Nenda kwa yaliyomo

Kichocho

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kichocho
(bilharzia, schistosomiasis)
Mwainisho na taarifa za nje
SpecialtyInfectious diseases Edit this on Wikidata
ICD-10B65.
ICD-9120
MedlinePlus001321
MeSHD012552

Kichocho, kisalisali au kisonono cha damu (pia schistosomiasis au bilharzia) ni ugonjwa ambao minyoo midogo ya aina ya Schistosoma (minyoo-kichocho) inaingia mwilini na kusababisha mwasho wa ngozi katika viungo mbalimbali, homa, udhaifu na baada ya muda damu katika kinyesi au mkojo na maumivu tumboni. [1]

Habari za msingi[hariri | hariri chanzo]

 • Kuna takriban watu milioni 200 duniani walioambukizwa na kichocho.
 • Asilimia kubwa wanaishi Afrika kwenye maeneo ambako hadi nusu ya wakazi wote wameambukizwa [2]
 • Hali ya ugonjwa inatokea ama polepole ambako wagonjwa mara nyingi hawana dalili kwa muda mrefu ama kwa mwendo mkali.
 • Utambuzi wake hufanyika kwa kuchunguza mavi, mkojo au damu.
 • Tiba kwa kawaida ni dawa ya praziquantel. Kama ugonjwa haukuendelea kwa muda mrefu mno wagonjwa wanaweza kupona kikamilifu wakitibiwa. [3]

Maambukizi[hariri | hariri chanzo]

Mzunguko wa minyoo-kichocho kati ya binadamu na konokono na hali za maendeleo yao.

Minyoo-kichocho inaendelea kwa hatua zifuatazo:

 • mnyoo mpevu anatega mayai yanayotolewa pamoja na kinyesi au mkojo
 • mayai yakifika katika maji yanabadilika kuwa lava aina ya mirasidio
 • mirasidio zinatafuta konokono wa maji, zinaingia na kuzaana bila ngono ndani ya konokono
 • baada ya muda fulani lava aina ya serkari zinatoka nje na kumtafuta binadamu zikitoboa ngozi yake na kuingia katika mzunguko wa damu
 • lava zinazunguka mwilini hadi kufikia ini, hapa zinakua kuwa minyoo wapevu wenye urefu wa mm 10-20 wanaokaa katika mishipa ya damu wanapotaga mayai
 • mayai huvurugisha kingamwili na kusababisha kuwaka kwa mishipa ya ndani ya mwili (yaani ugonjwa wenyewe), yanaingia katika viungo vya mkojo au utumbo mpana yanapotoka tena mwilini[4]

Kwa hiyo maisha ya Schistosoma na nafasi ya maambukizi huhitaji:

 • mwili wa binadamu (kwa aina nyingine ya wanyama pia)
 • konokono ya maji
 • mazingira ambako konokono wanastawi: maji ya bwawa au ziwa yenye mimea ya majini inayofaa kama chakula cha konokono
 • watu wagonjwa wanakojolea kwenye maji au kuacha kinyesi chao mle

Kwa hiyo njia ya kuambukizwa ni kuingia katika maji yenye konokono walioambukizwa. Siku hizi karibu kila ziwa au bwawa katika Afrika huwa na hatari ya kichocho; hatari inapungua katika mito yenye mwendo wa maji au katika sehemu ya maziwa makubwa ambako kuna pwani pana ya mchanga bila mimea iliyo chakula cha konokono.

Kinga na tiba[hariri | hariri chanzo]

Taratibu wa kukinga dhidi ya maradhi haya ni pamoja na upatakanaji wa maji safi na upungufu wa idadi ya konokono. Katika maeneo ambako maradhi yanaambukiza zaidi, makundi ya watu wengi wanaweza kutibiwa kwa wakati mmoja, kwa kuwapa mara moja kwa mwaka dawa iitwao praziquantel. Utaratibu huo unakusudia kupunguza idadi ya watu wanaoambukizwa na kwa hivyo kupunguza kuenezwa kwake maradhi yenyewe.

Praziquantel ni dawa inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani kwa ajili ya wale wanaojulikana kuambukizwa.[5].

Historia ya matibabu[hariri | hariri chanzo]

Theodor Bilharz aliyetambua minyoo inayosababisha Kichocho

Ugonjwa na kidusia chake vilitambuliwa mara ya kwanza mwaka 1851 na tabibu Mjerumani Theodor Bilharz alipochunguza maiti katika hospitali moja mjini Kairo, nchini Misri . Kwa hiyo ugonjwa umejulikana pia kwa jina la Bilharzia.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. http://www.nhs.uk/Conditions/schistosomiasis/Pages/Introduction.aspx
 2. http://www.who.int/schistosomiasis/en/ Schistosomiasis A major public health problem. World Health Organization. Iliangaliwa mnamo disemba 2015
 3. Patient Info schistosomiasis, imeangaliwa Disemba 2015
 4. WHO Fact sheet N°115 on Schistosomiasis, updated May 2015, imeangaliwa disemba 2015
 5. CDC Yellow Book, chapter 3, Schistosomiasis imeangaliwa disemba 2015
Makala hii kuhusu mambo ya tiba bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kichocho kama sababu yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.