Shingo ya nchi ya Panama

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ramani ya Panama.
Mahali pa shingo ya nchi ya Panama.

Shingo ya nchi ya Panama (kwa Kihispania Istmo de Panamá, kwa Kiingereza Isthmus of Panama) ni kanda nyembamba ya nchi kavu iliyopo kati ya Bahari Karibi upande wa kaskazini na Bahari Pasifiki upande wa kusini. Shingo ya nchi hii inaunganisha Amerika ya Kaskazini na Amerika ya Kusini.

Eneo hili liko ndani ya nchi ya Panama pamoja na kanda la Mfereji wa Panama.

Upana wa shingo ya Panama ni takriban kilomita 60 kwenye sehemu nyembamba.

Kutokea kwa shingo ya Panama[hariri | hariri chanzo]

Hadi miaka milioni 15 iliyopita sehemu mbili za Amerika zilikuwa mabara ya pekee yaliyotengwa na bahari[1].

Wakati ule mwendo wa gandunia ulisababisha kugongana kwa bamba la Karibi na bamba la Amerika ya Kusini na kutokea kwa volkeno kwenye tako la bahari. Volkeno hizo zilikua na kutokea juu ya uso wa bahari kama visiwa. Visiwa vilipanuka na hatimaye kuwa shingo ya nchi ya kuunganisha mabara yote mawili.

Umuhimu wa shingo ya Panama[hariri | hariri chanzo]

Kutokea kwa shingo ya Panama kulitenganisha maji ya Pasifiki na Atlantiki. Mikondo ya maji vuguvugu kutoka Karibi haikuweza tena kuendelea katika Pasifiki ikageuzwa na kuwa mkondo wa ghuba unaopeleka maji vuguvugu hadi Atlantiki ya Kaskazini na Mediteranea na hivyo kusababisha tabianchi ya Ulaya kuwa na mvua nyingi na jotoridi ya wastani.[2]

Shingo ya Panama ilikuwa pia kama daraja na tangu miaka milioni 3 hivi wanyama wa pekee waliowahi kutokea katika Amerika Kusini kutokana na hali yake kuwa kama kisiwa walianza kuvuka shingo ya Panama na kuingia kaskazini. Vilevile wanyama wa Amerika Kaskazini walianza kuenea kusini.

Shingo ya Panama kama njia kati ya bahari[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1501 Wahispania walifika Panama na Rodrigo Galván de Bastidas aliona hapa ndipo mahali ambako bahari mbili za Atlantiki na Pasifiki ziko karibu. Kwa hiyo baada ya kuanzisha utawala wa kikoloni Hispania ilianzisha barabara ya kusafirisha mizigo na watu kati ya pande mbili.

Mji wa Panama City ulianzishwa na kukua upande wa Pasifiki wa barabara hii ikiwa bandari muhimu.

Barabara hii ilikuwa njia fupi ya usafiri kati ya makoloni ya Hispania kwenye pwani ya magharibi ya Amerika Kusini na Ulaya. Njia nyingine ya hatari ilikuwa kupitia rasi Hoorn kwa jahazi iliyochukua muda mwingi.

Ugumu wa usafiri kwa barabara kwenye milima na misitu ya mvua ya Panama ulizaa mapema fikra za kujenga mfereji kati ya bahari mbili. Hii iliwezekana katika karne ya 20 tu.

Mwaka 1903 Marekani ilichochea na kusaidia waasi katika eneo la Panama kujitenga na Kolombia na kupata mkataba kutoka serikali huru mpya kuwa Marekani iliruhusiwa kujenga Mfereji wa Panama kuanzia 1904 hadi 1914 na kuitawala kama sehemu ya Marekani hadi mwaka 1999.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Kujisomea[hariri | hariri chanzo]

  • Mellander, Gustavo A.(1971) The United States in Panamanian Politics: The Intriguing Formative Years. Daville,Ill.:Interstate Publishers. OCLC 138568.
  • Mellander, Gustavo A.; Nelly Maldonado Mellander (1999). Charles Edward Magoon: The Panama Years. Río Piedras, Puerto Rico: Editorial Plaza Mayor. ISBN 1-56328-155-4. OCLC 42970390.

Seager, R. (2006) 'The Source of Europe’s Mild Climate.', American Scientist, 94(4), pp. 334.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]