Nenda kwa yaliyomo

Pomboo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Lipotidae)

Kwa kundinyota linalojulikana pia kama "delphinus" angalia Dalufnin (kundinyota)

Pomboo
Pomboo
Pomboo
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Cetacea (Wanyama kama nyangumi)
Oda ya chini: Odondoceti (Nyangumi wenye meno)
Ngazi za chini

Familia 7:

Pomboo (kwa Kiingereza dolphin) ni wanyama wa bahari wa familia mbalimbali katika oda ya Cetacea au nyangumi. Wanahesabiwa kati ya nyangumi wenye meno (Odondoceti).

Spishi nyingi zinaishi baharini lakini kuna pia spishi chache wanaokaa kwenye maji baridi ya mito. Kuna pia spishi za pomboo wa mtoni ambao ni familia tofauti hata wakifanana sana na pomboo za kawaida.

Kama nyangumi wote wana maisha yanayofanana na samaki lakini si samaki, bali mamalia wanaozaa watoto hai na kuwanyonyesha maziwa kwa kutumia viwele vyao. Wana damu moto na kupumua kwa mapafu, maana yake hawawezi kukaa chini ya maji muda wote kama samaki, bali wanapaswa kufika kwenye uso wa maji na kupumua kabla ya kuzama chini tena kwa muda mrefu.

Pomboo wanahesabiwa kati ya wanyama wengi akili sana, ijapokuwa ni vigumu kusema wanayo kiasi gani. Kujua kiwango cha akili kwa wanyama wengine, pomboo wamekwishafanyiwa tafiti nyingi wakiwa wanafugwa, au wanaishi peke yao. Aina kadhaa wana ubongo mkubwa sawa na mwanadamu, na ni marafiki wake wazuri, jambo linalowajengea umaarufu mkubwa.

Utangulizi

[hariri | hariri chanzo]

Pomboo ni wanyama wa majini wanaokaribiana sana na nyangumi; kuna takribani spishi arobaini katika jenasi kumi na saba. Wana ukubwa tofauti, kuanzia mita 1.2 na kilogramu 40 mpaka mita 9.5 na tani 10.

Wanapatikana duniani kote, hasa kwenye bahari za kina kifupi wao hula nyama na hasa samaki. Familia yao ya Delphinidae ndiyo kubwa katika jamii yao ya cetacean.

Pomboo wa sasa wanatokana na wale wa kale kadiri ya miaka milioni kumi iliyopita.

Mahusiano

[hariri | hariri chanzo]

Pomboo huchangamana sana wao kwa wao, na huweza hata kufikia kundi moja dogo. Makundi hayo yanaweza kuongezeka, hata kufikia pomboo 1,000. Pomboo kwenye kundi huweza kubadilikabadilika kwenye makundi yao. Hutumia milio mbalimbali katika mawasiliano yao, huku wakisaidiana sana hasa pale miongoni mwao wanapokuwemo wagonjwa, ambapo huweza hata kuwasaidia kupumua kwa kuwasogeza kwenye usawa wa masi waweze kupumua. Pomboo huko Nyuzilandi wameonekana wakilinda pomboo jike na ndama wao pomboo wameonekana pia wakiwalinda waogeleaji kwa kuwazunguka katika duara ili kuwalinda na papa au kuwakasirisha papa ili kuwafukuza.

Mara kadhaa pomboo wamekuwa wakigombana, hasa pomboo dume ambao huwa na makovu mengi mwilini mwao; sababu ya kupigana huwa ni kugombania nafasi ya kuwa na jike na wale wanaoshindwa huenda zao mbali.

Pomboo hujamiiana kwa vipindi vifupi lakini mara nyingi katika muda mfupi. Hubeba mimba kwa muda wa miezi 11-12 kutokana na spishi husika. Pomboo huanza mapema sana kuwa tayari kujamiiana katika umri mdogo, na umri hasa wa kukomaa kijinsia hutofautiana kutoka spishi moja mpaka nyingine.

Pomboo hufahamika kwa kufanya mapenzi kwa sababu nyingine mbali na kupata watoto, na wakati fulani hujamiiana kwa jinsia moja, baadhi ya pomboo hudiriki hata kujamiiana na pomboo wa spishi nyingine na mara ningine huonesha mapenzi hata kwa wanyama wengine, kujumuisha na binadamu.

Pomboo hula kwa namna mbalimbali, ambapo huwa na mbinu kadhaa za kushambulia samaki. Namna mojawapo ni ile ya kuwatenga samaki kadhaa kwa kuwazunguka, na kisha kuanza kuwashambulia taratibu. Namna nyingine ni pale pomboo wanapowafukuza samaki kwenye maji yenye kina kifupi na kisha kuwakamata kwa urahisi. Huko South Carolina, pomboo zaidi huwafukuzia samaki kwenye matope ili kuwakamata kwa urahisi.

Ajabu kubwa ni wale pomboo wanaoshirikiana na binadamu kuvua samaki. Pomboo huwafukuzia samaki walipo wavuvi na wavuvi huwakamata samaki hao kwa nyavu zao. Pomboo hao hufaidi samaki wanaokimbia toka kwenye nyavu.

Usingizi

[hariri | hariri chanzo]

Kwa kawaida, pomboo hulala kwa upande mmoja tu wa ubongo, huku mwingine ukiendelea kufanya kazi, ili kuratibu masuala mengine yote kama vile kupumua na kujihami na hatari za mazingira yao. Usingizi wa hatua za mwanzo hutokea katika sehemu zote za ubongo.

Wakiwa wanafugwa, pomboo wameonesha tabia za kulala/kusinzia kabisa, huku wakifunga macho yote kupumua ni bila ya ufahamu, huku mkia ukiendelea kujipiga piga. Kuishi kwenye maji yenye mkondo mkubwa huwa na hatari ya kuzama na kufa maji, hivyo inawapasa pomboo kuogelea nyakati zote. Hivyo, pomboo hulala kwa vipindi vifupi sana, ndani ya sekunde 4 na 60.

Spishi za Afrika

[hariri | hariri chanzo]

Spishi za mabara mengine

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mnyama fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pomboo kama uainishaji wake wa kibiolojia, maisha au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.