Nana Akufo-Addo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nana Akufo-Addo

Nana Addo Dankwa Akufo-Addo (* Swalaba, Accra, 29 Machi 1944) ni mwanasheria na mwanasiasa wa chama cha NPP nchini Ghana.

Tangu tarehe 7 Januari 2017 ni rais wa nchi baada ya kushinda mara mbili uchaguzi mkuu. Mwaka 2016 Akufo-Addo alikuwa anagombea urais wa Ghana dhidi ya rais mtendaji John Dramani Mahama ikiwa ni mara ya tatu baada ya majaribio ya awali miaka 2008 na 2012.

Familia na elimu[hariri | hariri chanzo]

Nana Addo Dankwa Akufo-Addo alizaliwa mjini Accra katika familia ya wanasiasa. Baba yake Edward Akufo-Addo alikuwa jaji mkuu wa Ghana na baadaye rais wa taifa kati ya miaka 1969 na 1972. Mjomba wake Joseph Boakye Danquah alikuwa kiongozi wa upinzani dhidi ya rais Kwame Nkrumah na mjomba mwingine, William Ofori Atta, alikuwa waziri wa mambo ya nje.

Baada ya kusoma shule ya msingi Accra alikwenda kwa masomo ya O- na A-level huko Lancing College, Sussex, Uingereza. Alianza masomo ya Falsafa, Siasa na Uchumi kwenye Chuo Kikuu cha Oxford bila kumaliza.

Baada ya kurudi Ghana alisoma uchumi kwenye Chuo Kikuu cha Ghana akapata cheti cha kwanza mwaka 1967. Akaenda tena Uingereza kusoma sheria akipata kibali cha kufanya kazi ya mwanasheria mwaka 1971. Alifanya kazi hiyo mjini Paris, Ufaransa, hadi mwaka 1975 aliporudi Ghana.

Hapa Accra alijiunga na kampuni ya sheria hadi kuanzisha kampuni yake mwenyewe mwaka 1979.

Siasa ya Ghana[hariri | hariri chanzo]

Tangu kurudi Ghana alishiriki katika harakati ya kidemokrasia ya "People’s Movement for Freedom and Justice" iliyolenga kumaliza serikali ya kijeshi iliyokuwepo Ghana hadi kurudi kwenye siasa ya vyama vingi kwa miaka michache kuanzia 1979.

Mwishoni mwa utawala wa kijeshi wa Jerry Rawlings alianza tena kuandaa chama kipya cha NPP kuanzia mwaka 1992.

Kuanzia mwaka 1996 hadi 2008 alichaguliwa mara tatu kuwa mbunge. Mwaka 1998 alijaribu kuwa mgombea wa urais kwa niaba ya chama cha NPP lakini hakufaulu. Aliendelea kumfanyia kampeni mgombea mshindi John Kufuor. Baina ya 2001 na 2007 alikuwa waziri katika serikali ya rais huyo, kwanza kama waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu, halafu kama Waziri wa Mambo ya Nje ya Ghana.

Alipokuwa Mwanasheria Mkuu alihusika na ufutaji wa sheria kuhusu kashfa za kijinai iliyowahi kukandamiza uhuru wa magazeti na uhuru wa kutoa maoni kwa jumla.

Mgombea wa Urais[hariri | hariri chanzo]

Alijiuzulu kutoka serikali baada ya kuamua kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2008 upande wa NPP lakini alishindwa na John Atta Mills. Akufo-Addo alipata kura 4,480,446 au asilimia 49.77, hivyo tofauti ilikuwa ndogo sana na Akufo-Addo alisifiwa kwa kukubali ushindi wa mpinzani wake na hivyo kuepukana na ghasia iliyohofiwa.

Mwaka 2012 aligombea pia lakini alishindwa tena kwa kura chache na John Dramani Mahama aliyewahi kuwa makamu wa rais Atta Mills.

Akufo-Addo alipewa nafasi ya kugombea kwa niaba ya NPP mara ya tatu katika uchaguzi wa rais wa tarehe 7 Desemba 2016 dhidi ya Mahama aliyejaribu kurudishwa. Tume ya uchaguzi ilitangaza matokeo ya kuwa

Mgombea Chama Kura %
Nana Akufo-Addo New Patriotic Party 5,716,026 53.85
John Dramani Mahama National Democratic Congress 4,713,277 44.40
Chanzo: Electoral Commission Ghana

Marejeo[hariri | hariri chanzo]


Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nana Akufo-Addo kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.