Koloni
Koloni ni neno linalotumiwa kwa kutaja:
- makazi mapya ya watu kutoka eneo moja katika eneo jingine
- eneo linalotawaliwa na nchi ya mbali hasa kwa kusudi la kufaidi malighafi yaliyopo au kwa shabaha ya kuwa na kituo cha kijeshi au cha biashara.
Asili ya neno
[hariri | hariri chanzo]Asili ya neno koloni ni Kilatini "colonia" kutokana na kitenzi "colere" (kulima, pia kuabudu). Colonia ilikuwa makazi ya Waroma wa Kale nje ya eneo lao la awali. Chanzo chake kilikuwa mji mpya uliokaliwa na wanajeshi wastaafu waliopewa ardhi kwa ajili ya mashamba kama pensheni yao.
Makoloni ya aina hiyo yalianzishwa hasa mpakani mwa maeneo mapya yaliyotwaliwa karibuni na kungizwa katika Dola la Roma. Walowezi walipewa mashamba yao kwa masharti ya kuwa tayari kutetea mipaka kama vita inatokea.
Aina za makoloni
[hariri | hariri chanzo]Makoloni yalienea hasa tangu upanuzi wa nchi za Ulaya kuanzia karne ya 15 kwa maana ya maeneo yaliyo chini ya nchi nyingine ambayo iko mbali. Makoloni hayo yalianzishwa kwa njia mbalimbali:
- Pengine vituo vya biashara viliundwa kwenye pwani za Afrika na Asia. Vingine viliimarishwa kuwa koloni kamili. Mfano wake ni Afrika Kusini ambako Waholanzi walipeleka walowezi kwa kusudi la kulima vyakula kwa mahitaji ya jahazi zilizosafiri kati ya Ulaya na Asia ya Kusini.
- Makoloni mengine yalianzishwa kwa kusudi la kulima mazao au kupata malighafi yasiyopatikana walikotokea wakoloni. Mfano wake ni Peru ambako Hispania ilijipatia kwa wingi madini ya fedha. Mfano mwingine ni visiwa vya Karibi vilivyogeuzwa kuwa mashamba ya miwa kwa mahitaji ya sukari ya Ulaya.
- Makoloni kadhaa yalianzishwa kwa shabaha za kijeshi ili kuwa na kituo cha kijeshi au bandari. Mfano wake ni Gibraltar.
- Makoloni yaliundwa tena kwa shabaha ya kupeleka walowezi huko. Mfano wake ni makoloni ya Uingereza katika Amerika Kaskazini yaliyounda baadaye nchi ya Marekani. Mengine yaliundwa kwa kusudi la kuwapeleka wafuasi wa madhehebu ya dini yasiyopendwa Uingereza penyewe au kwa shabaha ya kuwapeleka huko watu maskini waliokosa mashamba kwao. Australia ilianzishwa kama koloni la wafungwa wa magereza waliopelekwa mbali ili kuwaondoa nyumbani.
Ukoloni
[hariri | hariri chanzo]Hasa mwisho wa karne ya 19 nchi za Ulaya zilitwaa maeneo na kuyafanya makoloni kwa hofu ya kwamba nchi nyingine itayachukua. Kuwa na koloni kulikuwa kama dalili ya kuwa nchi yenye maana inayoheshimiwa. Mwisho wa karne hiyo takriban 80% za maeneo yote duniani yalitawaliwa kama koloni la namna moja au nyingine.
Kipindi hiki cha ukoloni kiliporomoka baada ya vita kuu ya pili ya dunia, ila kukawa na mwendelezo wake katika ukoloni mamboleo.
Koloni kamili, eneo la kudhaminiwa na nchi lindwa
[hariri | hariri chanzo]Hali za nchi chini ya utawala wa kikoloni zilitofautiana.
- Kwa upande mmoja palikuwa na makoloni yaliyotawaliwa moja kwa moja na watawala wa nje.
- Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia aina mpya ya koloni ilitokea iliyoitwa eneo la kudhaminiwa. Nchi tawala ilikuwa na mamlaka juu ya koloni kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa (League of Nations mandates), baadaye na Umoja wa Mataifa (Unites Nations trust territories). Maeneo ya kudhaminiwa yalikuwa kiasili chini ya nchi zilizoshindwa wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia yaani Ujerumani na Uturuki na kuhamishwa chini ya utawala wa nchi washindi kama Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji na Japani. Tofauti na koloni la kawaida ilikuwa katika masharti ya kutoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa na katika utaratibu wa kupata uhuru. Tanganyika ilikuwa eneo la kudhaminiwa mikononi mwa Uingereza kuanzia mwaka 1922 baada ya kuanzishwa kama koloni la Kijerumani.
- Kwa upande mwingine palikuwa na nchi na maeneo ambako watawala wenyeji waliendelea kuwa na madaraka fulani lakini walipaswa kushauriana na wawakilishi wa nchi kubwa. Nchi hizo zilitazamwa mara nyingi kama “nchi lindwa” (protectorate) chini ya ulinzi wa Uingereza, Ufaransa na kadhalika. Viwango vya mamlaka vya watawala wenyeji vilikuwa tofauti. Mara nyingi zilikuwa kama koloni za kawaida tu ilhali mamlaka halisi zilikuwa mkononi mwa mwakilishi wa mkoloni aliyetoa maagizo kwa jina la mfalme au sultani mwenyeji. Zanzibar ilikuwa nchi lindwa chini ya Uingereza.
Kuna mifano ambapo hali ya kuwa nchi lindwa ilidumu muda mfupi tu kabla ya kumezwa kabisa na kuwa sehemu ya koloni kamili. Mfano wake mmojawapo ni usultani wa Witu ulioingizwa katika koloni la Kenya bila kujali mawazo ya mtawala mwenyeji au ya watu wake.
Lakini kuna pia mifano ambapo mikataba asilia na wenyeji iliheshimiwa na mwisho wa ukoloni maeneo haya yamekuwa nchi huru. Kati ya mifano yake ni Falme za Kiarabu na Botswana iliyokaa nchi ya pekee nje ya Afrika Kusini ingawa serikali ya Afrika Kusini ilitaka iwe chini yake.
Kwa jumla Uingereza ulipendelea mara nyingi kutawala kupitia wenyeji kuliko kuwatawala moja kwa moja. Utawala wa moja kwa moja ulipendelewa kwa mfano na Ufaransa katika makoloni yake.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Koloni kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |