Nenda kwa yaliyomo

Mapatano juu ya matumizi ya maji ya mto Nile ya 1929

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bonde la Nile na nchi zake.

Mapatano juu ya matumizi ya maji ya mto Nile yalifikiwa baina ya serikali za Misri na Ufalme wa Maungano (Uingereza) mwaka 1929 kwa njia ya kubadilishana nyaraka za kidiplomasia.

Misri ilikubali kuongezeka kwa maji yaliyotumiwa kwa umwagiliaji nchini Sudan kama kiwango cha kutumiwa hakitaingilia haki za Misri juu ya maji ya Nile. Uingereza kama mlezi au mkoloni wa Sudan ilitambua haki za kihistoria za Misri juu ya maji ya mto huo ikakubali ya kwamba matumizi ya maji ya Nile katika maeneo juu ya utawala wake yasihatarishe mahitaji ya Misri.

Haki za Misri katika mapatano

[hariri | hariri chanzo]

Mapatano hayo yaliipa Misri haki zifuatazo: · Misri ina haki ya kukataza kazi zozote zinazoweza kuwa hatari kwa mwendo wa maji ya mto Nile. · Misri inaahidiwa matumizi ya mita za ujazo bilioni 55.5 katika jumla ya bilioni 84 ya maji ya Nile. · Misri ina haki ya kutembelea na kuchungulia kila mahali mwendo wa mto Nile na miradi yote ya matumzi ya maji kando yake.

Sababu za kufanya mapatano

[hariri | hariri chanzo]

Sababu ya kufikia mapatano hayo ilikuwa mabadiliko ya kilimo katika nchi zote mbili. Misri iliwahi kutumia maji ya Nile hasa kwa njia ya mafuriko yake iliyofunika kila mwaka mashamba kando ya mto na kuacha matope yenye rutuba juu ya mashamba yale na pia kwa njia ya mifereji midogo iliyopeleka maji kwa kanda nyembamba ya mashamba kando ya mwendo wa mto. Lakini tangu mwisho wa karne ya 19 kilimo cha pamba kilisambaa kilichohitaji umwagiliaji wa kudumu, pia mbali zaidi na mto. Kwa hiyo Wamisri walianza kuangalia na kupima kiwango cha maji yaliyopatikana.

Katika Sudan serikali ya kikoloni ililenga kupanua eneo la mashamba kwa njia ya umwagiliaji. Pia ilitaka kupunguza upotevu wa maji katika eneo la Sudd ambako vizuizi vinasababisha maji kukwama yakifunika eneo kubwa sana la maziwa na mabwawa matope kwa hiyo maji mengi kupotea kwa njia ya uvukizaji kwa sababu ya joto kali la sehemu zile. Kwa hiyo Waingereza walipanga kuchimba mfereji wa Jonglei kwa kusudi la kupunguza kiasi cha maji kinachokwama kwenye Sudd na kuvukizika, badala yake kuyapeleka kwa njia ya mfereji hadi Khartoum. Wakati huohuo mipango iliunda hofu ya kwamba maji yanaweza kutumiwa kumwagilia mashamba mapya kando ya mfereji.

Mapatano baada ya ukoloni

[hariri | hariri chanzo]

Tangu miaka ya 1950 na 1960 Uingereza haitawali tena maeneo ya Afrika na nchi huru zilianzishwa kando ya mto Nile ambazo ni Sudan, Uganda, Kenya na Tanzania zilizokuwa zote chini ya Uingereza.

Mnamo mwaka 1902 Waingereza waliwahi kufanya mkataba na serikali ya mfalme Menelik II wa Ethiopia alipoahidi kutojenga malambo au kuanzisha miradi inayopunguza mwendo wa maji ya Nile ya buluu. Katika kifungu III cha mkataba huo matini ya Kiingereza yanataja wajibu wa Ethiopia wa kupata kibali cha serikali za Uingereza na Sudan kabla ya kujenga malambo kwenye mto Naili, lakini katika matini ya Kiamhari masharti hayo hayatajwi. Ethiopia haikuwahi kutia sahihi mkataba huo, nakala ya Kiingereza pekee ilitiwa sahihi na Uingereza. [1]

Misri inadai hadi leo ya kwamba nchi zilizojitokeza tangu uhuru ni wafuasi wa Uingereza katika mapatano. Wanasiasa Wamisri waliwahi kudokeza ya kwamba Misri inatazama suala la maji kama jambo la usalama wa taifa au kwa maneno mengine yalitisha ya kwamba matumizi ya maji katika nchi nyingine yanaweza kusababisha vita.

Serikali za nchi nyingine zilikataa kukubali. Ila tu Sudan ilikubali mwaka 1959 mapatano mapya inapotambua kipaumbele cha Misri juu ya maji yale<ref>Agreement between the Republic of the Sudan and the United Arab Republic for the full utilization of the Nile waters signed at Cairo, 8 November 1959<, tovuti ya FAO/ref>.

Hadi mwaka 2011 majadiliano juu ya mapatano mapya yaaendelea kati ya nchi zote jirani wa Nile. Mwaka 2010 Ethiopia, Uganda, Tanzania na Rwanda zilitia saini mapatano mapya kati yao juu ya matumizi ya maji ya Nile lakini Misri ilikataa kukubali hatua hii.

  1. The Treaty between Great Britain and Ethiopia of May 15,1902, blogu ya we aspire, ya tarehe 15.06.2020, iliangaliwa Juni 2021

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]