Tabora (mji)
Tabora | |
Mahali pa mji wa Tabora katika Tanzania |
|
Majiranukta: 5°0′36″S 32°49′12″E / 5.01000°S 32.82000°E | |
Nchi | Tanzania |
---|---|
Mkoa | Tabora |
Wilaya | Tabora |
Idadi ya wakazi | |
- Wakazi kwa ujumla | 308,741 |
Tabora ni mji wa kihistoria wa Tanzania ya Kati na makao makuu ya mkoa wa Tabora wenye postikodi namba 45100. Eneo lake ni manisipaa yenye hadhi ya wilaya.
Mwaka 2012 palikuwa na wakazi 226,999. Katika sensa ya mwaka 2022 walihesabiwa 308,741 [1].
Historia
[hariri | hariri chanzo]Mji ulianzishwa na wafanyabiashara Waarabu na Waswahili kutoka Zanzibar mnamo 1825. Waliutumia kama kituo kwenye njia ya biashara ya misafara kati ya pwani ya Bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika katika nusu ya kwanza ya karne ya 19. Biashara kuu zilikuwa ndovu pamoja na watumwa. Tabora walijenga nyumba imara pamoja na ghala za bidhaa kwa ajili ya biashara hizo. Familia ya Tippu Tip ilikuwa kati ya wenye nyumba wa Tabora.
Mwaka 1871 jeshi la rugaruga wa Mtemi Mirambo lilishambulia mji. Ukajengwa upya. Tangu mwaka 1890 Wajerumani walianza kufika na baada ya kushinda Wanyamwezi walifanya Tabora kuwa kitovu chao katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ya kati; mji ukawa kituo cha kikosi cha jeshi na pia kikosi cha polisi. Hata hivyo, Tabora ilikuwa mji mkubwa wa koloni la Kijerumani mbali na miji ya pwani.
Umuhimu wa Tabora ukaongezeka kwa ujenzi wa reli ya kati iliyounganisha pwani na Ziwa Tanganyika ikipita Tabora kuanzia mwaka 1912. Karakana muhimu ya reli ikawekwa huko mjini. Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia pesa ya mwisho iliyotolewa na Wajerumani katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ilitengenezwa katika karakana ya reli mwaka 1916 maana Dar es Salaam ilikuwa tayari mikononi mwa Waingereza.
Mwaka 1916 Tabora ilivamiwa na Wabelgiji waliowafukuza Wajerumani lakini baada ya vita kuu kwisha mji ukawa sehemu ya Tanganyika.
Mwka 1964 kikosi cha pili cha Tanganyika Rifles cha Tabora kiligoma kikiunga mkono wenzake huko Dar es Salaam[2]. Baada ya kumaliza uasi bila kumwaga damu, kikosi hicho kilifutwa[3].
Usafiri
[hariri | hariri chanzo]Hadi leo Tabora ni kitovu muhimu cha mawasiliano cha Tanzania ya kati. Barabara za kufika mji zimeboreshwa, kuna njia ya lami kwenda Itigi - Dodoma, na pia kuelekea Nzega. Njia ya kwenda Kigoma imefika Mto Malagarasi kwa hali ya lami. Malori kutoka Dar es Salaam kuelekea Rwanda, Burundi au Kongo hupitia Tabora. Reli inapeleka abiria na mizigo kutoka Tabora kwenda Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza kwa kutumia mkono wa kaskazini wa njia ya reli iliyojengwa wakati wa ukoloni wa Kiingereza.
Njia mpya ya reli ya SGR inajengwa tangu mwaka 2020 kuelekea Mwanza na Dodoma- Dar es Salaam.
Kuna pia uwanja mdogo wa ndege.
Picha za Tabora
[hariri | hariri chanzo]-
Mtaa wa Tabora mnamo 1911
-
Boma la Kijerumani mnamo 1911 (leo kituo cha JWTZ)
-
Hoteli ya Tabora tangu enzi za Wajerumani (Leo Tabora Orion Hotel)
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ https://www.nbs.go.tz
- ↑ The Second Battalion Tanganyika Rifles also mutinied in Tabora.
- ↑ The East African mutinies of 1964, Mark Baynham 2008
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Red dots are rail lines
- Columbia Encyclopedia, Sixth Edition (at encyclopedia.com)
- Tabora page at fizzylogic.com Ilihifadhiwa 4 Mei 2006 kwenye Wayback Machine.
Kata za Manisipaa ya Tabora - Mkoa wa Tabora - Tanzania | ||
---|---|---|
Chemchem | Cheyo | Gongoni | Ifucha | Ikomwa | Ipuli | Isevya | Itetemia | Itonjanda | Kabila | Kakola | Kalunde | Kanyenye | Kidongochekundu | Kiloleni | Kitete | Malolo | Mapambano | Mbugani | Misha | Mpela |Mtendeni | Mwinyi | Ndevelwa | Ng'ambo | Ntalikwa | Tambuka-Reli | Tumbi | Uyui |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tabora bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Tabora (mji) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |