Chuo cha Kikristo cha Aleksandria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Chuo cha Kikristo cha Aleksandria (au Shule ya Elimu ya Kikristo ya Aleksandria) katika karne za kwanza BK kilikuwa kimojawapo kati ya vituo vikuu viwili vya elimu ya Kikristo na kati ya vyuo vya kwanza vilivyofundisha imani ya Kikristo kwa namna ya kitaalamu. Wakati wa Mababu wa Kanisa teolojia na ufafanuzi wa Biblia ya Kikristo vilivyotolewa huko vilitofautiana na Shule ya Antiokia. Majina ya vituo vyote viwili yalitokana na majiji vilipostawi katika Ukristo.

Wakati wanateolojia wa Antiokia ya Siria (leo nchini Uturuki) walifuata zaidi maneno yenyewe ya Biblia, wale wa Aleksandria (Misri) walipenda zaidi kuifafanua kiroho. Matokeo ya tofauti hizo yalijitokeza katika teolojia kuhusu fumbo la Yesu Kristo yakasababisha mafarakano makubwa ya karne ya 5.[1]

Kadiri ya Jeromu shule ya Aleksandria ilianzishwa na Mwinjili Marko. Baadaye anatajwa Athenagora wa Athene (176), lakini kwa hakika zaidi Panteno 181, aliyeacha uongozi kwa mwanafunzi wake bora, Klementi wa Aleksandria mwaka 190.[2]Huyo alifuatwa na Origene akiwa na umri wa miaka 18 tu, na wataalamu wengine wanaoheshimiwa kama watakatifu katika Kanisa la Kiorthodoksi na Kanisa Katoliki kama Gregori Mtendamiujiza, Heraklas, Dionisi wa Aleksandria na Didimo Kipofu.

Ilipoanzishwa kusudi lake lilikuwa kuwaelimisha Wapagani waliotafuta habari za imani mpya ya Kikristo kabla ya ubatizo. Chuo cha Aleksandria kikaendelea haraka kuwa kitovu cha elimu ya Kikristo na majadiliano kati ya imani ya Kikristo na falsafa ya Kigiriki iliyostawi sana Aleksandria, mji mkuu wa Misri wakati huo.

Ni kwamba kabla ya Misri kutwaliwa na Dola la Roma wafalme Watolemayo wa Misri waliwahi kuunda maktaba maarufu ambayo huaminiwa kuwa wakati wake ilikuwa maktaba kubwa zaidi duniani yenye vitabu 700,000. Kwa hakika ilikuwa maktaba kubwa kote Afrika, Ulaya na Asia ya Magharibi. Hii ilikuwa na thamani kubwa kupita kiasi wakati ambako vitabu viliandikwa na kunakiliwa kwa mkono tu, na hivyo kuwa haba. Aleksandria ilikuwa kitovu cha elimu na uchunguzi wa kitaalamu duniani.

Chuo kikastawi mwanzoni katika vipindi ambako Wakristo hawakuteswa katika Misri, kikaona matatizo mazito wakati wa madhulumu.

Tangu mwaka 311 uhuru wa dini ulitangazwa na Kaisari Konstantino Mkuu katika Dola la Roma na mateso ya Wakristo yalikwisha.

Chuo cha Aleksandria kikaendelea kutembelewa na wataalamu Wakristo kutoka pande zote za nchi za kandokando ya Mediteranea, kwa mfano Basili na Jeromu.

Kilibomolewa katika fujo zilizofuata Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381).

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Cross, F. L., ed. The Oxford Dictionary of the Christian Church. New York: Oxford University Press. 2005
  2. Cross, F.L.; Livingstone, E.A., eds. (1974). "Clement of Alexandria, St.". The Oxford Dictionary of the Christian Church (2 ed.). Oxford: Oxford University Press.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Chuo cha Kikristo cha Aleksandria kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.