Yom Kippur

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Yom Kippur (kwa Kiebrania יוֹם כִּפּוּר  ' Siku ya Upatanisho ') ndiyo siku takatifu zaidi katika dini za Uyahudi na Usamaria. [1] [2] [3] Inatokea kila mwaka siku ya 10 ya mwezi wa Tishri ambao ni wa saba katika kalenda ya Kiyahudi.

Ni siku ya toba na maadhimisho yake yanajumuisha saumu kamili kwa saa 25, pamoja na sala na maungamo ya dhambi (kwa kawaida katika ibada ya sinagogi).

Pamoja na sherehe ya Rosh HaShanah, Yom Kippur ni mojawapo ya " Siku Takatifu Kuu " za Uyahudi.

Rosh HaShanah na Yom Kippur[hariri | hariri chanzo]

Yom Kippur ni "siku ya kumi ya [mwezi] wa saba" [4] ( Tishrii ) na Rosh Hashanah ni siku ya kwanza ya mwezi huo kulingana na kalenda ya Kiebrania. Siku kumi kati ya Rosh Hashanah na Yom Kippur zinajulikana katika Uyahudi kama Siku Kuu Takatifu au Yamim Nora'im ("Siku za Kustaajabisha"). [5]

Desturi za siku[hariri | hariri chanzo]

Tabia kuu ni kufunga chakula na kila kinywaji kuanzia kabla ya machweo hadi baada ya machweo kwa hiyo kwa saa 25.

Kanuni ya mafungo ya Yom Kippur ni pamoja na

  • Hakuna kula wala kunywa
  • Hakuna kuvaa viatu vya ngozi
  • Hakuna kuoga wala kuosha
  • Hakuna kujipaka manukato wala mafuta ya kujipaka
  • Hakuna mahusiano ya ndoa

Hapo wanashiriki pia Wayahudi wengi ambao vinginevyo hawafuati dini wala sheria zake. Yom Kippur ni siku ambapo wengi kati ya Wayahudi hao wasio wa kidini wanafika kwenye sinagogi na kushiriki katika ibada.[6]

Jioni[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya macheo ya Yom Kippur, waumini hukusanyika katika sinagogi. Sanduku la Torati linafunguliwa na watu wawili wanaochukua kutoka humo magombo mawili ya Torati. Kisha wakasimama pande zote mbili za Mwimbaji Mkuu. Wote watatu kwa pamoja huimba kwa Kiebrania:

Katika mahakama ya mbinguni na mahakama ya duniani, tunaona ni halali kuswali pamoja na wakosaji.

Kisha mwimbaji mkuu anaimba sala ya Kol Nidre (Kiaramu: כל נדרי "viapo vyote"). Jina lake "Kol Nidre" limechukuliwa kutoka maneno ya ufunguzi, na hutafsiri "viapo vyote":

Viapo vyote vya binafsi ambavyo tunaweza kufanya, viapo vyote vya binafsi na viapo ambavyo tunaweza kuchukua kati ya Yom Kippur hii na Yom Kippur ijayo, tunakanusha hadharani. Vyote viachwe, vibatilishwe na visiwe imara wala vya maana. Viapo vyetu binafsi, nadhiri na viapo vyetu vya hadharani vizingatiwe kuwa si nadhiri wala viapo. [7]

Kisha kiongozi na kusanyiko wanasema pamoja mara tatu "Watu wote wa Israeli wasamehewe, pamoja na wageni wote wanaoishi kati yao, kwa maana watu wote wana hatia." Magombo ya Torati huwekwa tena ndani ya sanduku, na ibada ya jioni ya Yom Kippur huanza. 

Talmud inasema, "Yom Kippur hupatanisha wale wanaotubu na haileti upatanisho kwa wale wasiotubu". [8] Toba katika Uyahudi inafanywa kupitia mchakato uitwao Teshuva, ambao katika hali yake ya msingi kabisa inajumuisha kujuta kwa kufanya dhambi, kuazimia kutotenda dhambi hiyo katika siku zijazo na kuungama dhambi hiyo mbele ya Mungu. Kuungama katika Uyahudi kunaitwa Vidui (Kiebrania וידוי). Pia kuna amri ya kutubu kwenye Yom Kippur. [9]

Wayahudi husoma Vidui kamili jumla mara tisa.

Tarehe ya Yom Kippur[hariri | hariri chanzo]

Yom Kippur huadhimishwa kila mwaka siku ya 10 ya mwezi wa Kiyahudi wa Tishri, ambayo ni siku 9 baada ya siku ya kwanza ya Rosh Hashanah. Kwa mujibu wa kalenda ya Gregori, tarehe ya kwanza kabisa ambayo Yom Kippur inaweza kuadhimishwa ni Septemba 14, kama ilivyotokea hivi majuzi mwaka wa 1899 na 2013. Yom Kippur inaweza kutokea kuhusiana na tarehe za Gregori hadi 14 Oktoba, kama ilivyotokea mwaka wa 1967 na itavyotokea tena mwaka wa 2043. [10]

Tarehe za kalenda ya Gregori kwa sikukuu za hivi karibuni na zijazo za Yom Kippur ni:

Mwaka wa Kiyahudi Mwaka wa Kalenda ya Gregori
5783 5 Oktoba 2022
5784 25 Septemba 2023
5785 12 Oktoba 2024
5786 2 Oktoba 2025
5787 21 Septemba 2026

 

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Festival 2016: Seven Festivals Celebrated in the Israelite Samaritan Year (en-GB). Israelite Samaritan Information Institute. Iliwekwa mnamo 2022-09-13.
  2. The Festival of Yom Kippur (The day of Atonement) (en-US). The Samaritans. Iliwekwa mnamo 2022-09-13.
  3. Afflicting the Soul: A Day When Even Children Must Fast - TheTorah.com. thetorah.com. Iliwekwa mnamo 2022-09-13.
  4. Numbers 29:7 HE
  5. The High Holidays. My Jewish Learning. Iliwekwa mnamo September 27, 2020.
  6. Cohen, S.M.; Eisen, A.M.: The Jew Within: Self, Family, and Community in America, p. 169. Indiana University Press, 2000. "For completely uninvolved Jews ... the question of synagogue attendance rarely arises. They are unlikely ever to consider the matter, except at Rosh Hashanha and Yom Kippur or to attend a bar or bat mitzvah." See also Samuel C. Heilman, Synagogue Life, 1976.
  7. Translation of Philip Birnbaum, from High Holiday Prayer Book', Hebrew Publishing Company, NY, 1951
  8. Yoma 85b.
  9. Maimonodes, Mishneh Torah, Laws of Teshuva 2:7
  10. Rosh HaShanah and the Gregorian calendar. Oztorah.com. Iliwekwa mnamo September 12, 2012.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]