Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Eleanor Roosevelt akishika Tangazo kilimwengu la haki za binadamu (1949).

Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu[1] (pia: Tangazo la kilimwengu la haki za binadamu au Taarifa ya Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu[2], kwa Kiingereza: Universal Declaration of Human Rights) ni tamko la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu lililotolewa tarehe 10 Desemba 1948. Ilikuwa kati ya maazimio ya kwanza kabisa ya UM.

Msingi wa haki hizo uko katika kifungo cha kwanza kinachosema, "Watu wote wamezaliwa huru, wakiwa na hadhi na haki sawa. Wamejaliwa akili na dhamiri na kupaswa kutendeana kwa roho ya kidugu".

Haki zinaorodheshwa katika vifungu 30 vinavyoeleza haki za msingi ambazo kila mtu anastahili kuwa nazo "bila kubaguana kwa rangi, taifa, jinsia, dini, siasa, fikra, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine yoyote".

Haki zilizomo katika tangazo hili jinsi zilivyo si sheria ya kimataifa moja kwa moja, lakini zimekubaliwa na kila taifa lililojiunga na UM. Sehemu kubwa ya vipengele vyake imeingia katika mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiraia na kisiasa ya mwaka 1966 na mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ya mwaka 1976 na kwa njia hiyo zimekuwa sehemu ya sheria za kimataifa.

Mawazo ya msingi[hariri | hariri chanzo]

Mawazo ya msingi ya tangazo la haki za binadamu ni pamoja na:

 • kila mtu ana haki ya kuwa na uhai, uhuru na usalama.
 • kila mtu ana haki ya kupata elimu.
 • kila mtu ana haki ya kupata kazi.
 • kila mtu ana haki ya kufuata utamaduni wake.
 • kila mtu ana haki ya kutotendewa kinyama au kikatili.
 • kila mtu ana haki ya kuwa huru wa kutoa na kueleza maoni yake au kuchagua dini yake.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Azimio la UM si la kwanza katika historia kuorodhesha haki za binadamu. Mfano unaojulikana sana ni Tangazo la Haki za Kibinadamu na Kiraia lililotolewa na bunge la Ufaransa tarehe 26 Agosti 1789 wakati wa Mapinduzi ya Kifaransa.

Tamko la bunge la Ufaransa lilifuata katiba ya Marekani (4 Julai 1776) iliyotaja pia haki za msingi. Matangazo hayo yote mawili yanasimama kwenye msingi wa juhudi za falsafa ya zama za mwangaza katika karne ya 18, lakini mizizi yake katika ustaarabu wa Ulaya unategemea hadhi ya mtu kama sura na mfano wa Mungu katika imani ya dini ya Uyahudi na Ukristo.

Kanuni na maandishi kamili ya Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu [3][hariri | hariri chanzo]

Utangulizi[hariri | hariri chanzo]

Kwa kuwa kukiri heshima ya asili na haki sawa kwa binadamu wote ndio msingi wa uhuru, haki na amani duniani,
Kwa kuwa kutojali na kudharau haki za binadamu kumeletea vitendo vya kishenzi ambavyo vimeharibu dhamiri ya binadamu na kwa sababu taarifa ya ulimwengu ambayo itawafanya binadamu wafurahie uhuru wao wa kusema, kusadiki na wa kutoogopa cho chote imekwisha kutangazwa kwamba ndio hamu kuu ya watu wote,
Kwa kuwa ni lazima, ili mtu asishurutizwe kuomba msaada kutokana na maasi ya kupinga dhuluma na uonevu, kwamba haki za binadamu ziwe chini ya ulinzi wa sheria,
Kwa kuwa ni lazima kabisa kuendeleza uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa,
Kwa kuwa watu wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha tena katika Mkataba wao imani yao katika haki za asili, heshima na thamani ya binadamu na katika usawa wa haki kwa wanaume na wanawake, na kwa sababu wamekata shauri la kuendeleza mambo ya starehe na hali bora za maisha ya watu kwa kuwa na uhuru zaidi,
Kwa kuwa Nchi zilizo Wanachama zimeahidi, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, kukuza na kuheshimu haki za binadamu na uhuru wake wa asili,
Kwa kuwa kuzitambua haki hizi na uhuru huu ni jambo la maana sana kua kutimiza ahadi hiyo,
Kwa hiyo basi,
Baraza kuu linatangaza
Taarifa hii ya ulimwengu juu ya haki za binadamu kama ndio nguzo ya juhudi kwa watu wa mataifa yote ambayo hatimaye kila mtu na kila jamii ya watu - kwa kushikilia daima Taarifa hiyo - watajitahidi kufundisha jinsi ya kukuza heshima ya haki hizo na uhuru huo. Na mataifa yote yatajitahidi kuzifanya haki hizo zifahamike miongoni mwa Nchi zilizo Wanachama na miongoni mwa watu zinaowatawala.

Kifungu cha 1[hariri | hariri chanzo]

Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kindugu.

Kifungu cha 2[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu anastahili kuwa na haki zote za uhuru wote ambao umeelezwa katika taarifa hii bila ubaguzi wowote. Yaani bila kubaguana kwa rangi, taifa, wanaume na wanawake, dini, siasa, fikara, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine yoyote. Juu ya hayo usifanywe ubaguzi kwa kutegemea siasa, utawala au kwa kutegemea uhusiano wa nchi fulani na mataifa mengine au nchi ya asili ya mtu, haidhuru nchi hiyo iwe inayojitawala, ya udhamini, isiyojitawala au inayotawaliwa na nchi nyingine kwa hali na namna yoyote.

Kifungu cha 3[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu ana haki ya kuishi, haki ya uhuru na haki ya kulinda nafsi yake.

Kifungu cha 4[hariri | hariri chanzo]

Mtu yeyote asifanywe mtumwa au mtwana; utumwa na biashara yake ni marufuku kwa kila hali.

Kifungu cha 5[hariri | hariri chanzo]

Mtu yeyote asiteswe, asiadhibiwe, asidharauliwe au kutendewa kinyama au kikatili.

Kifungu cha 6[hariri | hariri chanzo]

Mbele ya sheria kila mtu ana haki ya kutambulika kama mtu.

Kifungu cha 7[hariri | hariri chanzo]

Mbele ya sheria watu wote ni sawa na wanastahili haki sawa za kulindwa. Wote wana haki sawa ya kulindwa kutokana na ubaguzi wowote unaoweza kuvunja taarifa hii na mambo yoyote yanayoweza kuleta ubaguzi huo.

Kifungu cha 8[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu ana haki ya kutetewa na baraza la hukumu kwa makosa ya kuvunjiwa haki zake za asili anazostahili kwa mujibu wa kanuni na sheria.

Kifungu cha 9[hariri | hariri chanzo]

Mtu yeyote asikamatwe, asifungiwe au kuhamishwa kutoka nchi yake bila sheria.

Kifungu cha 10[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu ana haki kamili ya kuhukumiwa vyema hadharani na baraza lililo huru na lisilo na upendeleo katika kutoa uamuzi wa haki zake na wajibu wake na wa makosa yoyote yanayo-mhusu.

Kifungu cha 11[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu anaeshtakiwa kwa kosa la kuvunja sheria ana haki ya kuangaliwa kama si mkosefu mpaka imethibitishwa kisheria, kwa kuhukumiwa hadharani, kwamba ana hatia.
 2. Mtu yeyote asitiwe hatiani kwa tendo lolote au jambo lolote halikupinga sheria ya taifa au ya kati ya mataifa wakati alipotenda. Wala asipewe adhabu kali zaidi kuliko ile iliyokuwamo katika sheria wakati alipofanya kosa.

Kifungu cha 12[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu asiingiliwe bila sheria katika mambo yake ya faragha, ya jamaa yake, ya nyumbani mwake au ya barua zake. Wala asivunjiwe heshima na sifa yake. Kila mmoja ana haki ya kulindaw na sheria kutokana na pingamizi au mambo kama hayo.

Kifungu cha 13[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu ana haki ya kwenda mahali anapotaka kuishi katika kila nchi.
 2. Kila mmoja ana haki ya kuhama kutoka nchi yoyote, hata nchi yake mwenyewe, na ana haki ya kurejea katika nchi yake.

Kifungu cha 14[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu ana haki ya kukimbilia na kustarehe katika nchi nyingine kwa ajili ya kuepukana na udhalimu.
 2. Haki hii haiwezi kuombwa kwa udhalimu ambao hautokani na makosa ya mambo ya kisiasa au na makosa ya maazimio na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Kifungu cha 15[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu ana haki ya utaifa
 2. Mtu yeyote asinyang’anywe utaifa wake bila sheria wala asinyimwe haki ya kubadili taifa lake kama akitaka.

Kifungu cha 16[hariri | hariri chanzo]

 1. Watu wazima, wanaume kwa wanawake wana haki ya kuoana na kuunda jamaa bila ya kizuio chochote kwa sababu ya rangi, taifa na dini. Wana haki sawa ya ndoa wakati wa maisha yao ya ndoa na wakati wa kutenguka ndoa.
 2. Ndoa inaweza kufungwa tu kwa hiari na mapatano kamili kati ya hao wanaotaka kuoana.
 3. Jamaa ni kiungo cha asili cha jamii ya watu, na inastahili kulindwa na watupamoja na serikali.

Kifungu cha 17[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu ana haki ya kuwa na mali yake binafsi au kwa kushirikiana na watu wengine.
 2. Mtu asinyang’anywe mali yake bila sheria.

Kifungu cha 18[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu ana haki ya uhuru wa mawazo, dhamira na dini; haki hii inahusu pia uhuru wa kubadili dini yake au imani, na uhuru wa kubainisha hadharani au faraghani -akiwa peke yake au na watu wengine- dini yake kwa kufundisha kwa vitendo, kuabudu na kwa kuadhimisha.

Kifungu cha 19[hariri | hariri chanzo]

Kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake; haki hii inahusu pia uhuru wa kushikilia maoni yake bila kuingiliwa kati na uhuru wa kutafuta na kutoa habari na moni kwa njiayoyote bila kujali mipaka.

Kifungu cha 20[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mkutano na chama kwa hali ya amani.
 2. Mtu yeyote asilazimishwe kuwa mwanachama wa chama fulani.

Kifungu cha 21[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mmoja anayo haki ya kushiriki katika serikali ya nchi yake yeye mwenyewe binafsi au kwa njia ya mjumbe aliyemchagua kwa hiari.
 2. Kila mmoja anayo haki sawa ya kufanya kazi katika serikali; matakwa hayo huonyeshwa katika uchaguzi halisi unaofanywa muda baada ya muda ambao kila mt hupiga kura na ambao hufanywa kwa kura ya siri na kila mtu hiari yake.
 3. Matakwa ya watu ndio yatakuwa msingi wa utawala wa serikali;hali itajidhihirisha kwenye chaguzi za haki kwa watu wote na ambazo zinafanyika kwa siri au namna nyingine ambayo itahakikisha uchaguzi kuwa huru.

Kifungu cha 22[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu, kama raia, anayo haki ya kutunzwa na anastahili kupata haki zinazotokana na uchumi, starehe na utamadun-ambazo ni lazima kwa hali bora na maendeleo ya nafsi yake-kwa njia ya juhudi ya taifa na ushirikiano kati ya mataifa na kwa mujibu wa utaratibu na utajiri wa kila nchi.

Kifungu cha 23[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu ana haki ya kufanya kazi, ya kuchagua kazi aipendayo, ya kuchagua yenye masharti mazuri na ana haki ya kulindwa asikose kazi.
 2. Kila mtu ana haki ya kupata mshahara sawa na wengine wenye kazi ya namna moja bila ubaguzi.
 3. Kila mfanyakazi anayo haki ya kupata mshahara wa kufaa na unaopendeza utakaomwezesha yeye mwenyewe pamoja na jamaa yake kuishi katika hali bora, na ahifadhiwe-ikiwa lazimamaisha yake kwa njia nyingine.
 4. Kila mtu anayo haki ya kuunda au kujiunga na chama chochote cha wafanyakazi kwa ajili ya kulinda haki zake za kazi.

Kifungu cha 24[hariri | hariri chanzo]

Kila mtu ana haki ya kupumzika na kufanya kazi kwa kiasi cha saa zinazostahili.Pia ana haki ya kupata likizo, kwa kipindi na kupokea mshahara kama vile angekuwa kazini.

Kifungu cha 25[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu anayo haki ya kupata hali bora ya maisha yeye mwenyewe pamoja na jamaa yake na kupata chakula, mavazi, nyumba, matibabu na hifadhi za lazima kwa maisha yake. Pia ana haki ya kutunzwa wakati wa kazi, wakati wa ugonjwa, wa kutojiweza, ujane, uzee au anapokosa riziki yake kwa kutoweza kujisaidia.
 2. Akina mama na watoto wanastahili kutunzwa na kupewa msaada maalum.Watoto wote-wawe wamezaliwa katika hali ya ndoa ama hapana-lazima watunzwe vyema.

Kifungu cha 26[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu ana haki ya kuelimishwa. Elimu yapasa itolewe bure hasa ile madarasa ya chini. Elimu ya madarasa ya chini ihudhuriwe kwa lazima. Elimu ya ufundi stadi iwe wazi kwa wote. Na elimu ya juu iwe wazi kwa wote kwa kutegemea sifa ya mtu.
 2. Elimu itolewe kwa madhumuni ya kuendeleza barabarahali ya binadamu, na kwa shabaha ya kukuza haki za kibinadamu na uhur wake wa asili. Elimu ni wajibu ikuze hali ya kuelewana, kuvumiliana na urafiki kati ya mataifa na kati ya watu wa rangi na dini mbalilmbali. Kadhalika ni wajibu iendeleze shughuli za Umoja wa Mataifa za kudumisha amani.
 3. Ni haki ya wazazi kuchagua aina ya elimu ya kufunzwa watoto wao.

Kifungu cha 27[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika maisha ya utamaduni ya jamii yoyote, na ana haki ya kufurahia ustadi wa kazi na kushiriki katika maendeleo ya mambo ya sayansi na faida zinazotokana nayo.
 2. Kila mtu ana ya kulindwa kwa kila hali kutokana na mambo ya sayansi aliyoandika, aliyochora au aliyogundua.

Kifungu cha 28[hariri | hariri chanzo]

Ni haki kila mtu alindwe na taratibu au kanuni za jamii na zinazohusu mataifa mbalimbali ambazo ndani yake uhuru na haki zilizoelezwa katika taarifa hii zinzweza kuhifadhiwa barabara.

Kifungu cha 29[hariri | hariri chanzo]

 1. Kila mtu ana wajibu kwa watu wa jamii yoyote ambao kati yao tu ndio yanaweza kupatikana maendeleo kamili ya hali ya maisha yake.
 2. Katika kutumia haki na uhuru wake, kila mtu itambidi kufuata kanuni zile tu zilizowekwa na sheria kwa ajili ya kulinda heshima inayotakiwa juu ya haki na uhuru wa watu wengine, na kwa ajli ya kuhifadhi kanuni za haki, usalama na hali njema ya maisha katika jamii ya kidemokrasia.
 3. Uhuru na haki hizi kamwe visitumiwe kinyume cha maazimio na kanuni za umoja wa mataifa.

Kifungu cha 30[hariri | hariri chanzo]

Hakuna maneno yoyote katika taarifa hii yanayoweza kubashiriwa kwamba yanaruhusu nchi yoyote, kikundi cha watu au mtu fulani kufanya au kushughulika na jambo lolote ambalo nia yake ni kuharibu haki na uhuru zilizoelezwa humu.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. linganisha [1] tangazo la UM kwa Kiswahili linalotumia umbo hili
 2. umbo kwenye tafsiri hili la UM
 3. "Matini ya azimio kutoka tovuti ya Tume la Haki za Binadamu Tanzania" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2012-03-02. Iliwekwa mnamo 2012-03-14.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya sheria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu kama historia yake au uhusiano wake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.