Nenda kwa yaliyomo

Tendaguru

Majiranukta: 9°42′S 39°12′E / 9.7°S 39.2°E / -9.7; 39.2
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

9°42′S 39°12′E / 9.7°S 39.2°E / -9.7; 39.2


Kiunzi mifupa cha dinosauri kutoka Tendaguru kwenye Makumbusho ya Historia Asilia mjini Berlin
"Oberaufseher präpariert grosse Rippe" - Msimamizi mkuu (Boheti bin Amrani) akisafisha ubavu mkubwa
Walter Janensch alivyoorodhesha hali ya visukuku vilivyopatikana Tendaguru

Tendaguru ni jina la mlima mdogo uliopo karibu na kijiji cha Nambiranji, kata ya Mipingo, takriban kilomita 60 upande wa magharibi-kaskazini kutoka Lindi kusini mwa Tanzania. Kilima hiki kinafahamika kwa kupatikana kwa visukuku vya dinosauri.

Umaarufu wa Tendaguru

Tendaguru imekuwa mashuhuri kimataifa tangu kupatikana kwa mifupa ya dinosauri kwenye mwaka 1906, wakati Tanganyika ilitawaliwa kama koloni kwa jina la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Ugunduzi huu ulifuatwa na msafara wa uchimbaji kwenye miaka 1909 hadi 1913 ambako hasa wataalamu wawili Werner Janensch na Edwin Hennig pamoja na mamia ya wafanyakazi wazalendo walichimbua mifupa mingi ya madinosauri pamoja na visukuku vingine vilivyopelekwa Berlin, Ujerumani. Kati ya mifupa hiyo vilipatikana viunzi kamili vya mifupa ya dinosauri wakubwa vinavyojulikana.

Msimamizi mkuu wa wafanyakazi wazalendo alijulikana kwa jina la Boheti bin Amrani[1]. Viunzi mbalimbali vilichimbuliwa chini ya uongozi wake maana wataalamu Wajerumani walikuwa wawili tu na mifupa iliyoonekana wakati ule ilisambaa katika eneo kubwa sana ilhali wenyeji waliendelea peke yao kwa wiki kadhaa hadi kutembelewa tena[2].

Janensch aliendelea kwa miongo iliyofuata kuchunguza visukuku kutoka Tendaguru vinavyohifadhiwa leo katika Makumbusho ya Historia Asilia Berlin.

Matabaka ya Tendaguru

Leo hii jina la "Tendaguru" linatumiwa pia kwa ajili ya matabaka ya miamba yenye visukuku vingi yanayoenea kwenye sehemu karibu na pwani ya Tanzania kusini; miamba hiyo inaonekana vizuri hasa katika eneo la Tendaguru lakini hadi sasa imetambuliwa kuanzia mto Matandu (karibu na Kilwa) hadi Ziwa Lutamba[3] lililopo upande wa magharibi wa Lindi mjini.

Matabaka ya Tendaguru huwa na unene wa mita 100 - 900. Yalitokea zamani za kipindi cha Kijura, yaani takriban miaka milioni 163 hadi 145 iliyopita. Wakati ule sehemu hizi zilizopo sasa kilomita 40-70 ndani ya bara zilikuwa maeneo ya pwani ambako wanyama wakubwa kama dinosauri lakini pia wadogo kama samaki au konokono waliishi kwenye maji ya bahari yasiyo na kina kirefu, ufukweni, katika mito iliyoishia baharini pamoja na mabwawa na maziwa karibu na pwani. Walipokufa miili yao ilikaa ikizama katika matopematope na kufunikwa.

Visukuku vya Tendaguru

Mizoga hiyo ikiendelea kuoza polepole matope yaliingia ndani ya seli za mwili na kuzijaza. Kama mchakato huu unaweza kuendelea bila mvurugo mwili wenyewe unapotea lakini kadiri matope, chumvi na madini mbalimbali vinaingia na kujaza sehemu za mwili maumbo ya viungo yanaweza kuhifadhiwa wakati matope na madini yanakauke. Sehemu hizi za pwani ziliinuliwa juu katika mwendo ya miaka mingi na kufunikwa na ardhi nyingine. Matope pamoja na mifupa au maganda ya konokono yalikauka yakagandamizwa polepole na kuwa mwamba unaotunza ndani yake maumbo ya kiunzi mifupa na maganda ya konokono ya bahari yaani kuonyesha matokeo yanayoitwa "visukuku".

Kitabu cha vijana kuhusu Tendaguru

Mengineyo

Cassian Magori na Charles Saanane walitunga mwaka 1998 kitabu kwa wasomaji wadogo kinachoitwa Dinosaria wa Tendaguru.[4]

Tazama pia

Marejeo

  1. Katika Hennig, E. (1912) Am Tendaguru, uk. 35, kuna picha yake kwa karibu
  2. Hennig (1912), uk. 35
  3. Bussert na wenzake (2009), uk. 151
  4. Cassian Magori, Dinosaria wa Tendaguru, E & D Limited, 1998, ISBN 9789987622061

Vyanzo

  • Hennig, E. (1912) Am Tendaguru. Leben und Wirken einer deutschen Forschungs-Expedition zur Ausgrabung vorweltlicher Riesensaurier in Deutsch-Ostafrika. Stuttgart: Schweizerbart online hapa
  • Bussert, Robert; Heinrich, Wolf-Dieter; Aberhan, Martin (August 2009). "The Tendaguru Formation (Late Jurassic to Early Cretaceous, southern Tanzania): definition, palaeoenvironments, and sequence stratigraphy". Fossil Record. 12 (2): 141–174. doi:10.1002/mmng.200900004. ISSN 1435-1943