Kitukutuku bandia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kitukutuku bandia
Tmesibasis lacerata
Tmesibasis lacerata
Lava wa spishi fulani kwenye jani
Lava wa spishi fulani kwenye jani
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Neuroptera (Wadudu walio na mabawa wenye vena nyingi kama kimia)
Nusuoda: Myrmeleontiformia (Wadudu kama vitukutuku)
Familia: Myrmeleontidae (Wadudu walio na mnasaba na vitukutuku)
Nusufamilia: Ascalaphinae
Lefèbvre, 1842
Ngazi za chini

Makabila 6:

Vitukutuku bandia ni wadudu wadogo hadi wakubwa kiasi wa nusufamilia Ascalaphinae[1] katika familia Myrmeleontidae wa oda Neuroptera (wadudu mabawa-vena) walio na mnasaba karibu na vitukutuku. Huitwa bandia kwa sababu lava wao hawachimbi mashimbo ya umbo la mpare au marima ili kukamata sisimizi. Kinyume hiyo hujificha chini ya takataka au wana rangi za kamafleji. Kuna karibu na spishi 450 za vitukutuku bandia zinazotokea duniani kote katika maeneo ya kitropiki na kinusutropiki[2].

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Vitukutuku bandia hutofautishwa kwa urahisi na vitukutuku kwa macho yao makubwa na vipapasio vyao virefu vyenye virungu, hiyo ya mwisho ambayo pia huwatofautisha na kereng'ende wanaofanana kijuujuu, ambao wana vipapasio vifupi kama nywele ngumu. Vitukutuku wana vipapasio vifupi vyenye virungu vidogo, macho madogo na mabawa yenye vena kama wavu[3][4]. Vitukutuku bandia wengi wana urefu wa sm 3-4, bila kujumuisha vipapasio, na mabawa yao yanaweza kuwa hadi sm 6[5]. Wapevu wa kabila Ululodini wana macho makubwa yaliyogawanyika na tabia ya kukiakia wakati wa mwanga kidogo, ambapo jina lao la Kiingereza "owlfly" lilitoka[5].

Kichwa[hariri | hariri chanzo]

Maono ya karibu ya kichwa cha Ascalaphus sinister; mstari kupitia macho inaonekana wazi.

Vipapasio ni virefu sana, mara nyingi karibu na urefu wa mwili. Viko vyembamba sana na hubeba vinundu vinavyofanana na rungu kwenye ncha zao, ambavyo vinaweza kuwa na rangi tofauti.

Macho ni makubwa zaidi kuliko yale ya vitukutuku. Katika makabila Ascalaphini na Ululodini macho yamegawanywa na kigongo katika sehemu ya juu na ya chini. Sehemu ya juu ni nyeti tu kwa mwanga wa UV huku sehemu ya chini ikiweza pia kuhisi mwanga wa bluu-kijani pamoja na UV[6][7]. Vitukutuku bandia hawana oseli (macho sahili).

Thoraksi[hariri | hariri chanzo]

Thoraksi ina nywele nyingi na hubeba miguu na mabawa. Miguu ni mifupi kiasi na minene na ina nywele nyingi. Pia huzaa miiba, ambayo ni kubwa zaidi kwenye tibia. Tarsi ni imara sana na zina pingili moja tu yenye kucha mbili.

Mabawa ni mangavu katika spishi zinazokiakia usiku. Katika spishi zinazokiakia mchana, mabawa mara nyingi huwa na rangi au yana madoa mazito na meusi. Njano ni rangi ya kawaida, lakini kahawia na kahawia-nyekundu pia hutokea. Rangi hizi husababishwa na nywele ndogo na sio vigamba kama kwa vipepeo. Mabawa ya mbele daima ni marefu na membamba kuliko mabawa ya nyuma. Kila bawa hubeba seli ya rangi karibu na ncha ya ukingo wa mbele, inayoitwa pterostigma. Ni nzito kuliko seli nyingine na hutoa usawa wakati wa kuruka. Wakati wa kupumzika, mabawa huwekwa juu ya fumbatio au kando yake.

Vitukutuku bandia ni warukaji wa nguvu zaidi kuliko vitukutuku, ingawa kwa mbali hawana nguvu kama kereng'ende. Pamoja na hayo, wana uwezo wa kukamata wadudu wengine wakiruka, ambao huwala. Hii ni tofauti tena na vitukutuku, ambao hujilisha kwa mbochi ikiwa kitu chochote.

Fumbatio[hariri | hariri chanzo]

Fumbatio huwekwa kwa pembe ili kufanana na kitawi kilichokatika.

Fumbatio ni ndefu lakini mnono kuliko ile ya vitukutuku. Mara nyingi, mgongo huwa na uvimbe, haswa kwa majike. Madume wana mchomozo kwenye upande wa mgongo wa pingili ya kwanza, ya pili au ya tatu, ambao haupo kwa majike. Pia wana serki kwenye ncha ya fumbatio, ambazo, tena, majike hawanazo. Spishi nyingi huweka fumbatio juu kwa pembe fulani wakipumzika, huku mabawa zikiwa zimeshikiliwa dhidi ya kitawi au shina. Hii inaifanya kuonekana kama kitawi kilichovunjika.

Lava[hariri | hariri chanzo]

Lava wanafanana na vitukutuku, lakini wana viambatisho vilivyorefuka, wakati mwingine kama vidole, kila upande wa kila pingili, vinavyoitwa michomozo kama skoli[8]. Katika spishi nyingi wako pia wakubwa kuliko vitukutuku. Hatimaye, kwa kawaida hutembea mbele badala ya kuelekea nyuma.

Biolojia[hariri | hariri chanzo]

Mayai ya kitukutuku bandia kwenye kitawi.

Wapevu wa vitukututku bandia hukamata wadudu wadogo wanaoruka, ambao huwala wakiruka. Lava hungoja kenye otea na kukamata invertebrata mbuawa wowote ambao hukaribia kwa kutosha na sio mkubwa sana. Mara nyingi hujificha chini ya takataka au hujifunika kwa vipande vidogo vya takataka. Wengine wana rangi za kamafleji ambazo huwafanya kuwa karibu kutoonekana kwenye uso wao uliochaguliwa, ambao unaweza kuwa mwamba, shina la mti au jani.

Kupandana hutokea wakiruka. Mayai hutagwa kwa mistari kwenye kitawi au shina la mmea au chini ya mawe. Baadhi ya makumi hadi mayai 100 hutagwa katika sehemu kadhaa. Mayai yana umbo la duaradufu na yana ganda gumu. Wana ukubwa wa mm 2-3. Baada ya kutoka katika mayai, lava wadogo hujilisha kwa maganda ya mayai kwa muda kabla ya kutawanyika. Wanapitia hatua tatu, mwishoni kwake husuka kifukofuko cha hariri huku wakijumuisha chembe za uso. Kuwa bundo hutokea kwenye kifukofuko hiki ambacho kimefichwa kwenye takataka za majani au katika udongo au chini ya mawe.

Spishi kadhaa za Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

  • Allocormodes inconspicuus
  • Allocormodes intractabilis
  • Allocormodes junodi
  • Allocormodes kolbei
  • Allocormodes lefebvrei
  • Allocormodes maculipennis
  • Allocormodes nigristigma
  • Afroasca doboszi
  • Ascalaphus festivus
  • Disparomitus brevistigma
  • Disparomitus horvathi
  • Disparomitus kimminsi
  • Disparomitus simplex
  • Disparomitus transvaliensis
  • Eremoides bicristatus
  • Palpares inclemens
  • Phalascusa hildebrandti
  • Suphalomitus buyssoni
  • Tmesibasis imperatrix
  • Tmesibasis laceratus
  • Tmesibasis majesta
  • Tmesibasis rothschildi
  • Tmesibasis scopsi
  • Tmesibasis waelbroecki

Picha[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Renato J. P. Machado (2019) Owlflies are derived antlions: anchored phylogenomics supports a new phylogeny and classification of Myrmeleontidae (Neuroptera), Systematic Entomology 44(2): 1-33.
  2. Neuroptera: Ascalaphidae. University of Florida (2009).
  3. Owlflies. Missouri Department of Conservation.
  4. Foltz, John L. (August 10, 2004). Neuroptera: Ascalaphidae. ENY 3005 Family Identification. University of Florida. Jalada kutoka ya awali juu ya 2010-06-01. Iliwekwa mnamo July 14, 2010.
  5. 5.0 5.1 Ululodes quadrimaculatus, "owlfly". Clemson University (2004). Jalada kutoka ya awali juu ya 2008-10-12. Iliwekwa mnamo April 24, 2008.
  6. Belusic, G. et al. (2008) The visual ecology of the owlfly (Libelloides macaronius) In: Devetak, D. et al., Proceedings of the Tenth International Symposium on Neuropterology. Piran, Slovenia. Pp. 89-96.
  7. | titel = Ultraviolet vision in European owlflies (Neuroptera: Ascalaphidae): a critical review| auteur = Karl Kral
  8. Badano, D.; Pantaleoni, R. A. (2014). "The Larvae of European Ascalaphidae (Neuroptera)". Zootaxa 3796 (2): 287–319. PMID 24870677. doi:10.11646/zootaxa.3796.2.4. Archived from the original on 2019-04-28. Retrieved 2022-10-03.