Utitiri-utando mwekundu
Utitiri-utando mwekundu | ||||||||||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Koloni ya utitiri-utando mwekundu
| ||||||||||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||||||||||
|
Utitiri-utando mwekundu (Tetranychus evansi) ni utitiri wa familia Tetranychidae katika oda Trombidiformes aliye msumbufu mbaya katika mashamba ya mboga. Inashambulia spishi za mimea za familia Solanaceae hasa na nyingi nyingine pia.
Kwa asili spishi hii ilitokea Amerika ya Kusini lakini siku hizi imevamia mahali pengi duniani, katika tropiki na nusutropiki hasa, kama vile Afrika kusini kwa Sahara, nchi za Bahari ya Kati, Asia ya Mashariki-Kusini na Australia.
Maelezo
[hariri | hariri chanzo]Hao ni matitiri wadogo na urefu wa majike ni mm 0.5 na wa madume ni mm 0.4. Rangi ya majike ni machungwa hadi nyekundu iliyoiva na kuna mabaka meusi yasiyo dhahiri kila upande wa mwili na miguu ina rangi ya machungwa isiyoiva. Madume ni machungwa-njano wenye miguu ya rangi ya machungwa isiyoiva. Mgongo una jozi 13 za manyoya mafupi na makunyanzi ya mgongo yanafuata urefu na kuunda muundo wa umbo la almasi juu ya jozi za tatu na za nne za miguu.
Majike wanaweza kutaga mayai hadi 200. Matitiri hao wanahitaji nyuzijoto ya juu ya 10.3ºC ili kukua. Kwa 36ºC hupitia hatua zote za maisha yao katika muda wa wiki moja. Baada ya yai kuna hatua moja ya lava na hatua mbili za tunutu (protonymph na deutonymph) na mwishowe mpevu. Mayai yasiyotungwa ya matitiri-utando hutoa madume na mayai yaliyotungwa hutoa majike (arrhenotoky).
Mimea vidusiwa
[hariri | hariri chanzo]Matitiri hao hujilisha kwa mimea ya familia Solanaceae hasa. Mimea mingine inayodusiwa ni miharagwe na mpamba na maua ya mapambo kama miwaridi. Magugu mengi kama Amaranthus, Chenopodium na Convolvulus hudusiwa pia.
Kwa kawaida matitiri wako kwenye upande wa chini wa majani, lakini utando wao unaweza kufunika mmea mzima. Wanaweza kutawanywa na upepo, maji ya umwagiliaji na wafanyakazi (juu ya mavazi na vyombo) na kwa mbali kubwa kwa njia ya biashara ya mimea.
Udhibiti
[hariri | hariri chanzo]Aina fulani za mazao, haswa za nyanya, zinapinga mashambulio kwa sababu ya nywele fupi kwenye majani na shina. Kupogoa na kuweka mashina kwenye waya hufanya iwe rahisi kudhibiti matitiri.
Dawa nyingi za kikemikali hazina ufanisi sana dhidi ya matitiri-utando. Pirethroidi zimekuwa na ufanisi lakini sasa zinapoteza ufanisi wao. Ufanisi wa bidhaa za mwarobaini na sulfidi ya kalisi bado ni ya kuridhisha. Walakini, siku hizi, udhibiti wa kibiolojia unazidi kupata umuhimu. Njia ya chaguo katika vibanda vya kukuzia mazao ni matumizi ya utitiri-mbuai Phytoseiulus longipes. Katika mashamba ya nje dawa za kibiolojia zinaweza kutumika, kama vile dawa zilizo na kuvu Metarhizium anisopliae au Beauveria bassiana ndani yao.