Ruge Mutahaba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rugemalila Mutahaba
Amezaliwa Ruge Mutahaba
1 Mei 1970
Brooklyn, New York, Marekani
Amekufa 26 Februari 2019 (miaka 49 )
Afrika Kusini
Nchi Tanzania
Majina mengine Ruge
Kazi yake Mwanzilishi-mwenza wa Clouds Media Group
Cheo Mkurugenzi wa vipindi Clouds Media Group
Chama cha kisiasa Chama Cha Mapinduzi
Dini Mkristo
Ndoa Hakufunga
Rafiki Joseph Kusaga
Watoto 5


Ruge Mutahaba (Alizaliwa Brooklyn, New York, Marekani, 1 Mei 1970 - Alifariki Afrika Kusini, 26 Februari 2019) alikuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Vipindi wa Clouds Media Group nchini Tanzania.[1][2]

Elimu[hariri | hariri chanzo]

Ruge ni Mtoto wa kwanza wa profesa Gelase Mutahaba na Christina Mutahaba, Ruge alipata elimu yake ya shule ya msingi mkoani Arusha darasa la kwanza hadi la sita, kisha akahamia Shule ya Msingi Mlimani ambako alihitimu elimu yake ya msingi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani mkoani Dar es salaam na kuhitimu kidato cha nne, na kidato cha sita katika shule ya sekondari Pugu. Alihitimu shahada ya Masoko kisha Shahada ya Sanaa katika Uchumi Chuo Kikuu cha San Jose huko Kalifornia, Marekani[3]

Taaluma[hariri | hariri chanzo]

Aliporejea Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha San Jose cha California (Marekani) ambako alihitimu masomo yake, Ruge alianza kutambulika kwenye jamii baada ya kuanza kufanya kazi na rafiki yake Joseph Kusaga ambaye alikuwa akiendesha Klabu yake ya usiku almaarufu kama disko iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Clouds Disco. Ushirikiano wao ulipelekea kuanzishwa kwa Clouds Media Group mjini Arusha ambayo, licha ya kuwa chombo cha habari na burudani kwa jamii, hasa vijana, ilifanya kazi ya kuhamasisha vijana wadogo wa Kitanzania kujiingiza katika kutafuta fursa na ujasiriamali ili kujiinua na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla wake.[3] Tokea maisha ya utotoni Ruge alikuwa mpenada muziki, lakini kipaji chake hakikuwa kwenye muziki peke yake. Alikuwa mchezaji mpira wa miguu (soka), alipewa majina mengi kwa kipaji hicho akicheza timu za mtaani, za Chuo Kikuu kuanzia Adanco na Summer Rangers na alifikia hatua ya kuchaguliwa katika timu ya mkoa wa Dar es salaam ya UMISETA. Pia alikuwa na kipaji cha kuandika. Vipaji vingine vyote havikuweza kunawiri kwani alikuwa na mapenzi na muziki zaidi.

Familia[hariri | hariri chanzo]

Ruge Mutahaba hakuwahi kufunga ndoa rasmi lakini alikuwa na mahusiano na Zamaradi Mketema[4] na walipata watoto wawili.[3] Pia alizaa wengine watatu na kufanya jumla ya watoto watano(5)[5]

Maradhi na kifo[hariri | hariri chanzo]

Ruge Mutahaba alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na tatizo la figo, Ruge alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, ambayo pia rais wa Jamhuri ya Tanzania John Magufuli alimchangia shilingi milioni hamsini [6], hadi mauti yalipomfika tarehe 26 Februari 2019.[2][7][8]

Watanzania wengi waliopokea habari za kifo chake, akiwemo Rais John Pombe Joseph Magufuli[7], walishtushwa na habari za mauti yake na kutuma jumbe za kuguswa kutokana na mchango mkubwa wa Ruge katika tasnia ya habari na burudani, ubunifu katika mipango mikakati, kuendeleza vipaji vya vijana wa Tanzania, kuhamasisha ari ya ufanyaji kazi kwa bidii katika jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.[2]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Ruge Mutahaba (16 August 2017). Jalada kutoka ya awali juu ya 2019-02-27. Iliwekwa mnamo 26 February 2019.
  2. 2.0 2.1 2.2 Ruge Mutahaba afariki dunia, Rais Magufuli amlilia. Iliwekwa mnamo 26 February 2019.
  3. 3.0 3.1 3.2 Ruge Mutahaba Biography, Career, Family (12 February 2018). Jalada kutoka ya awali juu ya 2019-02-27. Iliwekwa mnamo 26 February 2019.
  4. "Zamaradi Mketema", Wikipedia, kamusi elezo huru (in Swahili), 2019-04-30, retrieved 2019-12-28 
  5. https://www.mwananchi.co.tz/habari/Makala/Familia-ya-Ruge-nje-ya-Mutahaba/1597592-4995480-9i1ld1/index.html iliangaliwa tar 15 Machi 2019
  6. https://www.jamiiforums.com/threads/rais-magufuli-atoa-dola-20-000-kusaidia-matibabu-ya-ruge-mutahaba-mkurugenzi-wa-cmg.1511074/page-8
  7. 7.0 7.1 Tanzania: Clouds Media Group programmes director Ruge Mutahaba dies in South Africa. Iliwekwa mnamo 26 February 2019.
  8. TANZIA: Ruge Mutahaba afariki Dunia! Rais Magufuli aungana na Watanzania kuomboleza. Iliwekwa mnamo 26 February 2019.
People.svg Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ruge Mutahaba kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.