Nenda kwa yaliyomo

Anofelesi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Anopheles)
Anofelesi
Anofelesi wa Gambia (Anopheles gambiae) akifyonza damu
Anofelesi wa Gambia (Anopheles gambiae) akifyonza damu
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Diptera (Wadudu wenye mabawa mawili tu)
Nusuoda: Nematocera (Diptera wenye vipapasio kama nyuzi: mbu)
Oda ya chini: Culicomorpha (Mbu kama kuleksi)
Familia: Culicidae (Mbu walio na nasaba na kuleksi)
Meigen, 1818
Jenasi: Anopheles
Meigen, 1818
Ngazi za chini

Spishi ±460.

Anofelesi ni spishi za mbu za jenasi Anopheles katika familia Culicidae. Zaidi ya spishi 100 zinaweza kueneza malaria ya watu, lakini spishi 30-40 tu ni muhimu sana. Katika Afrika anofelesi wa Gambia (Anopheles gambiae kwa maana pana) ni muhimu kabisa, kwa sababu anatokea mahali pengi kusini kwa Sahara na hueneza spishi ya malaria hatari sana, Plasmodium falciparum. Hapo majuzi spishi nyingine, anofelesi wa Asia (Anopheles stephensi), amefika Pembe ya Afrika. Spishi hiyo ni hatari kwa sababu inaweza kuishi mijini kwa urahisi kuliko anofelesi wa Gambia, kwa hiyo inaweza kuongeza visa vya malaria katika Afrika.

Mikao ya kupumzika ya wadumili wa Anopheles (A, B), kulingana na mbu asiye anofelesi (C).

Kama mbu wote, wadumili wa anofelesi wana mwili mwembamba wenye sehemu tatu: kichwa, toraksi na fumbatio.

Kichwa kimetoholewa kwa kupata taarifa ya hisia na kwa kujilisha. Kina macho na jozi ya vipapasio virefu vyenye pingili nyingi. Vipapasio ni muhimu kwa kugundua harufu ya kidusiwa na pia harufu ya maeneo ya kuzaliana ambapo majike hutaga mayai. Sehemu za kinywa zinaunda mrija mrefu unaoelekea mbele na unaotumika kujilisha. Maksila zinabeba palpi zilizo na vipokezi vya dioksidi kabonia, kivutio kikubwa kinachoonyesha yupo wapi kidusiwa wa mbu.

Toraksi imetoholewa kwa mwendo. Jozi tatu za miguu na jozi moja ya mabawa zimeunganishwa kwenye toraksi.

Fumbatio limetoholewa kwa kumeng'enya chakula na kuzalisha mayai. Sehemu hii yenye pingili huvimba sana wakati jike anapofyonza damu ambayo ni chanzo cha protini kwa uzalishaji wa mayai.

Anofelesi wanaweza kutofautishwa na mbu wengine kwa palpi zilizo ndefu kama mrija na kwa uwepo wa mabaka ya vigamba vyeusi na vyeupe juu ya mabawa. Wadumili wanaweza pia kutambuliwa kwa mkao wao wa kawaida wa kupumzika: wakikaa mahali huweka fumbatio lao kwa pembe badala ya sambamba na uso ambapo wanapumzika (tazama mchoro).

Mayai ya anofelesi.

Madume na majike wote hula mbochi na vitu vingine vyenye sukari, lakini majike wanahitaji mlo wa damu kwa kila kundi la mayai ambalo hukua katika ovari zake. Spishi nyingi zinaweza kuchukua damu kutoka kwa wanyama wengi, haswa mamalia, lakini nyingine huchagua spishi chache na kadhaa hupendelea watu.

Mkao wa kupumua wa mabuu ya anofelesi (A) kulingana na mbu asiye anofelesi (B).

Majike hutaga makundi ya mayai 50-200 kila siku 2-3. Kwa kuzingatia kuwa wastani wa maisha ni kama wiki mbili, makundi 5-6 hutagwa na kila jike, ingawa hii inaweza kuwa chache zaidi ikiwa jike atashindwa kupata mlo wa damu kwa wakati. Mayai ni madogo kiasi (karibu mm 0.5 x 0.2). Mayai hutagwa peke yao na moja kwa moja juu ya maji. Hayo ni wa kipekee kwa kuwa yana kibunzi kila upande. Hutoa lava ndani ya siku 2-3 katika ukanda wa tropiki lakini hii inaweza kuchukua hadi wiki 2-3 katika maji baridi. Mayai siyo sugu kwa kukausha.

Lava au mabuu ya anofelesi wana kichwa kilichokua vizuri chenye brashi za kinywa zinazotumiwa kujilisha, toraksi kubwa na fumbatio lenye pingili tisa. Hawana miguu. Kinyume na mbu wengine hawana neli ya kupumua, kwa hivyo hujiweka ili mwili wao uwe sambamba na uso wa maji. Walakini, ili kupumua mabuu ya spishi zisizo anofelesi hujiambatisha na uso wa maji kwa neli yao ya nyuma, na mwili wao ukielekea chini (angalia mchoro).

Mabuu hupumua kupitia spirakulo zilizopo kwenye pingili ya nane ya fumbatio, kwa hivyo lazima waje kwenye uso mara kwa mara. Wanatumia wakati wao mwingi kujilisha na miani, bakteria, na vijidudu vingine kwenye tabaka jembamba la uso. Huzama chini ya uso tu wakati wanasumbuliwa. Mabuu huogelea ama kwa mashtuko ya mwili mzima au kwa kusukuma kwa brashi ya kinywa.

Mabuu hukua kupitia hatua nne, kisha hubadilika kuwa mabundo. Mwishoni kwa kila hatua mabuu huambua kiunzi-nje, au ngozi, kuwezesha ukuaji zaidi. Mabuu ya hatua ya kwanza wana urefu wa karibu mm 1, huku mabuu ya hatua ya nne kwa kawaida wawe na urefu wa mm 5-8.

Bundo wa anofelesi.

Mabuu hutokea katika makazi anuwai, lakini spishi nyingi hupendelea maji safi yasiyonajisiwa. Mabuu ya anofelesi wamepatikana katika maji baridi au vinamasi vya maji ya chumvi, kapa, mashamba ya mpunga, mitaro yenye nyasi, kingo za vijito na mito na mabwawa madogo ya mvua ya muda mfupi. Spishi nyingi hupendelea makazi yenye mimea. Wengine wanapendelea makazi bila mimea. Fulani huzaa katika mabwawa ya wazi yenye mwanga wa jua huku wengine wapatikane tu kwenye maeneo ya kuzaliana kwa kivuli kwenye misitu. Spishi chache huzaa kwenye mashimo ya miti au makwapajani ya mimea fulani. Mwishowe, spishi nyingine huzaa katika vitu vilivyojazwa maji na vilivyotengenezwa na bidamu kama madebe, vyombo vya plastiki, matangi ya maji na hata tairi zilizotupwa.

Mabundo wana umbo la mkato wakitazamwa kutoka upande. Kichwa na toraksi zimeunganishwa kwenye kefalotoraksi na fumbatio limezunguka chini. Kama mabuu, sharti mabundo waje kwenye uso wa maji mara kwa mara ili kupumua, ambayo hufanya kupitia jozi ya tarumbeta za kupumua kwenye kefalotoraksi yao. Baada ya siku chache kama bundo, ngozi ya juu ya kefalotoraksi inapasuka na mdumili huibuka. Hatua ya bundo hudumu siku 1-3 kulingana na nyuzijoto ya maji.


Spishi kadhaa za Afrika

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mdudu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Anofelesi kama uainishaji wake wa kibiolojia, maisha au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.