Ali Mufuruki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ali Mufuruki
Ali Abdul Mufuruki
Ali Abdul Mufuruki
Jina la kuzaliwa Ali Abdul Mufuruki
Nchi Tanzania
Kazi yake mhandisi mjasiriamali

Ali Abdul Mufuruki (15 Novemba 1958 - 7 Desemba 2019) alikuwa mhandisi, mjasiriamali na mfanyabiashara kutoka nchini Tanzania.

Elimu

Mufuruki alizaliwa mwaka 1958 Bukoba vijijini katika Mkoa wa Kagera.

Shule ya sekondari alimaliza vema katika masomo ya sayansi[1].

Katika miaka ya 1980 alijifunza Kijerumani akasomea uhandisi kwenye Chuo cha Uhandisi Reutlingen[2], Baden-Württemberg, Ujerumani alipohitimu masomo ya uhandisi mitambo (ubunifu) kwa shahada ya kwanza. Wakati wa masomo yake alikuwa mhandisi mkufunzi katika kampuni ya Daimler Benz iliyo karibu na Reutlingen.

Kurudi Tanzania

Baada ya kurudi Tanzania mwaka 1986 aliajiriwa katika kampuni ya National Engineering Co. Ltd. Mwaka 1989 aliondoka katika ajira akaanzisha kampuni yake ya Infotech Computers Ltd ambayo baadaye aliipanua ikawa Infotech Investment Group Ltd, aliyoendelea kuiongoza hadi kifo chake.

Mjasiriamali

Mufuruki aliwekeza katika biashara mbalimbali pamoja na kupata haki ya kutumia rajamu ya Woolworth kwa ajili ya maduka nchini Tanzania na Uganda (Dar es Salaam, Arusha na Kampala)[3] na kushiriki katika teknolojia ya habari pamoja na kampuni ya nyaya za intaneti[4].

Alichaguliwa kuhudumia kwenye bodi za shirika na makampuni mbalimbali za Afrika ya Mashariki na kimataifa, mara kwa mara akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi hizo. Makampuni haya ni pamoja na Vodacom Tanzania na Wananchi Ltd.[5]

Majadiliano kuhusu njia za Afrika

Mufuruki alilenga kujenga majadiliano baina ya viongozi wa sekta binafsi na viongozi wa siasa. Hapo alijulikana kwa mara ya kwanza mwaka 1996 alipochangia katika majadiliano kwenye ikulu ya rais Benjamin Mkapa[6]. Alitamka mara kadhaa kuwa tatizo kubwa la Afrika ni udhaifu wa viongozi wake.[7]

Mwaka 2016 alitoa kitabu kuhusu njia ya Tanzania kuhamia uchumi wa viwanda.

Kuaga Dunia

Kwenye Desemba 2019 aliugua na hivyo akapelekwa kwa ajili ya matibabu nchini Afrika Kusini alipoaga dunia tarehe 7 Desemba 2019 Jumamosi katika Hospitali ya Montnigside huko Johannesburg, Afrika Kusini [8] akiwa na umri wa miaka 61.

Aliacha mke wake Saada na watoto wanne.

Mufuruki kuhusu nafasi ya Kiswahili

Katika kitabu chake kuhusu Tanzania kuhamia uchumi wa viwanda, alisisitiza umuhimu wa lugha ya taifa akidokeza mfano wa mataifa kama Korea, Ujerumani, China, Norwei yanayofaulu ambayo yote hutumia lugha zao na kufundisha Kiingereza kama lugha ya kigeni tu.

"Tanzania inaweza kujivunia kuwa moja ya nchi chache za Kiafrika ambazo zimefaulu kutumia lugha asilia kama chombo cha kuwaunganisha watu wake katika jamii yenye nguvu na amani.

Lakini kuna ishara za kuleta wasiwasi kwamba athira ya Kiswahili kama msingi wa kuunganisha na chanzo cha fahari ya kitaifa imefifia. Ni dhahiri kuwa miaka mingi ya kutumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano haijaleta kutokea kwa utamaduni wa Kiswahili wa pamoja wenye nguvu kote nchini. Hii ni dhahiri tukitegemea kuona kutunga na kutafsiri kazi za fasihi, uchumi, biashara, historia, nk, kwa Kiswahili na kuhimiza utumizi mpana wa Kiswahili kati ya viongozi wa kisiasa na raia na kwa elimu rasmi, na katika uchumi. Badala yake tunaona Kiingereza kama ishara ya ujasusi; tunafikiria kuwa uchumi na falsafa na dhana za kiteknolojia zinaweza kusomwa kwa Kiingereza pekee. Tunajaribu kuendesha biashara zetu, shule na taasisi za utafiti kwa Kiingereza na viongozi wetu wa kisiasa hutumia Kiingereza wakati wajumbe wa kigeni hutumia lugha zao."[9]

Marejeo

  1. Doting father, husband and businessman, Mahojiano ya Mufuruki na gazeti The Citizen Archived 8 Desemba 2019 at the Wayback Machine.,tovuti ya Thecitizen.co.tz, 9 February 2014, iliangaliwa Desemba 2019
  2. Hochschule Reutlingen - University Reutlingen, tovuti rasmi
  3. W-stores company T-Ltd. Archived 8 Desemba 2019 at the Wayback Machine., tovut ya zoomtanzania.com, iliangaliwa Desemba 2019
  4. African millionaire Ali Mufuruki, (hitimisho ya shughuli zake), tovuti ya theafricanmillionaire.blogspot.com, iliangaliwa Desemba 2019
  5. (2019) Ali A. Mufuruki (kuhusu vyeo katika bodi mbalimbali mnamo 2019 Archived 8 Desemba 2019 at the Wayback Machine., tovuti ya philanthropyforum.org, ilitazamiwa Desemba 2019
  6. David Fick, Africa - Continent of Economic Opportunity, Real African Publishers, 1 Apr 2007 - pp 326 f, kupitia google books]
  7. Mufuruki's vision "Tanzanian executive pushes Africa’s leaders for “a better, more dignified life” Archived 8 Desemba 2019 at the Wayback Machine., tovuti ya compassmag.3ds.com, Compass magazin #15, iliangaliwa Desemba 2019
  8. Tanzanian dollar millionaire Ali Mufuruki dies in South Africa (en). The Citizen. Iliwekwa mnamo 2019-12-08.
  9. Ali A. Mufuruki, Rahim Mawji, Gilman Kasiga, Moremi Marwa, Tanzania’s Industrialisation Journey, 2016 – 2056, uk. 114