Nenda kwa yaliyomo

Panya manyoya-marefu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Lophiomyinae)
Panya manyoya-marefu
Panya manyoya-marefu
Panya manyoya-marefu
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Rodentia (Wanyama wagugunaji)
Nusuoda: Myomorpha (Wanyama kama panya)
Familia: Muridae (Wanyama walio na mnasaba na mabuku)
Nusufamilia: Lophiomyinae
Jenasi: Lophiomys
Milne-Edwards, 1867
Spishi: L. imhausi
Milne-Edwards, 1867
Msambao wa panya manyoya-marefu
Msambao wa panya manyoya-marefu

Panya manyoya-marefu (Lophiomys imhausi) ni mnyama mgugunaji wa nusufamilia Lophiomyinae katika familia Muridae anayetokea Afrika ya Mashariki.

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Mwili wa panya manyoya-marefu unaweza kukua hadi urefu wa sm 36 au sm 53 pamoja na mkia. Kuna manyoya marefu yenye ncha nyeusi au za fedha juu ya koti ya malaika kama sufu iliyo nzito, ya kijivu na nyeupe. Uso na miguu ina manyoya mafupi meusi. Arufu ya manyoya marefu na magumu zaidi yaliyo na miviringo myeusi na myeupe inakwenda kutoka kichwa hadi juu ya msingi wa mkia. Arufu hiyo inapakana na ukanda mpana wa manyoya meupe yanayofunika eneo la ngozi ya tezi. Nyayo za mbele ni kubwa na kidole 1 kina ukucha mfupi tu huku vidole 2-5 vikiwa na kucha ndefu zilizopindika.

Wakati paka huyo anapotishwa au kuchochewa arufu inasimama ikifichua ngozi ya tezi. Ncha za manyoya katika eneo hili ni ya muundo wa kawaida, lakini vinginevyo manyoya hayo ni kama sifongo yenye nyuzi na uwezo wa kufyonza kiowevu na yana muundo wa sega. Panya huyo anajulikana kupakia manyoya hayo kwa makusudi sumu kutoka kwa gome la msunguti, Acokanthera schimperi, ambalo hutafuna, na hivyo kuunda utaratibu wa ulinzi unaoweza kuugua au hata kuua mbuai wanaojaribu kumwuma. Ni mamalia pekee anayejulikana kutumia na kuhifadhi sumu kutoka kwa spishi tofauti ili kujikinga bila athari yoyote kwake inayoripotiwa.

Chakula[hariri | hariri chanzo]

Chakula cha panya huyo porini kinajumuisha majani, matunda na dutu ingine ya mimea, lakini anajulikana kula nyama, nafaka, mboga za mizizi na wadudu akiwa kifungoni. Chakula huliwa kwa kuketi kitako na kutumia miguu yake ya mbele kuleta vitu vya chakula mdomoni. Ni spishi pekee katika familia ya juu ya Muroidea ambayo tumbo lake lina vichumba vingi. Tumbo lina sehemu tano tofauti za kimaumbile ambazo zinafanana kijuujuu na mpangilio wa mifuko wa artiodactili wanaocheua. Kwa sababu ya saizi na biomasi yake kubwa panya manyoya-marefu ni labda mmojawapo wa panya wachache wa Muroidea ambao wanaweza kuwa na mikroflora ndani ya utumbo wa mbele na kufaidika kimetaboliki kutoka kwa uchachukaji wa selulosi katika utumbo.

Makazi[hariri | hariri chanzo]

Makazi ya panya manyoya-marefu yanaenda kutoka kwa karibu na usawa wa bahari huko Ethiopia na Somalia hadi misitu mikavu na misitu wazi ya nyanda za juu ya Somalia, Ethiopia, Sudani, Tanzania, Uganda na Kenya. Mabaki ya visukuku yamepatikana hadi kaskazini mwa Israeli hata hivyo. Mara nyingi hupatikana katika maeneo yenye miamba au katika mashina ya miti yenye uwazi na mashimo kando ya vilele vya mabonde na pia wamepatikana wakiwa wamejenga viota kati ya miamba kwenye nyuso za majabali.

Uzazi[hariri | hariri chanzo]

Panya manyoya-marefu aliaminika kukaa peke yake, lakini sasa anajulikana kuwa wa kijamii kiasi, na wanyama kadhaa wamenaswa katika eneo moja. Hukoroma na kusafishana, kwa hivyo inawezekana kama wanaunda vikundi vya familia ya dume, jike na uzao. Ukubwa wa mkumbo ni 1-3. Wachanga wana manyoya machache wakati wa kuzaliwa na mabaka meupe na milia myeusi huonekana mwilini baada ya siku 9. Kufikia siku ya 13 macho hufunguliwa. Manyoya ni marefu ya kutosha ili ushungi unaweza kusimama kwa siku ya 20. Wachanga huanza kutembea-tembea kwa siku ya 23 na huachishwa kunyonya kwa siku ya 40.