Nenda kwa yaliyomo

Nikolaus von Zinzendorf

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nikolaus Ludwig Graf von Zinzendorf, sehemu ya picha ya Balthasar Denner

Nikolaus Ludwig von Zinzendorf (26 Mei 17009 Mei 1760) alikuwa kiongozi wa dini ya Ukristo nchini Ujerumani na askofu wa Kanisa la Moravian.

Alizaliwa mjini Dresden katika familia ya makabaila Wajerumani Walutheri. Baba yake alikufa alipokuwa mdogo, akalelewa na bibi yake aliyemshawishi kwa mwelekeo wa uamsho wa Kikristo wa upietisti.

Baada ya kumaliza shule alisoma sheria kwenye chuo kikuu cha Wittenberg; baada ya masomo yake alifanya safari ya kuzunguka Ulaya, jinsi ilivyokuwa kawaida kwa vijana makabaila wa siku zile. Kwenye safari hii alikutana na kuwa rafiki na viongozi wa madhehebu mbalimbali kama Wareformed, Wakatoliki, Walutheri na wengine.

Kati ya miaka 1721 na 1732 alikuwa mshauri wa kisheria kwenye ikulu ya mfalme August wa Saksonia huko Dresden.

Sanamu ya kumbukumbu ya Zinzendorf huko Herrnhut

Mwaka 1722 alimwoa Erdmuthe na mwaka uleule alinunua mashamba ya kikabaila ya Berthelsdorf kutoka bibi yake. Ilikuwa eneo dogo lenye kijiji kimoja alipotawala kama mtemi chini ya Kaisari pekee, ingawa eneo lake dogo lilikuwa ndani ya jimbo kubwa La Saksonia.

Katika eneo hili alianza kupokea wakimbizi kutoka Moravia waliokuwa wafuasi wa Umoja wa Ndugu wa kale, mwelekeo wa Kiprotestanti wa Bohemia na Moravia uliopigwa marufuku tangu mwisho wa vita ya miaka 30. Aliwapa wakimbizi hao ardhi walipojenga kijiji kipya cha Herrnhut; hapa waliunda "Umoja wa Ndugu ulioanzishwa upya" unaojulikana kama Kanisa la Moravian au pia Ndugu wa Herrnhut.

Kutoka Herrnhut desturi ya kuchagua ubeti wa Biblia kama neno la mwongozo kwa kila siku ilianza kusambaa: mkusanyo wa maneno haya yanajulikana kama Kiongozi Kalenda.

Mwaka 1731 Zinzendorf alitembelewa na nduguye mkabaila mmoja kutoka Denmark aliyefika pamoja na mtumishi wake Mwafrika kutoka Visiwa vya Karibi aliyewahi kuwa mtumwa. Masimulizi ya huyu Mwafrika yalihamasisha ndugu wa Herrnhut kutuma wahubiri kwenda Karibi na hii ilikuwa chanzo cha uenezaji wa kimataifa wa kanisa la Moravian.

Zinzendorf aliwaandalia safari akitumia mawasiliano na ikulu ya mfalme wa Denmark. Zinzendorf mwenyewe alitembelea ndugu wa Herrnhut waliosafiri kuhubiri Saint Thomas (Karibi), Marekani, London na nchi jirani za Bahari Baltiki.

Aliendelea kusoma teolojia na mwaka 1734 akabarikiwa kama mchungaji Mlutheri. Hata hivyo alifukuzwa katika Saksonia (hapa Ulutheri ulikuwa dini rasmi) kutokana na shaka kuhusu imani yake, akapaswa kuhamia sehemu nyingine za Ujerumani alipoanzisha jumuiya mpya ya wafuasi wa Umoja wa Ndugu.

Mwaka 1737 alibarikiwa kama askofu wa Umoja wa Ndugu na askofu wa Umoja huu kutoka Polandi ambako shirika chache za Umoja wa kale ziliweza kuendelea.

Mwaka 1747 aliruhusiwa kurudi Saksonia na ndugu wa Herrnhut walikubaliwa kama jumuiya iliyoshikamana na kanisa la Kilutheri la Saksonia. Mke wake Erdmute aliyezaa watoto 12 aliaga dunia mwaka 1756, hivyo baadaye akamwoa Anna Nitschmann mmoja wa wakimbizi kutoka Moravia.

Zinzendorf anakumbukwa kama baba wa kiroho wa kanisa la Moravian. Alitunga nyimbo nyingi zinazoimbwa kwa Kijerumani hadi leo na nyingine zimetafsiriwa katika lugha mbalimbali.

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons