutoka shirika za misioni alioweza kufundisha kibinafsi. Hadi muhula wa pili wa 1908/09 aliendesha pia semina kuhusu mada ya Uislamu . Katika kitabu cha anwani cha Berlin aliorodheshwa mnamo 1908 kama mhadhiri na mnamo 1909 kama mmisionari . Mwishowe wanaisimu Bernhard Struck na Carl Meinhof walimsaidia Bakari kupata ajira kwenye taasisi mpya ya elimu ya koloni pale Hamburg . Katika barua yake ya kumpendekeza Becker, Meinhof alisifu maarifa ya Bakari, ustadi wake kama mwalimu, busara na ucheshi. [10]

Baada ya kupata kazi kutoka Hamburg, Mtoro Bakari na mkewe waliondoka Berlin mnamo Machi 1909 akaanza kufanya kazi kama "mwalimu msaidizi wa lugha" katika "Semina ya Lugha za Kikoloni" kwenye Taasisi ya Elimu ya Koloni ya Hamburg kuanzia muhula wa pili wa 1909/10. [12] Baada ya miaka kadhaa alipata mzozo na mhadhiri Mjerumani, ambako alihisi anabaguliwa, akalazimika kuondoka katika taasisi ya Hamburg mwaka 1913. Kisha wenza hao wakarudi Berlin. [13]

Baada ya Vita Kuu

[hariri | hariri chanzo]

Hadi miaka ya 1920, Mtoro Bakari alitoa mihadhara juu ya Afrika Mashariki kwenye taasisi mbalimbali katika miji mingi ya Ujerumani kufadhili maisha yake. [6] [13] Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Bakari aliona mara kwa mara changamoto ya ubaguzi wa rangi kwa sababu watu walimwona kama mmoja wa askari wa Kifaransa kutoka kolonia za Kiafrika waliowahi kuvamia maeneo ya magharibi ya Ujerumani kwenye Mto Rhine tangu 1919. Kwa hiyo Bakari aliandika barua kwa serikali ya Ujerumani mnamo 1922 ombi la kupewa barua ya ulinzi inayoweza kuonyeshwa kwenye mamlaka ya miji mbalimbali ili aweza kupata malalo bila kusumbuliwa kwenye safari zake za kufundisha. [14]

Kuanzia 1914 kuendelea, akina Bakari waliishi kwenye nyumba Lichtenrader Strasse 40 pale Berlin-Neukölln. Alipoaga dunia kwenye umri wa miaka 58, alizikwa kwenye makaburi ya Waturuki pale Berlin.[15]

Bertha Bakari mara ya mwisho aliorodheshwa huko kama mjane wa Mtoro katika kitabu cha anwani cha Berlin cha 1929. [16]

Kujisomea

[hariri | hariri chanzo]
  • Mtoro bin Mwinyi Bakari: "Khabari ya inchi ya Wazaramu", [17]
  • Mtoro bin Mwinyi Bakari: "Safari yangu ya Udoe hatta Uzigua na khabari za Wadoe na mila zao" online hapa uk. 205
(vyote viwili katika "Safari za Wasuaheli", ed. Carl Velten, Berlin 1901)
  • Ludger Wimmelbücker: Mtoro bin Mwinyi Bakari (c. 1869-1927). Mtoro bin Mwinyi Bakari (c. 1869-1927). Swahili Lecturer and Author in Germany. Dar es Salaam, (Tanzania): Mkuki na Nyota, 2009, ISBN 978-9987-08-008-3
  • Dictionary of African Biography. Vol. 1, Oxford u. a.: Oxford University Press, 2012 ISBN 978-0-19-538207-5
  1. Tazama Ludger Wimmelbücker: Mtoro bin Mwinyi Bakari (c. 1869-1927). Dar es Salaam 2009, uk. 5f., anaandika pia kuhusu tarehe tofauti zilizotajwa na Bakari kuhusu tarehe yake ya kuzaliwa; inaonekana tarehe hiyo alichagua mwenyewe ilhali wakati wake tarehe halisi hazikuandikwa kwa watoto wote, alipaswa kuchagua tarehe.
  2. Harald Sippel: »Im Interesse des Deutschtums und der weißen Rasse«. Behandlung und Rechtswirkungen von ‚Rassenmischehen‘ in den deutschen Kolonien Deutsch-Ostafrika und Deutsch-Südwestafrika. In: Jahrbuch für afrikanisches Recht 9 (1995), S. 123–159; noch 1912 wurden die Bakaris als negatives Beispiel in einer Reichstagsdebatte angeführt: s. Verhandlungen des Reichstags. Stenographischer Bericht. Bd. 285, S. 1729 (Sitzung v. 7. Mai 1912).
  3. Glassman, Jonathon.. Feasts and riot: revelry, rebellion, and popular consciousness on the Swahili Coast, 1856-1888, §323
  4. Mtoro bin Mwinyi Bakari: Mitteilungen über das Land Uzaramu nebst Sitten und Gebräuchen der Wazaramu. In: Carl Velten (Hg.): Schilderungen der Suaheli von den Expeditionen Dr. Bumillers, Graf von Götzens, und Anderer. Göttingen 1901, S. 225–276.
  5. Ludger Wimmelbücker: Mtoro bin Mwinyi Bakari (c. 1869-1927). Swahili Lecturer and Author in Germany. Dar es Salaam (Tanzania) 2009, S. 5–26.
  6. 6.0 6.1 6.2 6.3 6.4 Lora Wildenthal: German Women for Empire, 1884-1945. Durham NC 2001, S. 111–120.
  7. Ludger Wimmelbücker: Mtoro bin Mwinyi Bakari (c. 1869-1927). Swahili Lecturer and Author in Germany. Dar es Salaam (Tanzania) 2009, S. 27–40.
  8. Richard Niese: Das Personen- und Familienrecht der Suaheli. (Ein Beitrag zur vergleichenden Rechtswissenschaft). Jur. Diss. Universität Marburg, 1902, S. 9 (Vorwort).
  9. Mtoro bin Mwinyi Bakari: Meine Reise nach Udoe bis Uzigua sowie Geschichtliches über die Wadoe und Sitten und Gebräuche derselben. In: Carl Velten (Hg.): Schilderungen der Suaheli von den Expeditionen Dr. Bumillers, Graf von Götzens, und Anderer. Göttingen 1901, S. 138–197; Mitteilungen über das Land Uzaramu nebst Sitten und Gebräuchen der Wazaramu. In: Ob. Cit., S. 225–276; engl. als Mtoro bin Mwinyi Bakari: The Customs of the Swahili People. The ‘Desturi za Waswahil’ of Mtoro bin Mwinyi Bakari and Other Swahili. Berkeley CA: University of California Press, 1981.
  10. 10.0 10.1 10.2 10.3 Ludger Wimmelbücker: Mtoro bin Mwinyi Bakari (c. 1869-1927). Swahili Lecturer and Author in Germany. Dar es Salaam (Tanzania) 2009, S. 41–63.
  11. Oscar Hintrager: Südwestafrika in der deutschen Zeit. München 1955, S. 74.
  12. Jahrbuch der hamburgischen Wissenschaftlichen Anstalten XXVIII (1910), S. 44.
  13. 13.0 13.1 Ludger Wimmelbücker: Mtoro bin Mwinyi Bakari (c. 1869-1927). Swahili Lecturer and Author in Germany. Dar es Salaam (Tanzania) 2009, S. 64ff.
  14. zit. n. Marianne Bechhaus-Gerst: Kiswahili-speaking Africans in Germany before 1945. In: Afrikanistische Arbeitspapiere (AAP) 55 (1998), S. 155–172, hier: S. 161.
  15. Wimmelbücker, uk. 32
  16. Berliner Adreßbücher 1915–1929.
  17. online hapa uk. 126
Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtoro Bakari kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.