Kalenga
Kalenga ni kata ya Wilaya ya Iringa Vijijini katika Mkoa wa Iringa, Tanzania, yenye Postikodi namba 51201.
Katika sensa iliyofanyika mwaka 2022 wakazi walihesabika kuwa 11,491 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 6,963 waishio humo.[2] Msimbo wa posta ni 51201.
Hadi mwanzo wa ukoloni Kalenga ilitwa pia "Iringa"; baada ya Wajerumani kuanzisha "Iringa Mpya" (Neu-Iringa) mahali pa mji wa leo, waliita mahali asilia "Iringa ya Kale" (Alt-Iringa)[3].
Kalenga-Iringa na historia ya mtemi Mkwawa
[hariri | hariri chanzo]Kalenga ilikuwa makao makuu ya Mtemi Mkwawa[4] aliyeongoza upinzani wa Wahehe dhidi ya ukoloni wa Kijerumani katika miaka ya 1891 - 1896.
Huko Kalenga Mkwawa aliwahi kujenga boma imara ya mawe baada ya kujifunza kuhusu uenezi wa Wajerumani kutoka sehemu za pwani. Boma hii liliitwa Lipuli. Ujenzi ulianza mnamo 1887 ukachukua miaka minne. Mji wote ulijulikana kama "Iringa" maana jina hili linataja mahali palipozungukwa na ukuta[5].Kalenga-Iringa ilikuwa na sehemu mbili zilizotengwa na mto; upande wa kulia wa mto uliitwa "Unguja", upande wa kushoto "Bagamoyo". Mwaka 1891 kila sehemu ilikuwwa na msimamizi wake walioitwa Ngozingozi na Mtemiuma, waliuawa kwenye mapigano wa Lugalo[6].
Baada ya kushindwa kwa jeshi la Kijerumani la Schutztruppe katika mapigano ya Lugalo mwaka 1891, Wajerumani walirudi kwa nguvu zaidi wakashambulia Lipuli - Kalenga kwenye Oktoba 1894 kwa silaha kali kama mizinga na bombomu.
Mkwawa alifaulu kukimbia wakati wa kutekwa kwa boma akaendesha vita ya msituni hadi kujiua mwaka 1898 alipoona hatari ya kukamatwa ilhali alijeruhiwa vibaya. Inasemekana Wajerumani walikata kichwa chake na kutuma fuvu lake Ujerumani.
Baada ya kushindwa kwa Ujerumani katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, washindi, hasa Uingereza, walisisitiza fuvu lirudishwe: hivyo kuna fungu 246 katika Mkataba wa Versailles linalotaja fuvu la Mkwawa. Wajerumani walidai baadaye kuwa wanashindwa kulikuta, hivyo walichelewa hadi baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia wakati jeshi la Uingereza lilipokuwa na utawala juu ya sehemu ya Ujerumani ya kwamba Waingereza waliteua fuvu moja katika mkusanyiko wa Makumbusho ya Bremen na kulituma Tanganyika kama fuvu la Mkwawa.
Kalenga kuna makumbusho kwa heshima ya Mtemi Mkwawa na fuvu hilo linahifadhiwa humo tangu kurudishwa mwaka 1954.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ https://www.nbs.go.tz
- ↑ Sensa ya 2012, Iringa Region- Iringa District Council
- ↑ Kamusi ya Koloni za Kijerumani (1920), makala "Iringa", online hapa (jer.) Archived 25 Machi 2016 at the Wayback Machine.
- ↑ Fungu "Kalenga" kwenye Mkwawa.com, iliangaliwa Machi 2017
- ↑ Glauning (1898) uk. 47; Glauning (aliyekuwa afisa wa jeshi la Kijerumani alitaja pia miji mingine iliyoitwa "Iringa" kama ilizungukwa na ukuta, kwa mfano Utengule wa Mtemi Merere wa Usangu
- ↑ [Nigmann (1908), uk 16-17]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- *Glauning, Hans: Uhehe; Berlin, 1898 (Verhandlungen der Abteilung Berlin-Charlottenburg / Deutsche Kolonialgesellschaft, Electronic Edition Bremen : Staats- und Universitätsbibliothek, 2018, URN urn:nbn:de:gbv:46:1-15493)
- Nigmann, Ernst: Die Wahehe, ihre Geschichte, Kult-, Rechts-, Kriegs- und Jagd-Gebräuche; Berlin : Mittler, 1908; (Online hapa)
Kata za Wilaya ya Iringa Vijijini - Tanzania | ||
---|---|---|
Idodi | Ifunda | Ilolompya | Itunundu | Izazi | Kalenga | Kihanga | Kihorogota | Kising'a | Kiwere | Luhota | Lumuli | Lyamgungwe | Maboga | Magulilwa | Mahuninga | Malengamakali | Masaka | Mboliboli | Mgama | Migoli | Mlenge | Mlowa | Mseke | Nyang'oro | Nzihi | Ulanda | Wasa |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Iringa bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Kalenga kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |