Nenda kwa yaliyomo

Akili mnemba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 08:23, 24 Juni 2024 na Riccardo Riccioni (majadiliano | michango) (Riccardo Riccioni moved page Akili bandia to Akili mnemba over redirect: usahihi wa jina)
Kismet, kichwa cha roboti chenye uwezo wa kutambua na kuiga hisia za kibinadamu.

Akili mnemba (kwa Kiingereza: Artificial Intelligence, kifupi: AI) ni nadharia na uundaji wa mifumo ya kompyuta yenye uwezo wa kutekeleza kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili ya binadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha.

Teknolojia ya akili mnemba inatumika kwa kiwango kikubwa viwandani, serikalini, na kwenye tafiti za kisayansi. Baadhi ya matumizi yenye wasifu mkubwa ya akili mnemba ni pamoja na injini za utafutaji wa tovuti (kama ile ya Google), mifumo ya mapendekezo (inayotumika kwenye programu tumishi za YouTube, Tiktok, Amazon, na Netflix), kwenye utambuzi wa hotuba za binadamu (kama Google Assistant, Siri na Alexa), kwenye magari yanayojiendesha (kama Waymo), kwenye mifumo mikubwa ya lugha (inayotumika kwenye roboti za mazungumzo kama ChatGPT na Gemini), kwenye mifumo ya uzalishaji picha kama DALL-E na michezo ya kimkakati (kama Chess na Go) [1].

Akili mnemba kama taaluma ya sayansi ilianza rasmi mwaka 1956, neno "Akili mnemba" lilitungwa na John McCarthy, mwanasayansi wa kompyuta wa Marekani katika mkutano wa kwanza wa Akili mnemba uliofanyika kwenye chuo cha Dartmouth [2].

Tafiti mbalimbali za akili mnemba zina malengo tofauti na hutumia njia tofauti kufikia malengo hayo. Malengo yaliyozoeleka ya tafiti ya akili mnemba ni pamoja na ufikiriaji, uwasilishaji wa maarifa, upangaji, kujifunza, usindikaji wa lugha asili, utambuzi, na usaidizi wa roboti. Akili ya jumla (uwezo wa kukamilisha kazi yoyote inayowezwa kufanywa na binadamu) ni moja kati ya malengo ya muda mrefu ya taaluma hii.

Ili kufikia malengo hayo, watafiti wa akili mnemba wametumia na kuunganisha njia mbalimbali za kutatua matatizo, zikiwemo za utafutaji na uboreshaji wa kihisabati, mantiki rasmi, mitandao ya neva bandia, na njia nyingine zinazotegemea takwimu, utafiti shughuli na uchumi. Akili mnemba pia inategemea elimunafsia, isimu, falsafa, sayansi neva na nyanja nyingine.

Marejeo

  1. "AlphaGo". Google DeepMind (kwa Kiingereza). 2020-12-23. Iliwekwa mnamo 2024-01-02.
  2. "Artificial Intelligence (AI) Coined at Dartmouth | Dartmouth". home.dartmouth.edu (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2024-01-02.

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.