Nenda kwa yaliyomo

Mwenyezi Mungu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mwenyezi)

Mwenyezi Mungu katika lugha ya Kiswahili ni jina linalotumika kwa Muumba wa kila kitu, Mwenye kuabudiwa kwa haki, kinyume na neno mungu ambalo linamaanisha chochote au yeyote anayeabudiwa ikiwa kwa haki au si kwa haki.

Neno Mwenyezi linaunganisha Mwenye na enzi na kumpatia Mungu sifa ya kuweza yote, bila kuzuiliwa na yeyote wala chochote.

Kwa uweza huo, Mwenyezi Mungu ni Muumba wa mbingu na dunia na kila kilichomo ndani yake, naye ni Mlezi wa viumbe vyote na Mpaji riziki kwa kila chenye uhai ulimwenguni.

Mwenyezi Mungu, katika dini na mila nyingi duniani, ni yule anayestahiki kuabudiwa kwa haki ikiwa peke yake bila kushirikishwa na chochote, au kwa kushirikishwa na viumbe, kwa nia ya kuwa hawa viumbe vinamkurubisha naye.

Hii ni kwa sababu, kila dini au mila ina namna yake ya kumsawiri Mwenyezi Mungu, na njia gani sahihi ya kumuabudu, na kwa kuwa hakuna itifaki baina ya hizi dini, mila na madhehebu kuhusu Mwenyezi Mungu na namna anavyotakikana kuabudiwa, hizi tofauti chungu nzima zimetokea.

Sifa za Mwenyezi Mungu

[hariri | hariri chanzo]

Mwenyezi Mungu ana sifa mbali mbali kwa mujibu wa dini na mila na madhehebu tofautitofauti, na watu wanamsifu Mwenyezi Mungu kwa namna ambayo wanamjua wao kulingana na mafunzo ya dini na mila zao.

Hii ni kwa sababu, watoto tangu wazaliwapo hufunzwa na wazee wao habari za Mwenyezi Mungu na namna ya kumuabudu, na mafunzo haya hubakia katika mawazo na fikra zao, na kukua nayo mpaka ukubwani mwao.

Imani ya Waislamu

[hariri | hariri chanzo]

Uislamu, kwa mfano, unaeleza kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja tu, hana mshirika, hana mwanzo wala mwisho, hakuzaa wala hakuzaliwa, wala hapana yeyote mwenye kufanana au kushabihiana naye, naye ni Mola wa ulimwengu huu wote, na Muumba wa kila kitu.

Kwake Yeye inatoka riziki ya kila kiumbe, na ndiye Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha. Marejeo ya viumbe vyote wakisha kufa na kufufuliwa ni kwake Yeye tu siku ya Kiyama.

Yeye pekee ndiye Mwenye kuhukumu viumbe siku ya malipo, na ndiye atakayewapa waja wake ujira na thawabu na kuwatia Peponi kwa mema waliyoyafanya, au kuwatia adabu na kuwapa adhabu na mateso na kuwatia Motoni kwa maovu waliyotenda hapa duniani.

Waislamu wanafunzwa tangu utotoni mwao kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja tu peke yake, hana mshirika, naye ndiye mwenye kufaa kuabudiwa kwa haki bila ya kushirikishwa na chochote katika viumbe vyake, na kuwa Yeye ni wa kutegemewa katika kila kitu na kuombwa msaada na kuombwa msamaha wakati wa makosa na madhambi.

Yeye hana kitu kilichofanana naye, hakuzaa wala hakuzaliwa, hana mwanzo wala mwisho. Mwingi wa rehema na Mwenye kurehemu, Mtoa riziki, Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha. Hukumu yote ni yake siku ya Kiyama. Mtukufu na Mkubwa. Bwana na Mola wa walimwengu wote. Yeye tu ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa na Yeye tu ndiye Mwenye kufaa kuombwa na kutakwa msaada.

Imani ya Wakristo

[hariri | hariri chanzo]

Ukristo unakubaliana na Uyahudi na Uislamu katika mengi ya sifa hizi za Mwenyezi Mungu za kuumba, kuhuisha na kufisha, kuruzuku, kufufua, kuhukumu na kulipa ya kheri kwa mwenye kufanya kheri na ya shari kwa mwenye kufanya shari, lakini aghlabu ya madhehebu ya Kikristo, ijapokuwa si yote, yanampa Mwenyezi Mungu sifa ya kuwa Utatu Mtakatifu, na kumsifu kuwa huyohuyo ni Mungu Baba na Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, na kuwa wote hawa watatu wanachanga uungu pekee kwa umoja kamili kabisa kwa dhati.

Uislamu, kwa upande wake, unakataa katakata masuala ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote, na kwa hiyo ni Mmoja tu wala hana mshirika wa aina yoyote.

Katika majadiliano juu ya hilo, mara nyingi Wakristo wanahisi Waislamu wanakariri imani yao wenyewe bila kusikiliza maelezo ya upande wa pili, kwamba fumbo la Utatu Mtakatifu halimaanishi kushirikisha sifa za Mwenyezi Mungu na wengine wawili nje yake, bali kwamba ndiyo alivyo kwa ndani.

Kama vile sifa zote za Mungu (zilizoorodheshwa na Uislamu katika majina 99) zisivyovuruga umoja wake, ndivyo ilivyo kwa Utatu: kwa Wakristo karibu wote nafsi tatu ni za Mwenyezi Mungu yuleyule na zinadokeza kwamba milele yote Yeye (nafsi ya 1) anajifahamu (nafsi ya 2) na anajipenda (nafsi ya 3).

Dini nyinginezo

[hariri | hariri chanzo]

Dini nyinginezo, kadhalika, zina tasauri na fikra nyingine kuhusu Mwenyezi Mungu.

Kuna wale wanaoabudu viumbe mbalimbali wakichukulia kuwa wanamwakilisha Mwenyezi Mungu, kama kuabudu sanamu, nyota, jua, ng'ombe, wanyama mbalimbali, mizimu, miti, moto, viumbe wenziwao, malaika, majini na kadhalika.

Dini na mila hizi, pengine huchukulia kuwa vitu hivi vinatusaidia kutufikisha kwa Mwenyezi Mungu, na kuwa bila ya vitu hivi, ibada zetu haziwezi kufika.

Ama wengine huwa na imani kuwa vitu hivi ndio Mola mwenyewe wa kuabudiwa na kuombwa na kutakwa msaada.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.