Mohandas Karamchand Gandhi
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mohandas Karamchand Gandhi (Kigujarati: મોહનદાસ કરમચંદ ગાંધી:2 Oktoba 1869 - 30 Januari 1948) anajulikana zaidi kwa jina la Mahatma Ghandi. Alikuwa mwanasheria, mwanafalsafa, mpiganaji wa haki za binadamu na kiongozi wa kisiasa nchini Uhindi. Anajulikana kama kiongozi wa harakati ya uhuru wa Uhindi aliyepinga na kushinda ukoloni bila matumizi wa silaha kwa njia ya amani.
Yaliyomo |
[hariri] Maisha
Ghandi alizaliwa katika eneo la Gujarat kama mtoto mdogo wa Karamchand Gandhi na mama Putali Bai. Babake alikuwa waziri mkuu katika serikali ya maharaja wa nchi lindwa ndogo ya Porbandar wakati ilikuwa sehemu ya Uhindi wa Kiingereza. Familia yake walifuata dini ya Uhindu dhehebu la Wavishnu lakini nyumba ya Ghandi ilitembelewa pia na Waislamu na Wajain.
Mwaka 1883 akiwa na umri wa miaka 13 aliozwa na mke wake Kasturba wakazaa watoto 4.
[hariri] Masomo katika Uingereza
1888 alisafiri Uingereza akasoma sheria kwenye chuo kikuu cha London akapokelewa kama wakili kwenye mahakama za juu kuanzia 1891.
Huko Uingereza alisoma mengi juu ya Ukristo akipendezwa hasa na mahubiri ya Yesu na hotuba mlimani. Lakini hakuvutwa na nafasi ya pekee Yesu anayopewa katika imani ya kikristo.
Wakati uleule alianza kusoma vitabu vitakatifu vya Uhindu mara ya kwanza hasa Bhagavad Gita iliyoendelea kuwa mwongozo wa kiroho maishani mwake.
[hariri] Afrika Kusini
Baada ya mtihani alirudi Uhindi akafanya kazi kama wakili mjini Bombay. 1893 alitumwa Afrika Kusini kwa kesi moja lakini alibaki huko hadi 1914.
Katika Afrika Kusini Ghandi alijenga falsafa yake akaanza kujishughulisha na maswali ya siasa na haki za binadamu. Alihamasishwa hivyo na maarifa ya ubaguzi. Ghandi alisimulia katika kitabu juu ya maisha yale ya kwamba siku chache baada ya kufika Afrika Kusini alisafiri kwa treni akishika tiketi ya daraja la kwanza. Abiria wazungu walilalamika juu yake akaambiwa kuhamia kwenye behewa la mizigo. Ghandi alikataa akaondolewa na polisi akabaki kituoni. Baadaye alipata maarifa nyingine alipofukuzwa katika basi kwa sababu mzungu aliyeingia alidai kiti kilichokaliwa na Ghandi.
Hivyo Ghandi alifungua ofisi katika Afrika Kusini mjini Durban kwenye jimbo la Natal akaanza kupigania haki wa Wahindi katika Afrika Kusini waliobaguliwa kwa sheria za nchi. Wakati ule Wahindi walikuwa raia wa Milki ya Kiingereza waliokuwa na haki zote wakifika Uingereza penyewe lakini katika Afrika Kusini iliyokuwa pia sehemu ya milki ya Kiingereza walibaguliwa kutokana na rangi yao.
1894 aliunda chama cha Natal Indian Congress akifuata mfano wa Indian National Congress huko Uhindi. Chama hiki kilidai haki sawa kwa Wahindi katika Afrika Kusini. Wakati wa Vita ya pili ya Waingereza dhidi ya Makaburu 1899 na vita dhidi ya Wazulu 1906 aliunda kikosi cha usaidizi kwa Waingereza wailiokusanya wajeruhiwa na kuwatunza kwenye mahospitali.
Mwaka 1906 serikali ya jimbo la Transvaal ilianzisha sheria iliyopasa Wahindi kujiandikisha na kubeba vitambulisho. Ghandi alipinga sheria hii akaongoza maandamano na mikutano ya kuchoma vitambulisho. Alihimiza wafuasi wake kukubali kupigwa na kuadhibiwa bila kutumia mabavu wenyewe. Katika miaka iliyofuata Wahindi maelfu walipigwa na polisi, walikamatwa na kunfungwa jela pamoja na Ghandi mwenyewe. Baada ya miaka saba watu wengi walisikitika matumizi ya nguvu dhidi ya Wahindi walioandamana kitulivu na serikali ilipaswa kupunguza ukali wa sheria.
[hariri] Falsafa ya Satyagraha
Katika miaka híi Ghandi alijenga falsafa yake ya upinzani bila silaha wala mabavu aliyotumia baadaye Uhindini.
Imani ya Ghandi iliathiriwa na mafundisho ya Ujain aliyojua tangu utoto wake na hasa dai la kututumia mabavu lakini kufuata njia za amani. Kiini chake kilikuwa satyagraha inayomaanisha "kusimama upande wa ukweli". Satyagraha kwake ilikuja pamoja na kutokuwa na uhasama na kutotumia nguvu. Alisema "Ukweli haukubali nguvu kwa sababu hakuna mtu mwenye ukweli wote kwa hiyo hakuna mwenye haki ya kuadhibu wengine."
Dhana nyingine ni "swaraj" inayomaanisha "kujitawala". Ghandi aliona swaraj kwa ngazi mbili:
- swaraj kama kujitawala kwa kila mtu akitawala tamaa zake
- swaraj kama haki ya watu kwa pamoja kujiamulia mambo yao na kutotawaliwa na nje kwa mfano na wakoloni
[hariri] Kiongozi Uhindini
Baada ya kugonjeka aliondoka Afrika Kusini 1914 akarudi Uhindini. Alipokelewa kama mshujaa kwa sababu habari zake zilimtangulia.
Aliunda makazi ya pamoja ya ashram alimoishi pamoja na watu waliofuata imani yake ya satyagraha. Alianza kuvaa nguo za wakulima wa kawaida.
1920 alikuwa kiongozi wa Indian National Congress akaanzisha kempeni ya kitaifa shidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza. Alihimiza Wahindi wengi kutotii sheria za serikali ya Kiingereza bila kutumia nguvu.
Mfano moja ni maandamano ya chumvi mwaka 1930. Sheria ya Kiingereza iliweka biashara yote ya chumvi mkononi mwa serikali. Kutengeza chumvi na kuiuza ilikuwa haki ya serikali iliyokabidhi haki hii kwa makampuni waliolipa kodi za pekee. Ghandi aliongoza watu maelfu baharini walichota maji ya bahari wakaichemsha na kupata chumvi kidogo kwa njia hiyo. Kiasi cha chumvi kilikuwa kidogo mno lakini walivunja sheria kwa kusudi. Waingereza walianza kuwakamata wapika chumvi lakini walishindwa na idadi kubwa ya watu waliokubali kukamatwa. Tena ilikuwa vigumu kuwahamasisha askari walioona kosa lilikuwa dogo sana na wakosaji hawakuwa hatari yoyote kwao.
Ghandi wenyewe alikamatwa mara kadhaa akaka jela jumla miaka 8.
Mwishowe watu wengi huko Uingereza walichoka habari za Uhindi na mwisho wa vita kuu ya pili ya dunia serikali mpya ya chama cha Labour iliamua kuipa Uhindi uhuru wake.
[hariri] Kipindi cha uhuru na ugawaji wa Uhindi
Ndani ya Uhindi mwenyewe fitina ilianza juu ya nafasi ya Waislamu katika taifa jipya na sehemu kubwa ya Waislamu walidai kugawiwa kwa koloni katika nchi mbili.
Mapigano yalianza na watu maelfu waliuawa. Agosti 1947 nchi mbili za Uhindi na Pakistan zilianzishwa na Oktoba 1947 vita vikafuata kati ya nchi zote mbili juu ya jimbo la Kashmir. Vita ikaongeza uadui na watu mamilioni walifukuzwa yaani Wahindu katika Pakistan na Waislamu katika Uhindi.
Gandhi alijitahidi kupatanisha viongozi wa pande zote akafunga chakula akitangaza alikuwa tayari kufunga hadi kifo wasipopatana. Heshima kwa Ghandi ilisababisha viongozi wa pande mablimbali katika Uhindi kukutana na kutafuta njia za kumaliza uhasama.
[hariri] Kifo
Tar. 30 Januari 1948 Gandhi alipigwa risasi na kuuawa alitembea katika bustani ya nyumba huko Delhi. Mwuaji wake walikuwa Mhindu na mfuasi wa kundi lililofuata siasa kali. Huyu kijana alikasirishwa na hatua za kupatanisha Waislamu na Wahindu akaamini Ghandi alikuwa msaliti wa Uhindu.
[hariri] Mahatma
Gandi alijulikana hasa kwa jina la Mahatma. Neno hili la Kisanskrit lamaanihsa "roho kubwa" akaitwa hivyo mara ya kwanza alipofika Bombay wakati wa kurudi kutoka Afrika Kusini. Ghandi hakupenda jina hili lakini alishindwa kuzuia matumizi yake.

