Nenda kwa yaliyomo

Akili mnemba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kismet, kichwa cha roboti chenye uwezo wa kutambua na kuiga hisia za kibinadamu.

Akili mnemba (kwa Kiingereza: Artificial Intelligence, kifupi: AI) ni nadharia na uundaji wa mifumo ya kompyuta yenye uwezo wa kutekeleza kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili ya binadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha.

Teknolojia ya akili mnemba inatumika kwa kiwango kikubwa viwandani, serikalini, na kwenye tafiti za kisayansi. Baadhi ya matumizi yenye wasifu mkubwa ya akili mnemba ni pamoja na injini za utafutaji wa tovuti (kama ile ya Google), mifumo ya mapendekezo (inayotumika kwenye programu tumishi za YouTube, Tiktok, Amazon, na Netflix), kwenye utambuzi wa hotuba za binadamu (kama Google Assistant, Siri na Alexa), kwenye magari yanayojiendesha (kama Waymo), kwenye mifumo mikubwa ya lugha (inayotumika kwenye roboti za mazungumzo kama ChatGPT na Gemini), kwenye mifumo ya uzalishaji picha kama DALL-E na michezo ya kimkakati (kama Chess na Go) [1].

Akili mnemba kama taaluma ya sayansi ilianza rasmi mwaka 1956, neno "Akili mnemba" lilitungwa na John McCarthy, mwanasayansi wa kompyuta wa Marekani katika mkutano wa kwanza wa Akili mnemba uliofanyika kwenye chuo cha Dartmouth [2].

Tafiti mbalimbali za akili mnemba zina malengo tofauti na hutumia njia tofauti kufikia malengo hayo. Malengo yaliyozoeleka ya tafiti ya akili mnemba ni pamoja na ufikiriaji, uwasilishaji wa maarifa, upangaji, kujifunza, usindikaji wa lugha asili, utambuzi, na usaidizi wa roboti. Akili ya jumla (uwezo wa kukamilisha kazi yoyote inayowezwa kufanywa na binadamu) ni moja kati ya malengo ya muda mrefu ya taaluma hii.

Ili kufikia malengo hayo, watafiti wa akili mnemba wametumia na kuunganisha njia mbalimbali za kutatua matatizo, zikiwemo za utafutaji na uboreshaji wa kihisabati, mantiki rasmi, mitandao ya neva bandia, na njia nyingine zinazotegemea takwimu, utafiti shughuli na uchumi. Akili mnemba pia inategemea elimunafsia, isimu, falsafa, sayansi neva na nyanja nyingine.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Wazo la mashine zinazofikiri lina historia ndefu inayotangulia teknolojia ya kisasa. Mawazo ya awali kuhusu mashine zenye uwezo wa kufikiri au kuchukua maamuzi yalionekana katika falsafa ya Kigiriki, hadithi za kale, na baadaye maandiko ya karne ya 17 na 18 kama ya Gottfried Leibniz na Thomas Hobbes waliodokeza kuwa fikra za kibinadamu zinaweza kueleweka kama mchakato wa kihisabati. Hata hivyo, maendeleo halisi ya Akili Mnemba (AI) kama taaluma ya kisayansi yalianza katikati ya karne ya 20.

Mwaka 1956 unachukuliwa kama mwanzo rasmi wa AI kama uwanja wa utafiti, kufuatia Mkutano wa Dartmouth uliowakutanisha wanasayansi kama John McCarthy (aliyeasisi jina "Artificial Intelligence"), Marvin Minsky, Allen Newell, na Herbert Simon. Katika miaka ya 1950 na 60, AI ilizalisha matumaini makubwa, huku kompyuta za kwanza zikitengenezwa na programu zinazoweza kutatua matatizo ya kihisabati au kucheza michezo kama chess. Hata hivyo, ukosefu wa uwezo wa kompyuta na maarifa ya kutosha kuhusu lugha na hisia za binadamu ulisababisha kipindi cha kusuasua katika maendeleo hayo kilichoitwa "AI winter."

Kuanzia miaka ya 1990 na kuendelea, AI ilianza kupata mafanikio mapya kwa msaada wa kompyuta zenye kasi zaidi, data kubwa (big data), na mbinu mpya kama machine learning na deep learning. Mafanikio makubwa kama ushindi wa kompyuta Deep Blue dhidi ya bingwa wa chess Garry Kasparov mwaka 1997, na baadaye mafanikio ya AlphaGo dhidi ya bingwa wa mchezo wa Go mwaka 2016, yalionyesha uwezo mkubwa wa AI. Katika karne ya 21, matumizi ya AI yameenea katika sekta kama afya, usafiri, mawasiliano, na huduma za kifedha, huku masuala ya kimaadili na usalama wa kiteknolojia yakichukua nafasi kubwa katika mijadala ya kisasa ya kisayansi na kijamii.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. "AlphaGo". Google DeepMind (kwa Kiingereza). 2020-12-23. Iliwekwa mnamo 2024-01-02.
  2. "Artificial Intelligence (AI) Coined at Dartmouth | Dartmouth". home.dartmouth.edu (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2024-01-02.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.