Kreta
Kwa kisiwa kinachoitwa Kreta kwa lugha ya Kigiriki, ona hapa Krete

Kreta (pia kasoko, kwa Kiingereza: crater) ni uwazi kwenye ardhi uliotokana na mlipuko au mshtuko wa kugongwa na gimba.
Kreta ina umbo la duara; katikati ni kama shimo na ukingo wake unainuliwa juu ya uwiano wa mazingira yake. Duniani kreta zinapatikana mara nyingi kutokana na milipuko ya volkeno au milipuko mingine. Kwenye sayari au miezi yenye uso thabiti kuna kreat nyingi kama matokeo ya kugongwa na magimba kutoka anga-nje. Kwa mfano kwenye Mwezi wa Dunia kuna kreta nyingi zilizosababishwa na migongano ya asteroidi. Pigo la kitu kigumu linarusha mata iliyopo mahali pa mgongano ikae pembeni ya shimo hilo kwa umbo la ukingo wa mviringo.
Duniani kreta zilizosababishwa na mishtuko ya aina hiyo husawazishwa baada ya muda fulani kutokana na mmomonyoko unaosababishwa na mvua na upepo; kwenye magimba pasipo angahewa kama Mwezini zinabaki kwa muda mrefu.
Kuna aina mbalimbali za kreta:
- kreta ya mlipuko, kwa mfano wa bomu lililolipuka ndani ya ardhi au juu ya uso wa ardhi
- kreta ya dharuba (mgongano) kutokana na kugongwa kwa uso la gimba na gimba nyingine, kwa mfano kama Dunia, sayari nyingine au Mwezi imegongwa na meteoridi au asteroidi
- kreta ya volkeno: shimo ambako zaha (lava) inatoka nje au iliwahi kutoka nje
Kreta kubwa zaidi duniani zilisababishwa na asteroidi zilizogonga Dunia yetu. Kreta kubwa iliyojulikana hadi mwaka 2006 ilikuwa kreta ya Vredefort nchini (Afrika Kusini) yenye umbo la yai la urefu wa km 320 na upana wa km 180.
Mwaka 2006 wataalamu waligundua kreta kubwa zaidi yenye kipenyo cha km 500 huko Antarktika katika picha zilizopigwa kutoka angani. Iko chini ya barafu ya Antarktika katika eneo la Wilkes Land inatajwa kwa kifupi cha WLIC (ing.: Wilkes Land impact crater). Kasoko ya WLIC inaaminiwa imesababishwa na asteroidi yenye kipenyo cha takriban km 5.
Kreta ya tatu kwa ukubwa ni kreta ya Chicxulub, Yucatan, Meksiko.
Picha[hariri | hariri chanzo]
-
Kreta ya Tycho mwezini kutokana na dharuba ya kimondo
-
Kreta kutokana na milipuko ya bomu za kinyuklia chini ya ardhi kwenye eneo la jaribio la Marekani huko Nevada
![]() |
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kreta kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |