Nzi wa Nairobi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Paederus eximius)
Nzi wa Nairobi
Paederus littoralis anayefanana na nzi wa Nairobi
Paederus littoralis anayefanana na nzi wa Nairobi
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Staphylinoidea (Wadudu kama bungo mbawa-nusu)
Familia: Staphylinidae (Bungo mbawa-nusu)
Jenasi: Paederus
Fabricius, 1775
Ngazi za chini

Spishi 474, 3 katika Afrika ya Mashariki:

Nzi wa Nairobi (pia nzi wa Kenya) ni jina la kawaida la spishi kadhaa za mbawakawa za jenasi Paederus katika familia Staphylinidae ambazo zinaweza kusababisha shida ya ngozi inayoitwa uwati wa pederi (Paederus dermatitis). Mbawakawa hao ni spishi za bungo mbawa-nusu.

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Bungo hao ni wadudu wenye urefu wa mm 6-13. Pronoto (kidari) na fumbatio ni nyekundu na kichwa, elitra (mabawa ya mbele) na ncha ya fumbatio ni nyeusi lakini zikiakisi miale ya nuru zinaweza kuonekana rangi ya buluu au kijani.

Wanataga mayai yao katika mahali panyevu, k.m. majani yanayooza. Lava hupitia hatua mbili kabla ya kuwa mabundo. Lava na wapevu hujilisha wadudu wadogo.

Sumu[hariri | hariri chanzo]

Angalau spishi 20 za Paederus na spishi kadhaa za jenasi nyingine zihusianazo zina sumu kali katika hemolimfi (“damu”) yao, pamoja na spishi za nzi wa Nairobi. Sumu hiyo inaitwa pederini na ni kali kuliko ile ya buibui wa aina za black widow. Inazalishwa na bakteria za jenasi Pseudomonas zinazoishi katika tumbo la majike.

Nzi wa Nairobi hawang'ati wala kudunga, lakini wakipondwa dhidi ya ngozi sumu inasababisha athari za ngozi, mara nyingi kwenye shingo, uso na mikono.

Sifa za kitiba za uwati wa pederi[hariri | hariri chanzo]

Mtu anaweza kukosa dalili zozote kwa masaa 12 hadi 24, lakini baadaye anaweza kupata moto mkali na kuwasha karibu na eneo lililoathiriwa. Siku mbili hadi tatu baada ya kugusa bungo eneo hilo linaweza kuwa jekundu na kuvimba na malengelenge madogo yanaweza kuonekana ambayo yanaweza kuendelea kuonekana kama majipu. Kwa maeneo nyuma ya viungo, ambapo nzi wa Nairobi anaweza kuwa amepondwa, vidonda vinavyojulikana kama vidonda vya "busu" vinaweza kuonekana.

Baadaye malengelenge yatapasuka na kuungana mpaka kuonekana kama mahali palipochomwa. Kwa kweli watu wengi hugundua vidonda tu wakati eneo lililoathiriwa linaanza kuonekana kama mahali palipochomwa. Vigaga na magamba yanaweza kutokea, lakini takriban dalili zote hufifia katika wiki mbili hadi tatu. Pengine maeneo yaliyoathiriwa na nzi wa Nairobi yanaweza kupata maambukizo ya pili ya bakteria ambayo yanaweza kuonekana kama maambukizo ya ngozi. Zaidi ya hayo eneo lililoathiriwa linaweza kupata mabaka meusi.

Hali inayojulikana kama jicho la Nairobi itatokea wakati mtu anagusa jicho lake kwa mikono ambayo imegusana na sumu ya nzi wa Nairobi. Hii inaweza kusababisha uvimbe wa jicho, uwekundu au shida nyingine.

Uwati wa pederi unaweza kuchanganyikiwa na mkanda wa jeshi, kuchoma kwa kiowevu, athari kali za mzio, uwati wa majongoo na uwati wa mgusano. Msimu, uwepo wa nzi wa Nairobi au kuonekana kwa bungo huyu kwenye ngozi zinaweza kusaidia katika utambuzi.

Tiba[hariri | hariri chanzo]

  • Mara tu umegusa bungo au ikiwa bungo amepondwa dhidi ya ngozi, nawa mikono yako na eneo lililoathiriwa mara moja kwa sabuni na maji.
  • Paka dawa hafifu yenye steroidi ngozini, na mahali ambapo kuna uwezekano wa ambukizo la pili la bakteria, paka dawa ya kuua viini.
  • Antihistamini za kumeza zitapunguza kuwasha ambako kunasababisha kujikuna.

Kinga[hariri | hariri chanzo]

Ni muhimu kujiepuka kugusa nzi wa Nairobi hapo kwanza kwani uwati unaofuata unaweza kusababisha usumbufu mbaya mno na, katika visa vichache, makovu. Hii inaweza kupatikana kwa:

  • Katika majira ya mvua, wakati nzi wa Nairobi imeenea, funga milango na madirisha yote kabla ya kuwa giza.
  • Lala chini ya chandarua.
  • Ikiwa unaona nzi wa Nairobi akitambaa kwenye ngozi yako, mpeperushe badala ya kumfuta. Hii inapunguza hatari ya kumponda. Unaweza kutumia pia kipande cha karatasi kumwondoa kwenye ngozi yako.
  • Ukiponda bungo moja, epuka kugusa macho yako. Nawa mikono yako na eneo lililoathiriwa kwa maji na sabuni mara moja.
  • Tafuta bungo katika maeneo kuzunguka vitanda na dari kabla ya kulala.
  • Ondoa uoto wa ziada kutoka nyumba na karibu nazo.