Nenda kwa yaliyomo

Florence Nightingale

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Florence Nightingale

Florence Nightingale (12 Mei 182013 Agosti 1910) alikuwa muuguzi (nesi) mashuhuri kutoka nchini Uingereza.

Familia na mafunzo[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa mjini Firenze katika familia tajiri wakati wazazi walifanya safari ya Italia hivyo akapewa jina la Kiingereza la mji alikozaliwa yaani Florence.

Alipata elimu nzuri akifundishwa na baba yake nyumbani kwa sababu wakati huo hapakuwa na shule za sekondari kwa ajili ya wasichana wala nafasi ya kusoma kwenye chuo kikuu.

Florence alikataa kuolewa badala yake alisikia wito wa ndani kutoka kwa Mungu na kuanza kuwasaidia watu maskini na wagonjwa.

Alikwenda Ujerumani ambako ndiko alikojifunza kazi ya uuguzi kwenye taasisi ya Kilutheri ya diakonia ya Kaiserswerth akaendelea zake mjini Paris kwenye hospitali ya masista Wakatoliki.

Aliporudi Uingereza alipewa uongozi wa zahanati ndogo kwa ajili ya wanawake.

Vita ya Krimea[hariri | hariri chanzo]

Mwaka uleule wa 1853 magazeti ya Uingereza yalitoa taarifa juu ya hali ya askari waliojeruhiwa kwenye vita ya Krimea vilivyopigwa kati ya jeshi la Urusi kwa upande mmoja na jeshi la Milki ya Osmani, Uingereza na Ufaransa kwa upande mwingine. Ilikuwa vita vya kwanza vilivyoripotiwa na magazeti ya kisasa na taarifa juu ya mateso ya wajeruhiwa zilishtusha wasomaji huko Uingereza hasa kwa kwa sababu jeshi la Uingereza halikuwa na madaktari wala wauguzi wa kijeshi. Askari Wafaransa tu walipata msaada kutoka watawa wa shirika la Masista wa Huruma.

Hapo Florence Nightingale alijitolea pamoja na wauguzi wa kike 38 kwenda Krimea alipofika mwaka 1854 na kuwahudumia wajeruhiwa. Mara nyingi maafisa wakubwa wa jeshi walisikitika kwa sababu hawakupenda watu raia, tena wanawake, kujishughulisha na wanajeshi ,lakini Florence alipendwa na askari na sifa zake zilipelekwa Uingereza kwa njia ya magazeti.

Baada ya miaka mitatu aligonjeka mwenyewe akapaswa kurudi nyumbani.

Mwalimu na kielelezo wa uuguzi[hariri | hariri chanzo]

Hapo alianzisha chuo cha wauguzi na kwa njia hiyo aliongeza heshima ya kazi hii iliyowahi kutazamwa kama kibarua tu. Kwa njia hiyo aliweka msingi kwa ajili ya uuguzi wa kisasa.

Mswisi Henry Dunant aliguswa na habari za Florence Nightingale alipoanzisha shirika la Msalaba Mwekundu mwaka 1863. Serikali ya Marekani ilitafuta ushauri wa Florence wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani.

Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Florence Nightingale kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.