Nenda kwa yaliyomo

Joseph Makama Kusaga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Joseph Makama Kusaga

Joseph M. Kusaga
Maelezo
Majina ya utani Big Joe, Joe, Boss Joe, Biggy
Majina mengine Joseph Makama Kusaga
Umri Miaka 57
Tarehe ya kuzaliwa 9 Juni, 1966, Musoma, Tanzania.
Mtaalam wa Uhandisi
Kazi yake Mwekezaji, mjasiriamali.
Ndoa Mke mmoja
Utaifa Mtanzania

Joseph Makama Kusaga (maarufu kwa majina ya Big Joe, Biggy na Boss Joe; alizaliwa mkoani Mara, Tanzania, 9 Juni 1966) ni mwekezaji wa Tanzania mwenye maono ya kupigiwa mfano ya ujasiriamali wa kikampuni, anayefahamika kwa uasisi wake wa Clouds Entertainment Limited (sasa Clouds Media Group) kwa kushirikiana na aliyekuwa mbia na rafiki yake mkubwa, hyt. Ruge Mutahaba. [1] [2]

Maisha ya udogoni na elimu

[hariri | hariri chanzo]

Katika familia ya watoto 9 wa mzee Kusaga (wa kabila la Wakurya), Joe ni wa nne. Aliondoka Musoma na kuhamia Dar Es Salaam akiwa na umri wa miaka mitano kufuatia kuhamishwa kwa baba yake ambaye alikuwa mtumishi wa umma.[3] Aliendelea na masomo akiwa Dar katika shule za [msingi na sekondari] Muhimbili, Forodhani na Mzizima. Katika ngazi ya elimu ya juu, alisomea uhandisi wa umeme.[4] Kabla ya kuibuka na kuwa Joe anayefahamika hivi sasa, kichocheo cha awali kilikuwa kupenda kwake sana muziki na burudani wakati akisoma shule. Hali hiyo ilitanabaisha ukweli kuwa Joe alikuwa "upande wa mwenge wa shilingi" na baba yake alikuwa upande wa "kichwa" (Baba yake alipenda muziki na burudani sawa na Joe).

Kuanza kwake kuendesha shughuli za muziki na burudani katika umri mdogo huku akiwa chuoni, kulikubaliwa na wazazi wake japo kwa tahadhari. Walikuwa ni aina ya wazazi wasaidiao kufanikisha ndoto za mtoto.[5] Katika jitihada zake za mwanzo kabisa za kuendesha discotheques na boogies (matamasha ya muziki ya muda wa mchana), Joe alifuga kuku kujipati mtaji na aliazima vifaa vya kielektroniki vya familia.

Kutokana na kipaji na kukubalika kwake kama Dj na mpanga matamasha, Joe alipata mafanikio makubwa. Alifanya matamasha kwenye kumbi zote maarufu za Dar na mashabiki walimpachika majina kuashiria kuwa yeye ni mfalme wa tasnia. Baada ya mafanikio hayo, akajiwa na wazo la kufanya ziara nchini Marekani. Huko ndiko alikopata wazo la kuanzisha kituo cha redio kadhalika alikutana na rafikiye wa kuliana yamini, Ruge Mutahaba.[6] [7]

Kampuni na miradi

[hariri | hariri chanzo]

Kampuni ya kwanza kufunguliwa na Joe katika ubia na Ruge, ni Clouds Entertainment Limited mwaka 1998.[8] Miradi iliyokuwa chini ya kampuni hiyo ni pamoja na Clouds Disco na ule wa uratibu wa matamasha. Joe wa wakati huo ni yule Dj Emperor, pia 'Kinta Kinte'. Mwaka huohuo CloudsFm Radio (The peoples' station - Redio ya watu) ilianzishwa. "CLOUDS" ni finyanzo la "Cool, Lovable, Outrageous, Dynamic Sound." Joe anafunguka kwenye mahojiano na CloudsFm (Desemba 4, 2024);

Uanzishwaji wake ulikuwa mgumu kulingana na mazingira yale ambapo mamlaka zilizoea ukiritimba wa redio mbili nchini (RTD na iliyokuwa Radio One Stereo, sasa Radio One, ya IPP Media). Kufanikiwa kuisajili kulikuja kutokana na maono ya mbali ya uliokuwa uongozi wa TCC (sasa TCRA). Tulianza na frequency ya chini ya 90 (88.5 Dar Es Salaam) na ndani ya wiki 2 tuliwateka mashabiki wa Dar en masse.

Mwaka 2013 Joe alilifanyia ukarabati jina la kampuni na kuwa Clouds Media Group (sasa inavuma kama "Gen C" ) , (kutoka Clouds Entertainment Ltd). Kwa sasa kampuni hiyo ina takriban wafanyakazi 400, ina stesheni za redio 3 Tz na zingine zipo nje, stesheni za Tv 9, chaneli za kidijitali, chombo cha uchapishaji, mkongo wa Tv wenye chaneli 50, ushauri wa kitaalam kuhusu utangazaji, nk.[9] Kama ilivyo kwa CloudsFm upande wa redio, Clouds Tv iliyoanza rasmi 2010 inasikika zaidi.[10]

Joseph Makama Kusaga ameweka wazi falsafa yake ambayo ndiyo msingi wa mafanikio yake. Inajengwa kwa nguzo kuu tatu: Kufanya anachokipenda, Kumakinika na anachokifanya na Nidhamu kwenye utendaji. Nguzo hizo hujengwa na makunzi (materials) yafuatayo: kuifuata jamii na si kulazimisha jamii imfuate, kwenda na wakati kiteknolojia na ufundi, elimu na ujuzi bila ukomo, mipango na mikakati bora, azma ya mafanikio zaidi, kuwa wa mfano, kurejesha kwa jamii, kukua, kazi kitaalamu, upendo, heshima na kukataa fitina na rushwa [11]

Kurejesha kwa jamii

[hariri | hariri chanzo]

Chini ya uongozi wa Joe, CMG imerejesha kwa namna mbalimbali kwa jamii:

  • Fursa: ni mradi ulobuniwa na hyt. Ruge Mutahaba na kubarikiwa na Joe. Kuanzia mwanzoni mwa 2010, CMG imefanya kazi kubwa sana kuuelimisha umma wa Watanzania jinsi wanavyoweza kuzitumia fursa zinazowazunguka kujikwamua kiuchumi. Chini ya kaulimbiu za "tunakufungulia dunia," "kuwa unachotaka, "wewe ni mpanbanaji" na kadhalika, CMG imerejesha kwa jamii kupitia elimu ya bure ya ujasiriamali.[12][13]
  • Malkia wa nguvu: ni programu maarufu ya CMG ya Joe inayojielekeza katika kuwawezesha wanawake.[14] Huchechemua juhudi za wanawake katika uzalilishaji na ubunifu. Programu hii ni uso mpya wa iliyokuwa Mwanamakuka.
  • Ajira: Jumla kuu ya walioajiriwa CMG (wakati wote) inapindukia 400. Wengi waliajiriwa, wakawa maarufu na weledi na kuhamia kwingine.
  • Kuibua vipaji: Sifa kuu za kuajiriwa CMG ni akili, kipaji na uwezo wa kazi kivitendo. Watu kadhaa wasio watangazaji kwa kusomea wameibuka kuwa wabeba kampuni huku wakipata taaluma zaidi kazini. Hali kadhalika matamasha ya Fiesta na kazi za Prime time promotions vimechangia pakubwa tasnia ya sanaa na wasanii.[15]
  • Elimu kwa umma: Kila siku ni ya kozi za kielimu kupitia CMG: afya, amali, siasa, uchumi, lugha, muziki, biashara, jamii, nk. Yote yanajiri chini ya uongozi wa Joe Kusaga.

Mafanikio

[hariri | hariri chanzo]

Kutoka kuwa Dj na mwandazi wa matamasha hadi Mkurugenzi wa kampuni ya kimataifa iliyo mbioni kuweka hisa zake kibiashara kwenye soko la hisa, ni hatua kubwa. CMG ya Joe sasa imetapakaza nyayo zake maeneo mbalimbali duniani kama vile Jamaica, Abu Dhabi, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na kwingine[16] Muziki wa Bongo fleva ulikubalika katika hatua zake za awali kwa juhudi za Joe na CMG.

Umashuhuri wa Joe uligonga kwenye anga za kimataifa zaidi ya miaka 15 iliyopita. Jarida maarufu duniani la Forbes lilimtafuta na kufanya nae mahojiano akiwa ni mwafrika wa kwanza kuhojiwa nao kadhalika kupamba jalada la jarida hilo kwa picha yake. Pia Joe aliweza kuwaleta wasanii wafuatao Tz na kuishangaza Afrika: Eve, Fat Joe, P Square, Shaggy, 50 Cent, Kevin Lyttle, Koffi, Jay Z - kwa kuishirikisha MTV Base, Ja Rule, Hugh Masekela, Mya, Miriam Makeba, Youssou N’Dour na wengine.[17]

Mafanikio yake yanaakisiwa pia kwa kuwaibua nguli wengi wa utangazaji kama: Reuben Ndege, Sebastian Maganga, Paul James, hyt. Gardner G. Habash, hyt. Ephraim Kibonde, hyt. Amina Chifupa, hyt. Fred Fidelis (Fredwaa), Ibrahim Masoud, Phina Mango, Masoud Kipanya, Ray C., Barbara Hassan, Dina Marios, B. Dozen, Gerald Hando, Regina Mwalekwa, Millard Ayo, Geah Habib, Husna Abdul, Jose Mara, Fatma Ahmed (fettylicious), Caesar, Mussa Hussein, George Bantu, Adam Mchomvu, Alex Luambano, Masta Tindwa, Mbwiga Mbwiguke, Prisca Kishamba, Amri Kiemba, Loveness Diva, Zamaradi Mketema, Sofia Kessy, Mahija Zayumba, Mo Jay, Mamy Baby, Vido Vidox, Meena Ally, Kennedy The Remedy, John Jackson, Frida Amani ... Wote wanam-verify Joe[18] [19] [20]

Maisha binafsi

[hariri | hariri chanzo]

Joe ana mke (mama watoto wake) na watoto.[21] Maisha yake ni ya Kitanzania na anamudu kuweka mboga saba mezani.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
  1. https://www.jamiiforums.com/threads/historia-ya-joseph-kusaga.1748466/
  2. https://www.jifunzeujasiriamali.co.tz/2019/03/siri-kubwa-2-za-mafanikio-ya-ruge.html
  3. https://www.jamiiforums.com/threads/historia-ya-joseph-kusaga.1748466/
  4. https://tanzania.mom-gmr.org/en/owners/individual-owners/detail/owner/owner/show/joseph-m-kusaga/
  5. https://tanzania.mom-gmr.org/en/owners/companies/detail/company/company/show/clouds-entertainment-co-limited-1/
  6. https://www.jamiiforums.com/threads/historia-ya-joseph-kusaga.1748466/
  7. https://tanzania.mom-gmr.org/en/owners/companies/detail/company/company/show/clouds-entertainment-co-limited-1/
  8. https://www.jifunzeujasiriamali.co.tz/2019/03/siri-kubwa-2-za-mafanikio-ya-ruge.html
  9. https://tz.linkedin.com/company/clouds-media-group
  10. http://tanzania.mom-gmr.org/sw/vyombo-vya-habari/det
  11. https://www.slideshare.net/slideshow/clouds-media-profile/70251617?searchfrom=header&q=Clouds+Media+
  12. https://media.bongoexclusivetv.com/marissa-maina-kuwa-unachotaka-clouds
  13. https://www.instagram.com/cloudsfmtz/reel/DDSbiVRM6Pg/
  14. https://www.instagram.com/cloudsfmtz/p/C4Xf6yPNKmI/
  15. https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/magazines/the-beat/fredwaa-radio-is-all-about-creativity-2520846
  16. https://www.slideshare.net/slideshow/clouds-media-profile/70251617?searchfrom=header&q=Clouds+Media+
  17. https://www.forbesafrica.com/entrepreneurs/2011/10/01/ear-for-profits/
  18. https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/magazines/the-beat/fredwaa-radio-is-all-about-creativity-2520846
  19. https://www.wikiwand.com/en/articles/Clouds_FM
  20. https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/clouds-wagoma-kulihamisha-tamasha-la-fiesta-2941132
  21. https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/mke-wa-kusaga-na-diamond-wamiliki-wasafi-televisheni-2941498