Taarab
Taarab (pia: tarabu, taarabu) ni aina ya muziki ya Afrika ya Mashariki yenye asili yake katika utamaduni wa Waswahili. Neno lenyewe limetokana na Kiarabu "tarab" (طرب) linalomaanisha "uimbaji, wimbo".
Tabia za taarab
Taarab ni muziki wa Waafrika wa pwani uliopokea athira kutoka tamaduni nyingi, hasa muziki wa Waarabu na Wahindi. Kimsingi ni uimbaji wa mashairi unaofuata muziki wa bendi.
Bendi hizi hutofautiana kieneo: katika taarab ya Unguja vinanda vya kulingana na tarab za Kiarabu hupendelewa; katika taarabu ya Mombasa aina za ngoma ni muhimu; katika taarab ya Tanga gitaa inapendwa. Siku hizi vyombo vya kisasa vimetumiwa pia.
Historia
Neno "taarab" laaminiwa lina asili katika Unguja ambako mnamo 1870 Sultani Sayyid Bargash alialika kundi la wanamuziki kutoka Misri kuja Zanzibar walioleta uimbaji wao aina ya "tarab". Alipopenda muziki huu sultani alimtuma Mzanzibari Mohammed bin Ibrahim kwenda Misri ajifunze vyombo vya huku. Mohammed aliporudi alikuwa mwanashairi wa Sultani akaendelea kuwafundisha marafiki vinanda vyake. Pamoja waliunda kundi la Nadi Ikhwani Safaa linalosemekana ni bendi ya kwanza iliyotumia jina la "taarab".[1]. Kundi limeendelea hadi leo na kujulikana sasa kwa jina la "Malindi Taarab"[2].
Hata hivyo muziki wa Waswahili unaojulikana leo kwa jina la taarab lina asili ya kale kushinda jina hilo ambalo ni kawaida siku hizi. Kuna kumbukumbu kutoka Lamu ya muziki iliyoitwa "kinanda" iliyounganisha uimbaji pamoja na chombo cha kibangala na ngoma ndogo na waimbaji wake walihamia Zanzibar wakaitwa "taarabu" huko.
Taarab katika utamaduni wa Uswahilini
Katika utamaduni wa Waswahili taarab ilikuwa utamaduni wa pekee kwa sababu ilikuwa mahali pekee ambapo wanawake walifika kwenye jukwaa pamoja na wanaume na kuimba. Kwa sababu hiyo taarab imepingwa mara kwa mara na viongozi wa dini walioona aina kadhaa za taarab ni haramu, hazilingani na masharti ya Uislamu, hasa wakati wa mwezi wa Ramadhani na kama watu wanaanza kucheza.[3]
Miaka ya nyuma muziki wa taarab umesambaa hata barani, nje ya utamaduni wa Waswahili: unavuta wasikilizaji katika miji mikubwa kote Afrika ya Mashariki hadi Burundi na Rwanda.
Bendi mbalimbali zimeingiza vyombo vya kisasa vya muziki katika mtindo wao kama vile keyboard na gitaa ya umeme.
Taarab ya Tanga na asili ya Taarab ya kisasa (Modern Taarab)
Katika miaka ya 1950 wanawake tisa wa Tanga walijikusanya na kuanzisha kikundi cha kuimba walichokiita Raha til Fuad maana yake Raha ya Moyo. Akina mama hawa chini ya bibie aliyeitwa Mama Akida au aka Mama Lodi, waliendesha kikundi chao wakiwa wanaimba nyimbo za Siti Binti Sadi na tungo zao ambazo waliimba katika melody ya nyimbo za Kihindi zilizotamba wakati huo. Kundi hili liliendelea na kuanza kuruhusu wanaume kujiunga hasa wakiwa wapiga vyombo, akiwemo mtoto wa Mama Akida, Akida Jumbe hatimaye alijiunga na kundi hili kama mpiga accordion kwenye mwaka 1962. Kundi hili ambalo baadaye lilikuja kuitwa Young Noverty, liliendelea mpaka kukaweko na mgawanyiko uliozaa kundi la Shaabab Al Waatan.
Hapa ndipo kukaanza mtindo wa kuweko kundi pinzani jambo ambalo kwa njia ya ajabu sana likawa linadumu kiasi cha miaka kumi kumi. Miaka ya 1960 Young Noverty na Shabaab al Waatan, miaka ya 1970 Lucky Star Musical Club na Black Star Musical Club, miaka ya 1980 Golden Star Taarab na White Star Taarab, miaka ya 1990, Babloom Modern Taarab na Freedom Modern Taarab. Taarab ya Tanga ndo haswa inastahili kuitwa modern Taarab, kwani wao hawakufuata taarab ile iliyoletwa Zanzibar enzi ya Sultan Seyyid Barghash, makundi la taarab ya Tanga yalikuwa madogo na vyombo vyake vilikuwa pamoja na Gitaa la besi, gitaa la solo, drums bongos, akodion au kinanda, nyimbo zao zilikuwa fupi na si ndefu kama za Kizanzibari.
Nyimbo zilitegemea mipigo ya ngoma za asili za kumbwaya na chakacha na hata baadaye mitindo kama rumba, bossa nova ilitumika kama mapigo. Na Taarab ya Tanga ndio iliyoanzisha moto wa vikundi vya taarab Tanzania Bara. Moshi kulikuwa na New Alwatan, AzimioTaarab, na Blue Star Taarab , Arusha-Blue Star Taarab, Dodoma-Dodoma Stars, Kondoa –Blue Stars, Mbeya-Magereza Kiwira, Mwanza-Ujamaa Taarab, Bukoba wakiwa na Bukoba Stars, na muendelezo huu uliingia mpaka Burundi kutokana na mwanamuziki mmoja aliyejulikana kama Athmani Mkongo, alitoka Burundi na bendi yake kufika Tanga akawa mwanamuziki mahiri wa Taarab na hata kuipeleka kwao Burundi na kukaanzshwa huko vikundi kadhaa vya Taarab.[4]
Viungo vya nje
- Mifano ya muziki ya taarabu (audio)
- Mwambao.com juu ya "tarabu"
- Ntarangwi, Mwenda: A Socio-Historical and Contextual Analysis of Popular Musical Performance among the Swahili of Mombasa, Kenya; in: Cultural Analysis 2001, 2: 1-37, 2001 University of California
- Igobwa, Everett Shigenje: Taarab and Chakacha in East Africa, 2007 Ilihifadhiwa 23 Novemba 2008 kwenye Wayback Machine.
- Vikundi vya muziki vya Zanzibar Ilihifadhiwa 7 Aprili 2008 kwenye Wayback Machine.