Reale

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Reale ya Shamu (Dolar ya Maria Theresa)

Reale (pia: riale) ilikuwa jina la pesa kwenye Pwani la Afrika ya Mashariki wakati wa karne ya 19. Kwa kawaida ilimaanisha "Reale ya Shamu" jinsi Dolar ya Maria Theresa ilivyoitwa hapa na jina hili ikatumiwa pia kwa sarafu nyingine za fedha.

Asili ya jina[hariri | hariri chanzo]

Reale ni jina lenye asili ya Kireno[1] kwa maana ya "kifalme" lililofika katika mazingira ya Uswahilini tangu safari ya nahodha Mreno Vasco da Gama aliyevuka Rasi ya Tumaini Jema mnamo mwaka 1498 na kufika Uhindi kupitia Mombasa. Jina liliendelea kutumiwa katika Uarabuni na Afrika ya Mashariki kwa sarafu za fedha kutoka nchi mbalimbali. Katika nchi za Kiarabu jina limeendelea kwa pesa ya leo inayoitwa "Riyal" huko Oman, Saudia na Iran.

Reale ya karne ya 19[hariri | hariri chanzo]

Miji ya Waswahili haikutoa pesa zao za pekee bali ilitumia sarafu za nje. Hapo wafanya biashara waliangalia thamani ya sarafu hizi katika Uarabuni kusini na Uhindi kwa sababu hizi zilikuwa nchi muhimu zaidi kwa biashara ya nje.

Katika karne ya 19 "reale" ilitumiwa katika Afrika ya Mashariki kwa sarafu za fedha kutoka nchi mbalimbali. Hasahasa ilimaanisha sarafu za Dolar ya Maria Theresa au Maria-Theresien-Thaler. Pesa hii ilitolewa nchini Austria wakati wa malkia Maria Theresa kuanzia mwaka 1741. Ilisambaa haraka katika nchi za Mediteranea na Milki ya Osmani hadi Uarabuni ilipendwa kwa sababu asilimia ya fedha ndani yake haikupungua. Kutokana na madai Austria iliendelea kutoa sarafu hii hata baada ya kifo cha malkia mwaka 1780. Dolar ya Maria Theresa iliendelea kuwa pesa kuu Uarabuni na Ethiopia ikawa pia pesa ya kawaida Uswahilini, ikiitwa hapa "reale ya Shamu" na kutumiwa pamoja na rupia ya Kihindi kwa kubadilisha rupia mbili kwa reale moja.[2]

Sarafu hii (inayotolewa hadi leo kwa wakusanyaji wa sarafu) ina kipenyo cha milimita 39.5 na uzani wa gramu 28; kiwango cha fedha ndani yake ni 833⅓/1000 hivyi ina gramu 23.389 za fedha tupu.

Katika karne ya 19 sarafu hii ilitumiwa pia kama kipimo cha uzani wa wakia au aunsi moja.[3]

Jina reale kwa sarafu za Hispania na Ufaransa[hariri | hariri chanzo]

Reale mzinga (Real ya Hispania)

Kulikuwa pia na sarafu za Hispania na Ufaransa zilizoitwa "reale" ambazo zilifanana kwa uzani na kiasi cha fedha na reale ya Shamu.

"Reale mzinga" ilikuwa jina la "columnario" ya Kihispania, sarafu ya real nane za Kihispania yenye uzani wa gramu 27[4] na jina lilitokana na nguzo mbili kwenye uso wake.

Sarafu ya franc tano za Kifaransa ilijulikana kama "Reale ya Fransa"[5] ikiwa nyepesi kidogo kuliko Reale ya Shamu na Reale mzinga kwa gramu 25 lakini kiwango cha fedha ilikuwa 9000/1000 ikiwa na kipenyo cha milimita 37.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Real" ni pia neno la Kihispania, na hivyo jina la pesa ya fedha katika nchi jirani mbili wakati wa karne za kati hadi karne ya 19.
  2. Madan, uk 325
  3. Krapf 1882, uk 422: "Wakia, a weight of one dollar (small weight); ni uzito wa reali; e.g. the weight of a dollar when given for the same weight of something else; the dollar was formerly used as a weight"
  4. Columnario Archived 20 Machi 2018 at the Wayback Machine., tovuti iliangaliwa 24-03-2017
  5. Madan uk. 325