Mtume Barnaba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Kifodini cha Mt. Barnaba, kutoka Legenda Aurea ya Jacopo wa Varazze.

Yosefu wa Kupro, Myahudi wa kabila la Lawi, anajulikana hasa kupitia kitabu cha Matendo ya Mitume.

Humo tunapata habari kuwa aliongokea mapema Ukristo, akauza shamba lake na kuwakabidhi Mitume wa Yesu mapato yake ili wawasaidie maskini. Labda kwa sababu hiyo Mitume walimuita Barnaba, yaani "Mwana wa faraja" (Mdo 4:36-37).

Kisha kuheshimiwa hivyo katika Kanisa la awali huko Yerusalemu, alimtambulisha na kumdhamini Mtume Paulo muda mfupi baada ya huyo kuongoka huko Damasko (Mdo 9:26-28).

Watu wa mataifa walipoanza kuingizwa moja kwa moja katika Ukristo huko Antiokia, alitumwa huko kwa niaba ya Kanisa mama, akawa kiongozi mkuu wa jumuia hiyo mpya (Mdo 11:19-30; 13:1).

Baadaye Roho Mtakatifu alidai yeye na Paulo wapelekwe kufanya umisionari sehemu nyingine, wakaondoka pamoja na binamu yake, Yohane Marko, kuelekea kwanza kisiwani Kupro, halafu bara, katika maeneo ya Uturuki Kusini wa leo (Mdo 13:2-14:28).

Kazi yao ilipopata upinzani kwa kutodai Wapagani wakiongoka washike Torati yote, walikwenda pamoja Yerusalemu (mwaka 49 hivi, kwa mtaguso wa Mitume, ambao uliamua kuhusu suala hilo (Mdo 15:1-35).

Baada ya kutengana na Paulo, Barnaba alifunga tena safari kwenda Kupro pamoja na Marko (Mdo 15:36-39) kati ya miaka 50 na 53, na baada ya hapo hatuna tena habari ya hakika juu yake.

Kanisa Katoliki, Waorthodoksi, Waanglikana na Walutheri wanamheshimu kama mtakatifu tarehe 11 Juni.

Wataalamu wengine wanamtaja kama mtunzi wa Waraka kwa Waebrania, na Klemens wa Aleksandria alimtaja kama mwandishi wa Waraka wa Barnaba, lakini hakuna hakika.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Attwater, Donald and Catherine Rachel John. "The Penguin Dictionary of Saints," 3rd edition, New York: Penguin Books, 1993. ISBN 0-14-051312-4.

Kuhusu maandishi yake[hariri | hariri chanzo]

  • Die Apostolischen Väter. Griechisch-deutsche Parallelausgabe. J.C.B. Mohr Tübingen 1992. ISBN 3-16-145887-7
  • Der Barnabasbrief. Übersetzt und erklärt von Ferdinand R. Prostmeier. Series: Kommentar zu den Apostolischen Vätern (KAV, Vol. 8). Vandenhoeck & Ruprecht: Göttingen 1999. ISBN 3-525-51683-5

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Commons-logo.svg
Wikimedia Commons ina media kuhusu: