Gedi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Maghofu ya msikiti
Kaburi la mwaka 1399 kati ya maghofu ya Gedi

Gedi (pia: Gede) ni kijiji cha wakazi 600 kwenye pwani la Kenya takriban kilomita 16 kusini ya Malindi. Ni mahali pa maghofu ya mji wa Waswahili wa Kale.

Gedi ya kihistoria[hariri | hariri chanzo]

Kando la kijiji cha leo kuna eneo kubwa la maghofu. Kuta za mawe zaonekana kati ya miti. Nyumba za watu, jumba la mkubwa -labda mfalme-, msikiti na makaburi huonekana vizuri. Mji wote ulikuwa na takriban ekari 45 na mabaki ya ukuta uliozunguka yote yaonekana hadi leo lakini nyumba nyingi zilikuwa za watu maskini zilizojengwa kwa kutumia udongo na ubao tu hazionekani tena.

Hakuna uhakika Gedi ya Kale ilianzishwa lini lakini wataalamu hukadiria umri wa nyumba za kwanza zinazopatikana mnamo karne ya 13/14. Kuna maandiko ya Kiarabu kwenye makaburi yanayosidia makadirio haya. Hakuna habari za kimaandishi juu ya mji kwa hiyo maarifa yote yametegemea matokeo ya akiolojia.

Inaonekana Gedi ilikuwa mji tajiri uliostawi kwa biashara. Kuna mabaki ya bidhaa kutoka Venezia (ushanga wa kioo), China (jagi ya kauri ya kipindi cha Ming),Uhindi (taa ya chuma) na Hispania (mkasi).

Idadi ya wakazi inakadiriwa kuwa hadi 2,500. Nyumba kubwa za matajiri zilikuwa na vyoo vya maji na bafu.

Mnamo karne ya 16 mji uliachwa na wakazi wake. Hakuna uhakika kuhusu sababu yake.

Maghofu ya Gedi yalitangazwa kuwa hifadhi ya taifa na siku hizi yatawaliwa na makumbusho ya Kenya.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]