Nenda kwa yaliyomo

Kunguni-makasia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kunguni-makasia
Sigara fossarum
Sigara fossarum
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu, nge, buibui)
Nusufaila: Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita)
(bila tabaka): Dicondylia (Wadudu walio na mandibula zenye condyle mbili)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Nusungeli: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda ya juu: Paraneoptera
Oda: Hemiptera
Haeckel, 1896
Nusuoda: Heteroptera
Oda ya chini: Nepomorpha
Familia ya juu: Corixoidea
Familia: Corixidae
Leach, 1815
Ngazi za chini

Nusufamilia 5, jenasi 52, ?? katika Afrika ya Mashariki:

Kunguni-makasia ni wadudu wadogo wa maji wa familia Corixidae katika oda ya chini Nepomorpha ya oda Hemiptera wanaoogelea chini ya uso wa maji kwa msaada wa miguu yao ya nyuma inayofanana na makasia. Kinyume na kunguni-maji wengine, walio mbuai, kunguni-makasia hufyonza kiowevu cha mimea. Kuna takriban spishi 500 zinazotokea duniani kote kwa ujumla katika maji matamu lakini nyingi kiasi katika maji ya chumvi kidogo au hata maji ya bahari[1].

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Kunguni-makasia wana urefu wa mm 4-16. Mwili wao ni kama duaradufu iliyorefuka na kuwa mwembamba wenye miguu mirefu ya nyuma kama makasia. Wanafanana na waogeleaji-juuchini, lakini hawa wa mwisho huogelea juu chini na kuwinda wadudu wengine. Pia hukosa mistari myeusi sambamba kwenye pronoto na mabawa wa mbele ambayo kunguni-makasia wanayo[2].

Biolojia[hariri | hariri chanzo]

Wadudu hawa huogelea chini ya uso wa maji karibu na sakafu ambapo hutafuta chakula kama viani, diatoma, protozoa, nematoda na wadudu wadogo. Hawako wa kawaida miongoni mwa kunguni-maji kwa kuwa baadhi ya spishi si mbuai bali hula mimea na miani, ambayo huitoboa kwa kinywa chenye umbo la mrija na kuiingizia mate ambayo hufanya tishu zao kuwa kiowevu[3]. Kiowevu hiki kisha hufyonzwa. Hata hivyo, spishi nyingi sana si walamani kabisa na wanaweza hata kuwa mbuai kabisa, kama zile za nusufamilia Cymatiainae[4]. Kwa hakika, kunguni-makasia wana aina mbalimbali za mitindo ya kujilisha: walanyama, walataka, walamani na walavyote.

Miguu mifupi ya mbele hutumika ili kushikilia mimea na chembe za chakula na ile mirefu ya nyuma ili kuogelea. Miguu ya mbele hutumiwa pia kutoa sauti kwa kusugua vigingi juu yao dhidi ya miinuko juu ya kichwa ili kuvuta jike.

Kunguni-makasia huishi katika maji tamu hadi ya chumvi yenye uoto na dutu nyingi ya kioganiki, kama vile maziwa, mabwawa, mito inayotiririka polepole, vinamasi, nyangwa na ghuba tulivu. Wana mabawa yaliyostawi vizuri na huruka vizuri. Wanavutiwa na mwanga wakiruka. Mwili wao, hasa mabawa ya mbele, umefunikwa kwa nywele ndogo sana zinazoelekea ndani ambazo waogeleaji-juuchini hutumia kunasa mapovu ya hewa, ambayo inaongeza muda wanaoweza kutumia chini ya maji. Mdudu anapomaliza chanzo chake cha oksijeni, lazima arudi kwenye uso ili kupata hewa zaidi[3].

Wakati wa kupandana kunguni-makasia huruka kwa makundi ya wadudu hadi elfu kadhaa juu ya maji na kingo zake[2]. Baada ya kupandana, majike hurudi majini na kutaga mayai kwenye mimea. Baada ya wiki moja au mbili tunutu huibuka wanaoonekana kama matoleo madogo ya wapevu. Wanapitia hatua 5 kabla ya kukua mabawa na kuwa wapevu.

Spishi kadhaa za Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

  • Agraptocorixa dakarica
  • Agraptocorixa gestroi
  • Sigara chinana
  • Sigara hieroglyphica
  • Sigara pectoralis
  • Sigara sjostedti

Picha[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Randall T. Schuh; James Alexander Slater (1996). True Bugs of the World (Hemiptera:Heteroptera): Classification and Natural History (toleo la 2). Cornell University Press. ku. 119–122. ISBN 978-0801420665.
  2. 2.0 2.1 https://pondinformer.com/water-boatman-corixidae/
  3. 3.0 3.1 https://nathistoc.bio.uci.edu/hemipt/Corixid.htm
  4. Nieser, N. (2002): Guide to aquatic Heteroptera of Singapore and Peninsular Malaysia. IV. Corixoidea. The Raffles Bulletin of Zoology 50: 26-274.