Funguvisiwa la Kurili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mahali pa Kurili kati ya Japani na Kamchatka - Urusi bara

Funguvisiwa la Kurili (kwa Kirusi кури́льские острова́, kurilskiye ostrova) ni kundi la visiwa katika Pasifiki ya Kaskazini ambavyo ni sehemu ya Urusi. Ni visiwa 56 (pamoja na miamba midogo) viivyopangwa kama safu au nyororo yenye urefu wa kilomita 1300 kati ya rasi ya Kamchatka ya Urusi na kisiwa cha Hokkaido cha Japani. Kwa namna fulani inatenga Bahari ya Okhotsk na Pasifiki kubwa.

Majina[hariri | hariri chanzo]

Kuna majina mbalimbali kwa kundi hili la visiwa. Jina "Kurili" linatokana na lugha ya Waainu waliokuwa wakazi asilia. Kwao ilkuwa na maana ya "mahali pa watu" yaani visiwa vilivyokaliwa nao.

Kwa kipindi fulani cha historia Kurili zilikuwa sehemu ya Japani na kwa Kijapani vinaitwa Visiwa vya Chishima (Kanji 千島列島 chishima rettō, maana yake visiwa 1,000) au pia kama Visiwa vya Kuriru (Katakana: クリル列島 kuriru rettō yaani Funguvisiwa ya Kurili).

Jiografia ya Kurili[hariri | hariri chanzo]

Volkeno ya kisiwa Sarychev iliyolipuka mwaka 2009, jinsi ilivyoonekana kutoka kituo cha angani ISS.

Visiwa hivi vina asili ya kivolkeno; kila kisiwa ni kilele cha mlima wa volkeno iliyoanza kwenye tako la bahari na kukua kwa kumwaga magma chini ya maji hadi kufikia juu ya uso wa bahari.

Safu hii imetokea kama sehemu ya pete ya moto ya Pasifiki; hapa bamba la Pasifiki linasukumwa chini ya bamba la Amerika Kaskazini[1] na hivi kusababisha nafasi kwenye koti la dunia inayowezesha joto na magma kupanda juu.

Safu hii ya milima na visiwa ina volkeno takriban 100, na 40 kati ya hizi ni volkeno hai. Kuna matetemeko ya ardhi ya mara kwa mara; matetemeko makubwa zaidi yalitokea mwaka 1963, lenye nguvu ya 8.5, na mwaka 2006, lenye nguvu ya 8.3 lililosababisha tsunami iliyofika hadi pwani ya Kalifornia (Marekani). [2]

Tabianchi ni baridi; majirabaridi ni marefu, na majirajoto huwa na ukungu mwingi, hivyo jua kidogo tu. Sehemu kubwa ya usimbishaji hufika kwa umbo la theluji.

Tabianchi hii inasababisha visiwa vya kaskazini kuwa na uoto wa tundra na visiwa vya kusini na misitu inayofanana na taiga.

Miinuko mikubwa ni mlima Alaid wenye kimo cha mita 2,339 kwenye kisiwa cha Alasoy na mlima wa Tyatya wenye mita 1819 kwenye kisiwa cha Kunashir.

Bahari inayozunguka visiwa hivi ina samaki na wanyama wa bahari wengi.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Visiwa vya Kurili (majina ya Kirusi) na mipaka kati ya Japani na Urusi tangu karne ya 19.

Sawa na historia ya kisiwa cha Sakhalin, hata visiwa vya Kurili vilivutwa mara kadhaa kati ya Urusi na Japani katika mwendo wa karne za 19 na 20.

Wakazi asilia walikuwa Waainu waliofuata maisha ya uvuvi na kuwinda wakiwa na teknolojia asilia bila kutengeneza vyombo vya metali. Kwa hiyo walikosa uwezo wa kujitetea dhidi ya madola ya kisasa jirani kama Urusi na Japani.

Visiwa vya kusini vilikuwa chini ya athira ya Japani. Katika karne ya 19 meli za wavuvi Wajapani na Warusi waliingiliana, hivyo serikali za nchi hizi mbili zilifanya mkataba wa mwaka 1855 ya kuamulia mpaka uliokuwa kati ya visiwa vya Iturup na Urup. Sakhalin ilitajwa kama mahali wazi kwa watu wa pande zote mbili.

Mkataba wa Petersburg wa mwaka 1875 ulilenga kuondoa matatizo yaliyosababishwa na kutoelewana kwa walowezi Warusi na Wajapani huko Sakhalin. Japani ilikubali kukabidhi Sakhalin yote kwa Urusi na badala yake kupokea mamlaka juu ya visiwa vyote vya Kurili.

Kwenye mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945 Umoja wa Kisovyeti ilivamia Kurili na kuitwaa.

Tangu 1945 Kurili kwa jumla zinatazamwa kama sehemu ya Urusi, hali ambayo haikubaliwi na Japani. Visiwa vinatawaliwa kama sehemu ya mkoa wa Sakhalin Oblast.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Sehemu hii ya bamba la Amerika Kaskazini wakati mwingine hutazamwa kama bamba dogo la pekee kwa jina la Bamba la Okhotsk
  2. Central Kuril Island Tsunami in Crescent City, California Archived 26 Februari 2010 at the Wayback Machine. University of Southern California

Kujisomea[hariri | hariri chanzo]

  • Gorshkov, G. S. Volcanism and the Upper Mantle Investigations in the Kurile Island Arc. Monographs in geoscience. New York: Plenum Press, 1970. ISBN 0-306-30407-4
  • Krasheninnikov, Stepan Petrovich, and James Greive. The History of Kamtschatka and the Kurilski Islands, with the Countries Adjacent. Chicago: Quadrangle Books, 1963.
  • Rees, David. The Soviet Seizure of the Kuriles. New York: Praeger, 1985. ISBN 0-03-002552-4
  • Takahashi, Hideki, and Masahiro Ōhara. Biodiversity and Biogeography of the Kuril Islands and Sakhalin. Bulletin of the Hokkaido University Museum, no. 2-. Sapporo, Japan: Hokkaido University Museum, 2004.
  • Hasegawa, Tsuyoshi. Racing the Enemy: Stalin, Truman, and the Surrender of Japan. 2006. ISBN 978-0-674-02241-6.
  • Alan Catharine and Denis Cleary. Unwelcome Company. A fiction thriller novel set in 1984 Tokyo and the Kuriles featuring a light aircraft crash and escape from Russian-held territory. On Kindle.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]