Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu ni watawa Wafransisko wanaounda shirika la Kipapa lililoanzisha na Luis Amigo (1854-1934).

Ufupisho wake ni H.T.C.F.S. (kwa Kihispania Hermanas Terciarias Capuchinas de la Sagrada Familia).

Historia[hariri | hariri chanzo]

Masista walianza kuishi kijumuia mwaka 1878 kwenye patakatifu pa Nuestra Señora de Montiel huko Benaguacil (Hispania mashariki).

Kisha kupata kibali cha askofu wa Valencia, tarehe 11 Mei 1885 masista wa kwanza waliweka nadhiri zao.

Padri Amigó aliwapa kanuni ya Utawa Hasa wa Tatu wa Mtakatifu Fransisko na katiba maalumu aliyoiandika mwenyewe.

Muda mfupi baadaye masista walijitosa kuhudumia wagonjwa wa kipindupindu huko Massamagrell, mji alipozaliwa mwanzilishi wao: wanne kati ya masista hao waliambukizwa wakafa.

Tarehe 6 Machi 1902 Papa Leo XIII alikubali shirika ambalo likaja kuhusianishwa na lile la mwanzilishi (Ndugu Wadogo Wakapuchini tarehe 15 Septemba 1905.

Mtindo wa maisha[hariri | hariri chanzo]

Masista wanafuata mtindo wa maisha ya Familia Takatifu ya Yesu, Bikira Maria na Yosefu (mume wa Maria). Hasa wanamfuata Yesu Kristo aliyeishi kwa useja. ufukara na utiifu kwa Baba.

Uenezi[hariri | hariri chanzo]

Masista wanaishi katika nchi 30 duniani, kuanzia Ulaya (Ubelgiji, Ujerumani, Italia, Polandi, Slovakia, Hispania), Afrika (Benin, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea ya Ikweta, Tanzania), Asia (Korea ya Kusini, Ufilipino) na katika nchi nyingi za America ya Kilatini.

Tarehe 31 Desemba 2005 walikuwa 1.347 katika nyumba 223, zikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro na Msolwa (wilaya ya Kilosa).

Kazi[hariri | hariri chanzo]

Masista wanatoa hasa huduma za:

  • elimu bora ya kiroho na ya kimwili katika ngazi zote;
  • malezi kwa watoto na vijana walio katika mazingira magumu;
  • afya wakihudumia wagonjwa, wazee na walemavu;
  • misheni wakifundisha Neno la Mungu katikaparokia hata za nchi ambapo Ukristo haujaenea;
  • utume wa kijamii, wakizingatia mahitaji mbalimbali ya watu, kwa kutembelea familia na kufundisha kazi mbalimbali za mikono.

Wafiadini[hariri | hariri chanzo]

Shirika lilizaa wenye heri 3: Rosario de Soano, Serafina de Ochovi na Francesca de Rafelbuol waliofia dini kwao Hispania mwaka 1936.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Tovuti ya shirika kwa lugha mbalimbali