Historia ya Jamhuri ya Dominika

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Jamhuri ya Dominika inahusu eneo la Karibi linalounda Jamhuri hiyo.

Mwanzo na koloni la Hispania[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya kuja kwa Wahispania kisiwa cha Hispaniola kilikaliwa na Waindio Waarawak wa kabila la Wataino kuanzia karne ya 7.

Kristoforo Kolumbus alikanyaga ardhi ya Amerika mara ya kwanza katika eneo la Jamhuri ya Dominika.

Nchi ilikuwa koloni la Hispania kwa jina la "Santo Domingo", ikabaki hivyo hata baada ya Ufaransa kununua theluthi ya magharibi ya kisiwa iliyokuja kuwa Haiti baadaye.

Tangu mwaka 1510 Wahispania walianza kuleta watumwa kutoka Afrika kama wafanyakazi kwenye mashamba makubwa, hasa ya miwa.

Wengi walitoroka na kuanzisha jumuiya huru porini katika milima ya kisiwa.

Hata kama leo zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wote wana damu ya Kiafrika kwa kiasi fulani, watumwa hawakuwa wengi katika Santo Domingo jinsi ilivyokuwa upande wa Haiti chini ya utawala wa Ufaransa. Damu ya Kizungu imechangia zaidi, wakati ile ya Kiindio imechangia kidogo kuliko ya Kiafrika.

Utawala wa Haiti[hariri | hariri chanzo]

Santo Domingo ilitangaza uhuru wake tarehe 30 Novemba 1821 baada ya kuona Hispania ilishindwa kote Amerika Kusini isipokuwa katika visiwa vya Karibi. Lakini baada ya wiki chache nchi ilivamiwa na jeshi la Haiti ikatawaliwa na Wahaiti kwa miaka 22.

Utawala huo ulionekana na wenyeji kama utawala wa mabavu na kuanzia 1838 shirika la siri lilifanya mipango ya kuwa nchi ya pekee tena.

Uhuru tena[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 27 Februari 1844, wakati wa mapinduzi katika Haiti, matajiri wa Santo Domingo walitangaza uhuru wa Jamhuri ya Dominika.

Miaka iliyofuata Haiti ilijaribu kuvamia nchi mara tano ili kurudisha utawala wake lakini watetezi walishinda.

Kurudi kwa Wahispania[hariri | hariri chanzo]

Kati ya miaka 1861 na 1865 rais Santana alikabidhi Dominika tena kwa Hispania kwa sababu aliamini ya kwamba nchi ilikosa nguvu ya kusimama peke yake. Lakini raia wengine walipinga kurudi kwa Wahispania na kwa msaada wa kijeshi wa Haiti Wahispania walilazimishwa kuondoka.

Jamhuri ya pili[hariri | hariri chanzo]

Jamhuri ya Dominika iliendelea kuwa nchi dhaifu. Kati ya miaka 1865 na 1879 serikali 21 zilihesabiwa pamoja na matukio ya uasi wa kijeshi 50.

Mwisho wa karne ya 19 rais Ulises 'Lilís' Heureaux alikopa pesa nyingi kutoka benki za Ulaya, lakini kutokana na kushuka kwa bei ya sukari alishindwa kulipa. Lakini nchi za nje zilidai pesa zilizokopwa.

Utawala wa Marekani[hariri | hariri chanzo]

Tangu Januari 1905 mamlaka ya ushuru ilichukuliwa na Marekani.

Wakati wa Vita vikuu vya kwanza Marekani ilivamia kisiwa chote cha Hispaniola, kwanza Haiti, halafu pia Jamhuri ya Dominika. Utawala wa Marekani uliendelea hadi mwaka 1930.

Udikteta wa Trujillo[hariri | hariri chanzo]

Kilifuata kipindi cha udikteta wa mkuu wa jeshi Rafael Leónidas Trujillo aliyechukua utawala kwa miaka 30 hadi kifo chake tarehe 30 Mei 1961. Alitawala kwa unyama na kupora mali ya umma.

Kipindi cha mapinduzi[hariri | hariri chanzo]

Rais Juan Bosch aliyefuata siasa ya ujamaa alichaguliwa tarehe 27 Februari 1963.

Matajiri na serikali ya Marekani walihofia ya kwamba atafuata mfano wa Fidel Castro nchini Kuba, akapinduliwa kwa msaada wa idara ya ujasusi wa Marekani CIA.

Kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe kilifuata hadi Umoja wa Mataifa ulipoingilia kati na kutuma wanajeshi wa kurudisha amani.

Hadi sasa[hariri | hariri chanzo]

Mnamo Juni 1966 Joaquín Balaguer, aliyewahi kuwa makamu wa rais Trujillo, alichaguliwa kuwa rais. Uchaguzi huo ulileta wasiwasi mwingi kama kura za baadaye.

Katika miaka iliyofuata Balaguer alirudishwa hadi mwaka 1978. Baada ya vipindi vya marais wengine, Balaguer alirudishwa tena miaka 1986, 1990 na 1994.

Kura za mwisho baada ya Balaguer ziliteua marais Leonel Fernández Reyna, Hipólito Mejía na tena Leonel Fernández Reyna tangu 2004.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Jamhuri ya Dominika kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.