Nenda kwa yaliyomo

Historia ya Wapare

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Wapare ni kabila kutoka milima ya Pare, Mkoa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa nchi ya Tanzania.

Lugha yao ni Kipare (au Chasu).

Asili ya Waasu

[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya kuingia huko, inasemekana walikuwa Taveta, Kenya, kwa zaidi ya karne moja iliyopita na wakati huo walikuwa wakijulikana kwa jina la Waasu.

Masimulizi yanasema walipoingia Tanganyika, walitamani kufanya makao yao kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro, lakini wakavurumishwa na wenzao waliokuwepo kabla yao, yaani Wachagga.

Wachagga hao hawakuwa radhi kuwaruhusu Wapare kuwa na makazi eneo hili, hivyo waliwafukuza kwa kupigana kama ilivyokuwa tabia ya makabila mengi hapo zamani.

Asili ya neno Wapare

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa kupambana walikuwa wakiambiana, “mpare… mpareee” wakimaanisha "mpige sana… mpige!" Waasu hawa wakatimka mbio na kuparamia milima ambayo sasa inaitwa milima ya Upare. Waasu wakaanza kuitwa Wapare kwa maana ya "wapige".

Hata hivyo huo ni utani wa Wachaga kwa Wapare, na ilivyotokea muingiliano wa maana ya neno hilo (coincidence) kwamba kulitokea vita kati ya Wachaga na Wapare, na neno hilo la Kichaga "Mpare" likawa na maana ya mpige, basi watani hao wakasema wao ndio waliotoa jina la kabila la Wapare.

Hizi ni hadithi zinazosimuliwa na baadhi ya Wachagga ambao ndio watani pekee wa Wapare, utani uliozaliwa baada ya purukushani hizo za kuingia Tanganyika.

Hata hivyo, hakuna hata Mpare mmoja anayeafiki maelezo hayo, isipokuwa wanakiri kuwa walitokea Taveta: ndiyo maana hata baadhi ya maneno na lafudhi yao haviko mbali sana na maana halisi ya neno Wapare: watu wa Taveta.

Kutokana na tafiti za lugha na matamshi mbalimbali, inasemekana matamshi ya neno la Kipare "mb" hubadilika na kuwa "p" katika Kiswahili. Kwa mfano Mbengo, kwa Kiswahili ni Pengo. Neno Mbinga, kwa Kiswahili ni Pinga. n.k. Hivyo neno Pare linatokana na neno "mbare", likiwa na maana ya kabila, au Mkabila au hata mara nyingine aina - katika kutofautisha aina za vitu (kwa Kiingereza "Classification"). Kwa mfano unaweza kusema mbuzi hawa ni "mbare ani"? Hivyo Wapare walijiita "Vambare" wakiwa na maana ya "sisi wa kabila moja, tunaoongea lugha ya Chasu". Hapo ndipo neno Vambare linabadilika katika Kiswahili na kuwa Wapare.

Tukumbuke katika lugha ya Kipare pia wanatambua makabila mengine kama Vashamba (Wasambaa); Vaagha (Wachaga); Vambughu (Wambugu); Vakwavi (Wamasai); Vakizungo (Wahaya); Vakamba (Wakamba); Vajaluo (Wajaluo) na wale ambao hawatambuliki kwa makabila yao huitwa Vanyika (au Mnyika kama ni mmoja). Wachaga nao wanalo neno linalofanana na hilo linaloitwa "Chasaka".

Wapare wamegawanyika katika makundi mawili makubwa; wapare wa Pare ya Kusini ambao ni Wapare wa Same na Wapare wa Pare ya Kaskazini ambao ni Wapare wa Mwanga ambao nao wamegawanyika mara mbili: Wapare wa Ugweno (wanatumia lugha inayoitwa Kigweno) na Wapare wa Usangi (wanatumia lugha inayofahamika zaidi kama Kipare ambayo inatumiwa pia na Wapare wa Pare ya kusini ingawa inatofautiana kidogo katika matamshi).

Wapare wanatokea katika wilaya za Same na Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, lakini pia wapo katika wilaya ya Moshi Vijijini sehemu za Kahe, Chekereni, Himo, Mabungo, Moshi mjini, tena katika wilaya ya Hai sehemu za Rundugai na mto Weruweru. Wapare pia wanaishi katika wilaya ya Lushoto, sehemu za Mgwashi, Mavumo, Lukozi, Shume na Makose.

Wapare wanasemekana wametoka katika nchi ya Kenya sehemu za Taita, Taveta na Ukamba. Wapare ni miongoni mwa makabila ambayo watu wake wamesoma sana. Wapare pia ni kabila la watu wanaopenda haki (yaani hawapendi kuonewa wala kumuonea mtu). Ndiyo maana watu wengine wanadhani wanapenda kesi, bali kesi ni njia mojawapo ya kuhakikisha haki inatendeka katika jamii. Dhuluma kwa Wapare ni kitu kilichokuwa kimepigwa marufuku hata kwenye matambiko yao, japo siku hizi kuna uwezekano baadhi yao wakawa hawana sifa hii tena.

Zamani Wapare walikuwa na sala tofauti kwa kila ukoo na eneo lao la tambiko. Katika karne ya 19 hadi 20 wamisionari wa Ukristo waliingia maeneo mengi ya Upare.

Imani za Wapare kwa sasa zinatofautiana kutokana na maeneo: walio kusini mwa wilaya ya Same katika maeneo ya Ndungu, Kihurio, Bendera, Hedaru, Makanya, Suji, Chome, Tae, Gonja, Mamba hadi Vunta kuna waumini wa kanisa la Sabato wengi sana.

Maeneo kama Chome, Mbaga, Gonja, Vudee, Usangi yana waumini wengi wa Kanisa la Kilutheri.

Katika Wilaya ya Mwanga kuna idadi kubwa ya Walutheri na Waislamu.

Wakatoliki, japo ni wachache, wanapatikana zaidi katika maeneo ya Kilomeni, Kisangara Juu, Vumari, Gonja, Kighare na Mbaga. Ukatoliki uliingia Upare kwa mara ya kwanza katika kata ya Kilomeni mwaka 1909.

Shughuli za uchumi

[hariri | hariri chanzo]

Jamii za Wapare zimegawanyika katika makundi ya wafugaji na wakulima. Wakati wafugaji wengi walihamia katika tambarare za Upareni, wakulima wao waliishi milimani na wafuaji wa vyuma walikaa maeneo yote yaliyokuwa na uwezekano wa kupata chuma.

Kwa asili Wapare hupeleka vijana wa kiume jando (mshitu) ambako walipata mafunzo jinsi ya kuishi na familia, japo siku hizi utamaduni huo hufuatwa na watu wachache.

Hata hivyo Wapare wa Mwanga wamegawanyika katika jamii mbili: Wasangi na Wagweno. Wakati Wasangi wanaongea Kipare kinachoongelewa pia na Wapare wa maeneo mengine, Wagweno wao wana lugha yao iitwayo Kigweno. Kigweno ni mchanganyiko wa Kipare na Kichagga. Hii inaonesha kuwa asili ya Wagweno ni huko Uchaga. Hata hivyo mila na desturi za Wagweno zinafanana zaidi na zile za Wapare wengine.

Wapare ni wachapakazi sana wakichanganya kilimo, ufugaji na biashara, ndiYo maana hata leo wana uchumi mzuri katika viwango vya Tanzania.

Wapare walianza kufua chuma kabla ya mwaka 1700 na wafuaji walikuwa wakiitwa Washana, na huo ukoo upo hata leo hii. Wapare walikuwa wakiuza bidhaa zinazotengenezwa na chuma kama majembe,mapanga, visu, silaha kama mikuki kwa makabila ya jirani mfano Wachaga,na wamekuwa na uhusiano tangu siku nyingi. Bidhaa zao hizi ziliuzwa hata kwa Wasambaa.

Mfumo wa maisha

[hariri | hariri chanzo]

Inasemekana Wapare ni kabila lenye ujasiri na ni watu wa kupanga kabla ya kutenda. Pia ni wavumilivu wenye kustahimili hali ngumu ya maisha ikiwa ni pamoja na njaa au kutokuwa na pesa.

Zamani za ukoloni waliweza kuungana na kufanya mgomo wa kukataa kodi zilizokithiri. Mgomo huo uliofanikiwa ulijulikana kama ‘mbiru’.

Kati ya mila na desturi zilizowajengea Wapare taratibu za kuwa na mifumo ya maisha kuna zile walizoziita ‘Ndala’, ‘Msaragambo’ na ‘Kiwili’.

Neno ‘ndala’ kwa Kipare humaanisha utaratibu wa familia au watu wanaoishi jirani mno kuwa na tabia ya kula chakula kwa pamoja, kama wengi tuonavyo waislamu waliofunga na wanapofuturu pamoja.

Utaratibu wa Wapare ulikuwa kwamba kila mama anapotayarisha chakula kwa familia yake, ilibidi akitoe achanganye na chakula kingine cha wenzake na familia zote ziketi na kula pamoja. Mfumo wa ndala kwa maana ya familia kula chakula kwa pamoja unaonekana kuwa na manufaa yafuatayo.

Kwanza unajenga mahusiano mema baina ya familia na majirani katika kushirikiana. Pili kushirikiana katika kula kunachochea ushirikiano katika mambo mengine kama shida au raha.

Lakini pia watoto wanaokuzwa katika mfumo huo wanajengwa katika maadili mazuri wasiwe walafi na wachoyo maana wanazoea kuwa na wenzao na hii ndiyo sababu kabila hili lilikuwa na sifa ya kuwa wakarimu.

Watoto walifundishwa kuwa na nidhamu ya wakati wa chakula, kwa mfano kutonawa mikono au kuanza kula kabla ya wakubwa.

Msaragambo

[hariri | hariri chanzo]

Neno msaragambo linamaanisha mfumo uliokubaliwa na jamii katika kitongoji, kijiji au kata wa kushirikiana katika kufanya kazi zenye faida kwa watu wote, maarufu kwa kazi za ujenzi wa taifa.

Kwa kazi hizi ni za ridhaa zilipaswa kwanza zikubaliwe na wengi vinginevyo haikuwa rahisi mtu mmoja kuitisha wito wa kazi fulani na watu wengine kuja kuifanya.

Kazi hizi ambazo hata serikali ya awamu ya kwanza ilizikazania sana mara baada ya Tanganyika kupata uhuru, ni pamoja na ujenzi wa mashule, kuchimba visima vya maji, kuchimba barabara na kadhalika. Upo ushahidi wa kutosha kuhusu Wapare walivyotumia mfumo huu na kupata maendeleo makubwa Wilayani mwao.

Zipo barabara za Mwanga hadi Ugweno na Usangi; Ndungu hadi Mamba na Vunta; Hedaru hadi Mwala; Makanya hadi Chome,Mpirani hadi Bombo Song’ana,Gonja Maore hadi Vuje naVudee hadi Mbaga, Lembeni hadi Kilomeni. Hata hivyo, si barabara tu lakini zahanati, na shule nyingi zimejengwa na wapare wa wilaya za Same na Mwanga na kuinua kiwango cha maendeleo yao.

Nakumbuka watu hawa si watu wapenda misaada ya mteremko ndiyo maana pamoja na kukabiliana na hali mbaya ya uhaba wa mvua mara kwa mara wamekuwa si watu wa kupiga yowe haraka.

Kazi zilizofanywa kupitia utaratibu huu wa msaragambo ziliufanya Mkoa huu wa Kilimanjaro uongoze kwa maendeleo ya barabara nzuri, ujenzi wa shule nyingi hadi katika vitongoji.

Kiwili ni msamiati mwingine wa Kipare ambao ni mfumo wa maisha walioukubali katika kuendesha maisha ya familia na jamii zao kwa kusaidiana kazi.

Kiwili ni utaratibu ambapo familia au majirani hualikana ili kusaidiana katika kazi za kilimo, na hata mavuno hasa pale mmoja wao anapokuwa na kazi shambani mwake na kuhitaji msaada. Siku hiyo, watu hukutana na kufanya kazi hiyo waliyoitiwa, mwenye kazi huandaa chakula ambacho watu watapata baada ya kumaliza kazi.

Utaratibu huu ulikuwa na manufaa makubwa maana ulirahisisha kazi na kujenga moyo wa kusaidiana. Kiwiri pia kiliweza kuitishwa na majirani kuwalenga wazee waliochoka au wagonjwa, ambao kwa namna moja au nyingine walionekana kushindwa kumudu kazi zao za shambani.

Kupitia kazi za kusaidiana maisha ya familia nyingi za Wapare ziliokolewa na majanga ya kufikwa na njaa.

Bila shaka zipo mila na desturi nzuri ambazo Watanzania tulikuwa nazo, lakini wageni wakatuhadaa na kutulaghai kwamba ya kwetu yote yalikuwa si mema nasi tukaanza kuyaacha.

Vyakula vikuu vya Wapare

[hariri | hariri chanzo]

Makande (Mbure),ugali(hasa ule wa muhogo wanauita ibadaa), ndizi, wali kwa wale wanaoishi maeneo ya tambarare kama Ndungu, Kisiwani, Ngullu Kavagala Kwakoa Maore na Mpirani. Pia kuna vyakula kama Kishumba, Kibulu, na mboga maarufu "Msele" nkokoro n.k vyakula hivi vinaliwa katika maeneo ya Kilomeni, Sofe, Kisangara Chanjale

Wapare pia wana ukaribu na makabila ya Mkoa wa Tanga hasa Wasambaa, Wazigua na Wanguu. Ukaribu wao uko katika lugha ambapo maneno mengi ya makabila haya yanafanana. Vile vile hata majina ya baadhi ya maeneo yaliyopo kwa Wapare yapo pia kwenye maeneo wanamoishi makabila kama vile Wasambaa na Wanguu. Kwa mfano, kwa Wapare kuna majina ya maeneo kama vile Gonja, Ndeme, Ndolwa n.k. Majina haya yapo pia maeneo ya Wanguu na Wasambaa. Hii inaonesha kwamba makabila haya yana asili moja.

Mapacha kati ya Wapare

[hariri | hariri chanzo]

Kulikuwa na imani potovu kuwa mwanamke akizaa watoto mapacha analeta mkosi na laana kwenye ukoo pia mtoto akianza kuota meno na yakaanza kuotaa ya juu,kwa hiyo watoto hao waliuawa kwa kutupwa au huegeshwa juu kilele pembezoni wakiwa wamelala baada ya kunyonyeshwa ama kulishwa uji na wazazi wao kwenye jiwe kubwa ambalo kule Mbaga - Pare ya kusini linaitwa Malameni, Usangi - Mwero linaitwa Ikamba, Songoa ljiwe likaitwa mkumba vana, pia na Mfinga ya Kikweni makutano ya kwenda Ugweno na Usangi linaitwa Lubegho ambapo ni aghalabu mtoto kupona kwani akiamka toka usingizini akijigeuza tu hudondoka toka kule ju hadi chini nakufa. Maajabu ni kwa mtoto mmoja aliye okotwa na Mzee Mgaya kule Ikamba na kumlea hadi akakuwa na kuwa Mtumishi wa Mungu jasiri na maarufu Marehemu Mchungaji Nathanaeli Mgaya. Hadi leo hii mawe hayo yapo.

Watu mashuhuri wa Upare

[hariri | hariri chanzo]

Inasemekana Wapare ni kabila la watu wachache lakini wana ushawishi mkubwa katika nyanja za siasa, vyombo vya habari na uchumi wa Tanzania sambamba na nyanja nyingine mbalimbali. Baadhi ya watu wake maarufu ni: