Muhammad Ahmad ibn Abd Allah Al-Mahdi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mohammad Ahmad al-Mahdi.

Mohammed Ahmad ibn Abd Allah (12 Agosti 1844 - 22 Juni 1885) alikuwa mwenyeji wa Sudani aliyejitangaza kuwa ndiye mahdi. Alifaulu kuunganisha makabila mbalimbali ya nchi hiyo kwa vita ya jihadi akamaliza utawala wa kikoloni wa Misri iliyosaidiwa na Uingereza na kuanzisha Dola la Mahdi.

Baada ya miaka ya kufundisha Uislamu na kusafiri nchini Sudani Muhammad Ahmad alijitangaza kuwa al-Mahdi al-Muntazar (mwokozi anayetarajiwa) mwaka 1881. Katika barua ya tarehe 29 Juni 1881 aliwaeleza Wamisri ya kwamba aliteuliwa kuunganisha nchi zote za Waislamu na kurudisha uataratibu wa siku za Mtume Muhamad.

Gavana Mmisri alijaribu kumkamata lakini askari zake walishambuliwa na kuuawa na wafuasi wa al-Mahdi. Baada ya hayo Muhamad Ahmad alitangaza vita ya jihadi akafaulu kukusanya maansar au wasaidizi wengi. Watu walimfuata kwa sababu mbalimbali. Wengine hasa watu wengi maskini walimwamini ndiye al-Mahdi wa Allah. Viongozi wa makabila ya Waarabu walichukia utawala wa Wamisri wakamkubali kama kiongozi atakayewaondoa. Wengine tena walikuwa wakitajirika kwa njia ya biashara wa watumwa wakakasirika majaribio ya serikali ya Misri iliyotaka kukandamiza biashara hiyo.

Katika mapigano mbalimbali maasar waliweza kushinda jeshi la Wamisri na kukamata bunduki nyingi pamoja na risasi na dhahabu. Kilele cha jihadi kilikuwa kutekwa kwa mji mkuu wa Khartum tarehe 26 Januari 1885. Gavana Mkuu jenerali Gordon Pasha aliuawa. Al-Mahdi alianzisha mji mkuu mpya Omdurman kando ya mto Nile ng'ambo ya Khartum uliokuwa mji mkuu wa Dola la Mahdi.

Hapo aliaga dunia tarehe 22 Juni 1885. Dola lililoanzishwa naye likaendelea hadi mwaka 1895 lilipovamiwa na jeshi la Waingereza pamoja na Wamisri na kurudi chini ya utawala wa nchi hizo pamoja.