Msikiti wa Sultan Ahmed

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Msikiti wa Sultan Ahmed

Msikiti wa Sultan Ahmed ni msikiti mashuhuri mjini Istanbul katika nchi ya Uturuki. Inajulikana pia kwa jina la "msikiti buluu" kutokana na rangi ya vigae vinavyopamba undani wake.

Msikiti huu ulijengwa kuanzia mwaka 1609 - 1616 kwa maagizo ya Sultani Ahmed I aliyetawala milki ya Osmani.

Ni msikiti mkuu wa Istanbul ukihesabiwa kati ya majengo mazuri na muhimu ya usanifu wa Kiosmani.

Muundo wa jengo[hariri | hariri chanzo]

Msanifu wake Mehmet Agha alikuwa mwanafunzi wa Mimar Sinan. Aliiga mfumo wake wa kimsingi akifunika ukumbi mkuu wa kati kwa kuba kubwa, na kando yake akaongeza kuba ndogo 6.

Ukumbi mkuu una umbo ambalo unakaribia mraba akiwa na mita 53 x 51. Kuba kubwa una kipenyo cha mita 23.5 na kufikia kina cha mita 43. Kuba kubwa linashikwa kwa tao nne zinazolala juu ya nguzo nene nne zenye kipenyo cha mita 5.

Ukumbi unapokea mwanga kwa madirisha 260 yenye vioo vya rangi.

Msikiti huo, yaani jengo la ibada, ulijengwa pamoja na majengo ya kando kama vile madrasa, hospitali na kaburi la sultani Ahmed I.

Geti kuu upande wa magharibi lina nyororo nzito juu ya nafasi ya kuingia. Kusudi lake lilikuwa kumlazimisha sultani kuinama kichwa chini akiingia msikitini juu ya farasi yake. Nyororo hii ilikuwa na kazi ya kuonyesha ya kwamba Mungu ni mkubwa kuliko mtawala.

Minara[hariri | hariri chanzo]

Msikiti huu una minara sita. Wakati wa ujenzi hii ilileta matatizo maana wakati ule msikiti wa Kaaba mjini Makka pekee ulikuwa na minara sita. Kwa hiyo sultani alishtakiwa kuonyesha majivuno makubwa mno akiupa msikiti wake minara sawa na Makka. Kwa hiyo sultani Ahmed I aliagiza mnara wa saba uongezwe huko Makk.[1]

Historia ya ujenzi[hariri | hariri chanzo]

Sultan Ahmed I aliamua kujenga msikiti huu kama jengo la toba baada ya kushindwa katika vita dhidi ya Dola Takatifu la Roma (Ujerumani-Austria). Mwaka 1606 Milki ya Osmani ilipaswa kukubali amani iliyomaliza malipo ya kila mwaka yaliyowahi kutolewa na kaisari wa Vienna.

Vita dhidi ya Uajemi iliyoanza baadaye ilienda pia vibaya na mwaka 1612 Waosmani walipaswa kurudishwa maeneo ya Kaukazi kwa Waajemi.

Ahmed aliamua kujenga msikiti wake karibu na Hagia Sofia (maabadi yaliyowahi kuwa kanisa kuu la Konstantinopoli na kubadilishwa kuwa msikiti baada ya uvamizi wa Waturuki) na juu ya mabaki ya ikulu ya makaisari wa Bizanti na pia juu ya sehemu ya uwanja wa shindano la farasi wa Bizanti.[2]

Picha[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Nakala iliyohifadhiwa. Jalada kutoka ya awali juu ya 2014-10-13. Iliwekwa mnamo 2014-07-29.
  2. http://www.bluemosque.co/history.html

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons