Amri Kumi
Amri Kumi ni orodha ya amri kuu za Mungu katika Biblia. Za kwanza zinamhusu Mwenyezi Mungu mwenyewe, na zile zinazofuata mpaka mwisho zinahusu jirani, yaani binadamu wengine kuanzia wazazi.
Toleo la awali linapatikana katika kitabu cha Kutoka 20:1-17. Toleo la pili liko katika Kumbukumbu la Torati 5:1-21.
Amri hizi ni sehemu ya Torati ya Kiyahudi na kukubaliwa pia na Wakristo walio wengi kama amri zinazowahusu wao pia, tena wanaziona kuwa kimsingi zinawadai watu wote.
Hata hivyo wafuasi wa Yesu Kristo wanazishika kadiri ya utimilifu wake ulioletwa naye kama Agano Jipya. Mifano ya ukamilisho huo ni mafundisho ya Yesu katika Injili ya Mathayo 5:17-48.
Maneno ya Amri Kumi
[hariri | hariri chanzo]Maneno yanayojulikana kama “Amri Kumi” yanapatikana katika vitabu vya Biblia "Kutoka" na "Kumbukumbu la Torati".
Kitabu cha Kutoka 20:2–17 | Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:6–21 |
---|---|
2. Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 3. Usiwe na miungu mingine ila mimi. |
6. Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 7. Usiwe na miungu mingine ila mimi. |
Mpangilio wa Amri Kumi
[hariri | hariri chanzo]Maneno katika Kutoka 20 huwa na amri mbalimbali. Namba kumi ni hesabu iliyotiwa baadaye katika orodha hii, haikuwa nia asili kuwa na amri “10” kamili. Ila tu wakati wa Biblia ilikuwa kawaida tayari kuziita "amri 10", lakini bila kuonyesha namba au mpangilio katika maneno ya Biblia yenyewe.
Hali hii ilisababisha tofauti ndogo katika hesabu ya amri hizi kati ya mapokeo ya madhehebu mbalimbali. Tofauti kuu ni kati ya Wayahudi wakifuatwa na Wakristo mbalimbali kwa upande mmoja na Wakatoliki pamoja na Walutheri na Wamoravian kwa upande mwingine kuhusu kutokuwa na sanamu za kuchonga. Tangu Agostino wa Hippo Wakatoliki walijumlisha sehemu kuhusu kutoabudu sanamu za kuchongwa pamoja na amri ya kutokuwa na miungu mingine. Kwa kufikia namba kumi Agostino aligawa sehemu ya mwisho kuwa amri mbili. Martin Luther alimfuata Agostino lakini Wareformed waliona mpangilio tofauti wakaihesabu kama amri ya pekee.
Amri | Wayahudi | Waanglikana, Wareformed na wengineo | Waorthodoksi | Wakatoliki, Walutheri, Wamoravian |
---|---|---|---|---|
Mimi ni Bwana Mungu wako | 1 | (utangulizi) | 1 | 1 |
Usiwe na miungu mingine ila mimi | 2 | 1 | ||
Usijifanyie sanamu ya kuchonga | 2 | 2 | ||
Usilitaje bure jina la Bwana | 3 | 3 | 3 | 2 |
Ikumbuke siku ya sabato uitakase | 4 | 4 | 4 | 3 |
Waheshimu baba yako na mama yako | 5 | 5 | 5 | 4 |
Usiue | 6 | 6 | 6 | 5 |
Usizini | 7 | 7 | 7 | 6 |
Usiibe | 8 | 8 | 8 | 7 |
Usishuhudie jirani yako uongo | 9 | 9 | 9 | 8 |
Usiitamani nyumba ya jirani yako Usitamani mke wake |
10 | 10 | 10 | 9 |
Usiitamani cho chote alicho nacho jirani yako | 10 |
Amri Kumi katika Ukristo
[hariri | hariri chanzo]Katika Ukristo, amri za Mungu alizopewa Musa zinatazamiwa kutekelezwa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, anayeweka wafuasi wa Yesu huru kutoka utumwa wa sheria, kwa sababu ni masharti ya upendo yaliyodaiwa na Yesu pia. “Ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili: Umpende jirani yako kama nafsi yako” (Gal 5:13-14). “Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu: tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito” (1Yoh 5:2-3).
Yesu alidai wafuasi wake washike amri za Mungu ili waufikie uzima wa milele. “Tazama, mtu mmoja alimwendea akamwambia, ‘Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?’ Akamwambia, ‘Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri’. Akamwambia, ‘Zipi?’ Yesu akasema, ‘Ni hizi: Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako, na, mpende jirani yako kama nafsi yako” (Math 19:16-19).
Bila kushika amri hizo mtu hawezi kutukuzwa mbinguni kwa sababu anaonyesha hajali vya kutosha uhai, utakatifu wa ndoa, mali ya watu, ukweli, heshima kwa wakubwa na upendo kwa watu kwa jumla. Kupuuzia tunu hizo muhimu ni kumpuuzia Muumba aliyeziweka ziongoze wote maishani. “Ee Israeli, tu heri sisi, maana mambo yampendezayo Mungu yamejulishwa kwetu” (Bar 4:4). “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi” (1Kor 6:9-10). “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati, wala mchafu, wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu” (Ef 5:5).
Injili haitaji amri zinazohusu ibada kwa Mungu kwa sababu Yesu aliona haja ya kusisitiza zile zinazohusu jirani, na kwa sababu hakutaka hizo za kwanza zifuatwe na Kanisa lake kama Wayahudi wanavyofanya. “Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha... Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu” (Yoh 2:19; 5:18). “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia” (Mk 2:28). “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16-17). “Basi, torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zilezile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao... Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana, maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu” (Eb 10:1; 13:16).
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Aaron, David H (2006). Etched in Stone: The Emergence of the Decalogue. Continuum. ISBN 0-567-02791-0.
- Abdrushin (2009). The Ten Commandments of God and the Lord's Prayer. Grail Foundation Press. ISBN 1-57461-004-X. http://the10com.org/index.html Archived 23 Mei 2010 at the Wayback Machine.
- Barenboim, Peter (2005), Biblical Roots of Separation of Powers, Moscow: Letny Sad, ISBN 5-94381-123-0.
- Freedman, David Noel (2000). The Nine Commandments. Uncovering a Hidden Pattern of Crime and Punishment in the Hebrew Bible. Doubleday. ISBN 0-385-49986-8.
- Friedman, Richard Elliott (1987). Who Wrote the Bible?. Englewood Cliffs, NJ: Prentice Hall. ISBN 0-671-63161-6.
- Hazony, David (2010). The Ten Commandments: How Our Most Ancient Moral Text Can Renew Modern Life. New York: Scribner. ISBN 1-4165-6235-4.
- Kaufmann, Yehezkel (1960). The Religion of Israel, From Its Beginnings To the Babylonian Exile. trans. Moshe Greenberg. Chicago: University of Chicago Press.
- Kuntz, Paul Grimley (2004). The Ten Commandments in History: Mosaic Paradigms for a Well-Ordered Society. Wm B Eerdmans Publishing, Emory University Studies in Law and Religion. ISBN 0-8028-2660-1.
- Mendenhall, George E (2001). Ancient Israel's Faith and History: An Introduction To the Bible In Context. Louisville: Westminster John Knox Press. ISBN 0-664-22313-3.
- Mendenhall, George E (1973). The Tenth Generation: The Origins of the Biblical Tradition. Baltimore: Johns Hopkins University Press. ISBN 0-8018-1267-4.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Ulinganishaji wa matoleo ya Amri Kumi katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, tafsiri ya Kiingereza, katika tovuti ya Vatikani. Katika kurasa zinazofuata kuna ufafanuzi mrefu wa amri hizo kwa jumla na mojamoja
Makala hii kuhusu mambo ya Agano la Kale bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Amri Kumi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |