Nenda kwa yaliyomo

Mapito ya kaskazini-magharibi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mapito ya Kaskazini-magharibi kati ya Atlantiki na Pasifiki.
Mistari nyekundu inaonyesha Mpitto wa kaskazini-magharibi.

Mapito ya kaskazini-magharibi ni njia ya bahari inayoruhusu kupita kutoka Atlantiki kufika Pasifiki (na kinyume) upande wa kaskazini wa Amerika. Njia hiyo inapita katika Bahari Aktiki na kwa sababu ya wingi wa barafu katika sehemu hizo za kaskazini, kwa kawaida hakupitiki na meli. Lakini siku hizi barafu inapungua na kuruhusu mipango ya kuunda njia mpya za mawasiliano, biashara na kuendeleza uchumi wa nchi zinazopakana na Aktiki.

Historia za kutafuta mapito ya kaskazini-magharibi[hariri | hariri chanzo]

Hamu ya mataifa ya Ulaya kupata njia ya bahari kufika Asia[hariri | hariri chanzo]

Tangu karne za kati mataifa ya Ulaya Magharibi walitafuta njia ya kufikia Uhindi na China, nchi ambazo bidhaa zao zilifika tu Ulaya kwa bei ghali sana kupitia kwa wafanyabiashara Waislamu wa Asia ya Magharibi.

Wareno walitangulia kuvuka Afrika na kufika Uhindi na Asia Kusini Mashariki; kwa nia ya kuepukana na ugomvi kati ya mataifa mawili jirani, wafalme wao na wa Hispania walipatana mwaka 1494 katika Mkataba wa Tordesillas kwa msaada wa Papa kugawa kati yao maeneo mapya ya Dunia yatakayovumbuliwa; Wahispania waliahidiwa maeneo upande wa magharibi wa mstari uliofuata longitudo ya 46° 37′. Waliendelea kutafuta njia ya kuzunguka Amerika ili waweze kuendelea hadi China na Uhindi. Mwaka 1520 nahodha Magellan alivuka pembe ya kusini ya Amerika akaingia katika Pasifiki na kuwezesha wasafiri wenzake kumaliza mzunguko wa Dunia.

Kutafuta njia mbadala upanda wa kaskazini-magharibi[hariri | hariri chanzo]

Ilikuwa dhahiri kwamba njia kutoka Ulaya hadi China ingekuwa karibu na nafuu kabisa kama njia ya kupita upande wa kaskazini ingepatikana. Mapito ya kaskazini-magharibi yanafupisha safari kati ya Ulaya na Asia Mashariki kiasi cha kilomita 4,000.

Hii ilileta uhamasisho mkubwa kwa mataifa ya Ulaya Magharibi kutafuta mapito hayo ya kasakazini-magharibi.

Mabaharia na wapelelezi Wahispania, Wafaransa, Waitalia, Wadenmark, Waingereza na wengine walijaribu kukuta njia hiyo. Waliingia katika mito mikubwa na hori zilizoweza kufikiwa kutoka pwani ya Atlantiki lakini njia hizo hazikufika hadi Pasifiki. Wakaendelea kuelekea kaskazini wakiingia kati ya visiwa vya Aktiki lakini mara kwa mara walisimamishwa na ukuta wa barafu.

Ugumu wa mazingira asilia kwenye Aktiki[hariri | hariri chanzo]

Hali halisi hakuna njia rahisi kwa meli na jahazi za zamani kwa sababu ya wingi wa barafu; hata katika miezi ambapo halijoto ya hewa inapanda juu na barafu ya bahari inaanza kuvunjika, vipande vikubwa vya barafu vinaelea kwenye maji yanayoweza kuzamisha hata meli kubwa.

Roald Amundsen alikuwa mtu wa kwanza aliyefaulu kusafiri kwenye mapito ya kaskazini akilazimishwa kupumzika njia mara mbili na kusubiri hadi baridi kali ilipokwisha na barafu ilipoyeyuka tena.

Meli ya kwanza iliyoweza kupita bila kupumzika ilikuwa SS Manhattan katika Septemba 1969 katika muda wa wiki nne. Meli hiyo iliwahi kuimarishwa kwa feleji nyingi ili kuiwezesha kusukuma pande kubwa za barafu zinazoelea majini na kuvunja barafu. Laini meli ilihitaji matengezo mengi baada ya safari.

Mabadiliko ya tabianchi na kufunguliwa kwa njia ya kaskazini[hariri | hariri chanzo]

Ni tangu kupanda kwa halijoto duniani katika miongo iliyopita kwamba barafu katika eneo la Aktiki imeanza kupungua. Tangu mwaka 2008 meli chache zimeanza kubeba mizigo kupitia njia hii wakitumia wiki chache ambapo barafu imevunjika kwa uhakika.

Baada ya mwaka 2010 safari hizo ziliongezeka.

Kadiri barafu ya Aktiki inavyopungua kipindi cha mwaka ambapo uwezekano wa kupita upo unaongezeka.

Tayari viumbehai vya kwanza kutoka Pasifiki ya kaskazini vimeanza kuingia Atlantiki, mfano planktoni ya Pasifiki na pia spishi za nyangumi ambazo hazikuwepo upande huu.

Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.