Funduku

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Sarcoptes scabiei)
Funduku
Funduku chini ya hadubini
Funduku chini ya hadubini
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Faila: Arthropoda
Nusufaila: Chelicerata
Ngeli: Arachnida
Nusungeli: Acari
Oda: Sarcoptiformes
Nusuoda: Astigmata
Familia: Sarcoptidae
Jenasi: Sarcoptes
Latreille, 1802
Spishi: S. scabiei
(Linnaeus, 1758)

Funduku (Sarcoptes scabiei) ni utitiri mdogo sana wa familia Sarcoptidae katika oda Sarcoptiformes anayesababisha ugonjwa au hali ya ngozi iitwayo upele wa funduku. Utitiri huyu huishi katika ngozi ya watu na wanyama mbalimbali.

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Wapevu wana umbo la duaradufu. Urefu wa majike ni mm 0.3-0.45 na upana wao ni mm 0.25-0.35. Ukubwa wa madume ni nusu ya ule wa majike. Hawana macho lakini wana jozi nne za miguu, mbili mbele na mbili nyuma. Ncha za miguu ya mbele ya majike zina mibenuko mirefu kwa umbo la vineli inayoweza kumung'unya, na ncha za miguu ya nyuma zina manyoya magumu. Funduku hutumia miundo hiyo kujianga ndani ya upenyo akichimba. Madume wana miundo ya kumung'unyia kwenye miguu yote isipokuwa jozi ya tatu, ambayo inawatofautiana na majike.

Majike huchimba penyo katika ngozi ambamo wanataga mayai mawili au matatu kila siku moja hadi tatu. Kuchimba na kutaga kunaendelea wiki 2-3 na baada ya kutaga mayai 30 jike anakufa mwishoni kwa upenyo. Penyo zina umbo la S mara nyingi.

Mayai hutoa lava wenye miguu sita baada ya siku 3-10. Hao huenda juu ya ngozi na kutafuta folikali za nywele au mahali pengine pazuri kupenya. Wanachimba upenyo mfupi ambamo wanakula. Baada ya siku 3 au 4 wanajibua na kubadilika katika tunutu wenye miguu minane. Kutoka hatua hii madume hujibua ili kuwa wapevu. Majike wana hatua moja nyingine ya tunutu kabla kuwa wapevu. Kwa sababu ya hiyo majike ni wakubwa kuliko madume. Madume huingia penyo za majike ili kupandana. Kisha majike wanaondoka na kutafuta mahali pa kuchimba upenyo wa kujilisha na kutaga mayai.

Dalili[hariri | hariri chanzo]

Uwepo wa funduku hugunduliwa wakati majike wanaanza kuchimba ndani ya ngozi. Hii husababisha kuwasha sana na upele wa vipele vidogo. Mayai na kinyesi katika penyo vinaweza kusababisha athari kali ya mzio, ambayo husababisha kuwasha zaidi. Ngozi huharibiwa mara nyingi kwa sababu ya kujikuna, ambayo inaweza pia kuleta maambukizo ya sekondari. Katika visa vibaya, ngozi inaweza kufunikwa kwa vigaga. Sehemu za mwili zinazoathiriwa mara nyingi sana ni mikono na vifundo vyao, lakini sehemu nyingine ni tumbo, makombe ya mabega, makwapa, viwiko, magoti, matako na sehemu za mbeleni.

Watu wengine huendeleza athari za wepesi kupita kiasi kuhisi zinazachelewa ambazo huanza siku 30 baada ya uvamizi wa kwanza. Wakivamiwa tena, watu kama hao wanaweza kuonyesha dalili ndani ya masaa.

Wanadamu sio mamalia wa pekee ambao ni vidusiwa wa funduku. Mbwa na paka wa porini na wa kufugwa wanaweza kuathiriwa, ambayo ni sababu moja ya upele wao. Wanyama wengine ni ng'ombe, kondoo, nguruwe-mwitu, wombati, koala na masokwe. Wanyama hawa wana vigaga mara nyingi kuliko watu, labda kwa sababu ya ngozi zao zenye manyoya.

Funduku huenea kwa kugusana ngozi mara kwa mara, kwa wanadamu na kwa wanyama. Aina za Sarcoptes scabiei kutoka wanyama na spishi nyingine za Sarcoptes zinaweza kusababisha dalili za muda mfupi kwa wanadamu, lakini funduku hawa hawazaani katika kidusiwa wa kibinadamu.