Nenda kwa yaliyomo

Kuleksi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kuleksi
Kuleksi (Culex quinquefasciatus) akifyonza damu
Kuleksi (Culex quinquefasciatus) akifyonza damu
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Diptera (Wadudu wenye mabawa mawili tu)
Nusuoda: Nematocera (Diptera wenye vipapasio kama nyuzi)
Oda ya chini: Culicomorpha (Mbu kama kuleksi)
Familia: Culicidae (Mbu walio na nasaba na kuleksi)
Meigen, 1818
Jenasi: Culex
Linnaeus, 1758
Ngazi za chini

Spishi >1000.

Kuleksi ni spishi za mbu za jenasi Culex katika familia Culicidae. Spishi nyingi zinaweza kueneza ugonjwa ya vertebrata, pamoja na binadamu. Hayo yanashirikisha magonjwa yanayosababishwa na virusi, kama virusi ya Naili ya Magharibi, na pia malaria ya ndege na vijinyoo (microfilaria). Katika Afrika, vekta kuu za virusi ya Naili ya Magharibi ni Culex pipiens na C. univittatus na kwa kadiri fulani C. quinquefasciatus. Spishi ya mwisho pia ni vekta ya matende katika Afrika ya Mashariki. Spishi kadhaa za "Culex" ni vekta za malaria ya ndege kwenye Afrika.

Mkao wa kupumzika wa mdumili wa Anopheles (A, B) kulingana na mdumili wa kuleksi (C)

Kama mbu wote wadumili wa kuleksi wana mwili mwembamba mwenye sehemu tatu: kichwa, toraksi na fumbatio. Hizi ni kama katika anofelesi lakini palpi za maksila ni fupi. Kulingana na spishi wanafika urefu wa mm 4-10.

Licha ya palpi zao fupi kuleksi wanaweza kutofautishwa na anofelesi kwa ukosefu wa mabaka ya vigamba vyeusi na vyeupe juu ya mabawa. Wadumili wanaweza pia kutambuliwa kwa mkao wao wa kawaida wa kupumzika: wakikaa mahali huweka fumbatio yao sambamba na uso ambapo wanapumzika badala kwa pembe (tazama mchoro).

Madume na majike wote hula mbochi na vitu vingine vyenye sukari, lakini majike wanahitaji mlo wa damu kwa kila kundi la mayai ambalo hukua katika ovari zake. Spishi nyingi zinaweza kuchukua damu kutoka kwa wanyama wengi, na ndege mara nyingi; kadhaa hupendelea watu.

Kioleza cha mayai ya kuleksi.

Majike hutaga makundi ya mayai hadi 300 kila siku kadhaa ambayo huambatana katika kioleza kinachoelea juu ya maji. Kwa kuzingatia kuwa wastani wa maisha ni kama wiki mbili, makundi 5 yanaweza kutagwa na kila jike, ingawa hii inaweza kuwa chache zaidi ikiwa jike atashindwa kupata mlo wa damu kwa wakati. Mayai ni madogo kiasi (karibu mm 0.5 x 0.2)???. Hutoa lava ndani ya siku 2-3 katika ukanda wa tropiki lakini hii inaweza kuchukua hadi wiki 2-3 katika maji baridi.

Lava au mabuu ya kuleksi wana kichwa kilichokua vizuri chenye brashi za kinywa zinazotumiwa kujilisha, toraksi kubwa na fumbatio yenye pingili tisa. Hawana miguu. Kinyume na anofelesi wana neli ya kupumua, wanayotumia kujiambatisha na uso wa maji wakati mwili ukielekea chini. Walakini, anofelesa huweka mwili wao sambamba na uso wa maji (tazama mchoro).

Mkao wa kupumua wa buu wa anofelesi (A) kulingana na buu wa kuleksi (B)
Mchoro wa kuleksi

Mabuu wanatumia wakati wao mwingi kujilisha na dutu ya kioganiki na vijidudu anuwai. Huzama chini ya uso tu wakati wanasumbuliwa. Mabuu huogelea wa mashtuko ya mwili mzima.

Buu na bundo wa kuleksi.

Mabuu hukua kupitia hatua nne, kisha hubadilika kuwa mabundo. Mabundo] wana umbo la mkato wakitazamwa kutoka upande. Kichwa na toraksi zimeunganishwa kwenye kefalotoraksi na fumbatio limezunguka chini. Kama mabuu, sharti mabundo waje kwenye uso wa maji mara kwa mara ili kupumua, ambayo hufanya kupitia jozi ya tarumbeta za kupumua kwenye kefalotoraksi yao. Baada ya siku chache kama bundo, ngozi ya juu ya kefalotoraksi inapasuka na mbu mdumili huibuka. Hatua ya bundo hudumu siku 1-5 kulingana na spishi na nyuzijoto ya maji.

Spishi nyingi za kuleksi hupenda kutaga mayai kwenye miili midogo ya maji iliyo na dutu ya kioganiki, pamoja na madimbwi, mabwawa, mitaro, debe, ndoo, chupa na matangi ya kuhifadhi maji (mashimo katika miti yanafaa spishi chache tu). Muda kutoka kwa kutaga mayai hadi kujitokeza kwa mdumili unategemea halijoto lakini ule wa chini ni siku saba.

Spishi kadhaa za Afrika

[hariri | hariri chanzo]
  • Culex antennatus
  • Culex neavei
  • Culex pipiens
  • Culex quinquefasciatus
  • Culex theileri
  • Culex tritaeniorhynchus
  • Culex univittatus