Mashirika ya kilimwengu
Mashirika ya kilimwengu ni mashirika yaliyokubaliwa na viongozi wa Kanisa Katoliki kwa waamini (wenye daraja takatifu au la) wanaojisikia wito wa kushika mashauri ya Kiinjili kama watawa, lakini si lazima kwa kuishi kijumuia.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Tangu mwanzo wa Kanisa kulikuwa na Wakristo walioshika maisha ya useja na pengine walianzisha jumuia.
Kufuatana na mifano ya Yesu Kristo na Bikira Maria, Agano Jipya linatoa habari za wanaume na wanawake waliojinyima ndoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu, kama vile mabinti wanne wa Filipo waliokuwa mabikira na manabii (Mdo. 21:9). Hasa mtume Paulo aliwahimiza Wakristo wowote wanaoweza wafanye hivyo kama alivyofanya mwenyewe kwa kufuata shauri la Bwana (taz. 1Kor 7:25-34).
Mababu wa Kanisa kuanzia karne I waliandika juu ya wanaume waseja wanaozungukazunguka ili kuhubiri, na juu ya mabikira ambao utakatifu wao unaonyesha Ukristo ulivyo bora kuliko ulimwengu wa anasa unaoliudhi Kanisa.
Nje ya Dola la Kirumi (Mesopotamia na Persia) useja ulitazamwa kama agano na Kristo la kuwafaa wote.
Polepole mabikira walianza kuorodheshwa na kukubaliwa na askofu na kukusanywa katika jumuia. Ilitokea vilevile kwa wanaume wa toba walioanzisha miundo kamili kuliko juhudi za nyumbani mwao, wakishika ufukara fulani wa hiari, mafungo, kujinyima vyakula mbalimbali, kukesha usiku, kuimba Zaburi na kusali kwa moyo.
Karne XX, ngumu kwa Kanisa na kwa dunia yote, ilileta mang’amuzi mapya hasa katika maisha ya ulimwenguni. Kwa mara nyingine walei walichangia sana hali mpya ndani ya Kanisa Katoliki, ya kuthamini na kushughulikia mambo ya kidunia.
Katika juhudi za kuratibu nyanja zote za maisha ya binadamu, baadhi walijisikia haja ya kuwekwa wakfu bila ya kujitenga na maisha ya kawaida.
Polepole Kanisa likafikia uamuzi wa kuwakubalia (1950) mashirika ya kilimwengu ambayo waamini wanawekwa wakfu wawe chumvi, mwanga na chachu kati ya watu. Hivyo wanajitahidi kuwa na moyo wa kujikana na bidii ya kitume kama watawa, lakini pia utaalamu wa kisasa na urahisi wa kupenya mazingira yoyote kama walei.
Takwimu
[hariri | hariri chanzo]Idadi ya wanashirika inazidi kupungua, hasa kutokana na hali ya Italia, iliyokuwa inaongoza duniani kwa wingi wa miito.
Mwaka | Jumla | Afrika | Amerika | Asia | Oceania | Ulaya | (Italia) |
1990 | 31.419 | 451 | 4.757 | 892 | 47 | 25.272 | ...... |
1998 | 30.772 | 378 | 5.610 | 1.200 | 49 | 23.535 | 13.395 |
2000 | 30.687 | 444 | 5.780 | 1.457 | 45 | 22.961 | 11.911 |
2003 | 29.607 | 513 | 5.963 | 1.486 | 46 | 21.599 | 10.796 |
2004 | 28.942 | 528 | 6.043 | 1.527 | 44 | 20.800 | 10.404 |
2005 | ..... | ..... | ..... | ..... | .. | ...... | 10.080 |
2006 | ..... | ..... | ..... | ..... | .. | ...... | 9.514 |
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Annuario Pontificio per l'anno 2007, Città del Vaticano, Libreria Editrice Vaticana, 2007. ISBN 978-88-209-7908-9.