Jua

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 18:29, 8 Desemba 2015 na Riccardo Riccioni (majadiliano | michango) (Masahihisho aliyefanya 188.64.240.39 (Majadiliano) yalirejeshwa hadi sahihisho la mwisho na Riccardo Riccioni)
Jua

Jua ni nyota ambayo ni karibu na dunia yetu kuliko nyota nyingine. Jua ni kitovu cha mfumo wa jua likizungukwa na sayari nane. Dunia yetu ni moja ya sayari hizo katika mfumo wa jua na sayari zake.

Umbo la jua linakaribia tufe kamili. Maada yake ni utegili yaani gesi ya joto sana inayoshikwa na nguvu ya kisumaku.

Kipenyo cha jua ni takriban kilomita 1,392,684 ambayo ni mara 109 kipenyo cha dunia yetu. Masi yake ni mara 330,000 masi ya dunia.

Kikemia masi ya jua ni hasa hidrojeni (73%) na heli (25%). Kiasi kinachobaki ni elementi nzito zaidi, kama vile oksijeni, kaboni, chuma na nyingine. Hata kama hizi elementi nzito ni asilimia ndogo tu za masi ya jua, bado zinalingana na mara 5,000 masi ya dunia kutokana na ukubwa wa jua.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa jua liliundwa takriban miaka bilioni 4.57 iliyopita kutoka katika gimba kubwa la mawingu lililoundwa na asilimia kubwa za hidrojeni.

Jua linatoa mwanga, joto na mnururisho mwingine wa aina mbalimbali. Asili ya nishati hii ni mchakato wa myeyungano wa kinyuklia ndani yake. Katika myeyungano huo hidrojeni inabadilishwa kuwa heli. Elementi nyingine zinatokea pia kwa kiasi kidogo. Badiliko kutoka hidrojeni kwenda heli inaachisha nishati inayotoka kwenye jua kwa njia ya mnururisho.

Nishati ya mnururisho huu ni msingi wa maisha ya mimea na viumbe hai katika dunia. Nuru ya jua inabadilishwa na mimea kwa njia ya usanisinuru kuwa nishati ya kikemia inayojenga miili yao itakayokuwa lishe tena ya mimea na wanyama.

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Jua kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.