Mange Kimambi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mange Jumanne Ramadhan Kimambi (alizaliwa mkoa wa Arusha, 1980) ni mmoja wa wanawake wanaharakati wenye ushawishi mkubwa katika nchi ya Tanzania.

Mange Kimambi kabila lake ni Mpare. Ameolewa na mzungu raia wa Marekani na wamebahatika kupata watoto wawili wa kiume. Hadi sasa amekuwa akiishi jijini Los Angeles nchini Marekani tangu mwaka 2008.[1] [2].

Elimu

Mange Kimambi alipata elimu ya msingi katika Shule ya msingi Arusha; baadaye alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Arusha lakini alipelekwa na baba yake kusoma elimu hiyo katika jiji la Harare nchini Zimbabwe.

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari Mange Kimambi alipata nafasi ya kwenda nchini Marekani kwa ajili ya masomo ya juu, lakini wakati akiwa masomoni alipata ujauzito na kujifungua mtoto wa kike aitwaye Bhoke.

Baadaye aliamua kurejea nchini Tanzania ili kujipanga tena kwa ajili ya kuendelea na shule. Dada huyu alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mnamo mwaka 2004 ambapo alisoma na kutunukiwa shahada ya Business Administration. Baada ya kupata shahada alikwenda Dubai katika Falme za Kiarabu ambapo alisoma na kupata shahada ya uzamili(MBA).

Maisha baada ya shule

Maisha ya Mange Kimambi baada ya shule yaliambatana na umaarufu uliokuwa ukikua siku baada ya siku na hii ilichangiwa zaidi na kuandikwa zaidi na magazeti ya udaku pamoja na blogu mbalimbali za Tanzania. Kwa kiasi kikubwa dada huyo hakuwa akifurahishwa na taarifa nyingi zilizokuwa zikiandikwa na kuripotiwa juu yake katika magazeti ya udaku na blogu: jambo hilo lilipelekea Mange Kimambi kuanzisha blogu yake aliyoiita U-Turn kwa ajili ya kujibu mashambulizi ya wale waliokuwa wakimuandama kupitia magazeti na blogu. Kwa muda mrefu amejikuta akiingia katika migogoro na wasanii, wanamitindo na wanablogu maarufu nchini. Baadhi yao ni Zari The Bosslady, Diamond Platnumz, Lemutuz, Wema Sepetu. Kitendo cha yeye kuingia katika majibizano na mastaa hao kimempelekea kuwa maarufu sana nchini, hasa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Katika ulingo wa siasa

Tangu alipoanza kufuatilia na kujihusisha na mambo ya siasa alifikia hatua akawa anasema hajui maisha yake yangekuaje bila CCM. Lakini amejizolea na kujipatia umaarufu zaidi kuanzia mwaka 2016 maara baada ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kuingia madarakani. Umaarufu wa Mange Kimambi umetokana zaidi na kitendo cha yeye kuonesha na uthubutu wa kupinga waziwazi mambo mengi yanayofanywa na Serikali iliyo chini ya chama tawala CCM. Umaarufu wake huu umepelekea kuwa ni miongoni mwa watu wenye wafuatiliaji wengi katika mitandao ya kijamii, hasa Instagram, kiasi cha kufikia kuwa na wafuatiliaji karibu milioni tano.

Tanbihi

  1. "Who Is Mange Kimambi? Jua ukweli wenye facts sio grapevine kumhusu huyu mtu, biography and facts! - JamiiForums". JamiiForums (kwa en-US). Iliwekwa mnamo 2018-09-10. 
  2. YOUR-NAME, "Makala : Mange Kimambi ni Nani? Kumbe kasoma Arusha? Na Jeff Msangi.", Wazalendo 25 Blog (kwa en-US), iliwekwa mnamo 2018-09-10 

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mange Kimambi kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.