Kunguni-maji mkubwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kunguni-maji mkubwa
Lethocerus oculatus nchini Madagaska
Lethocerus oculatus nchini Madagaska
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu, nge, buibui)
Nusufaila: Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita)
(bila tabaka): Dicondylia (Wadudu walio na mandibula zenye condyle mbili)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Nusungeli: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda ya juu: Paraneoptera
Oda: Hemiptera
Haeckel, 1896
Nusuoda: Heteroptera
Oda ya chini: Nepomorpha
Familia ya juu: Nepoidea
Familia: Belostomatidae
Leach, 1815
Ngazi za chini

Nusufamilia 3; jenasi 11, 5 katika Afrika:

Kunguni-maji wakubwa, wauma kidole au mende-maji ni wadudu wadogo hadi wakubwa sana wa maji wa familia Belostomatidae katika oda ya chini Nepomorpha ya oda Hemiptera ambao madume wa spishi nyingi (isipokuwa zile za Lethocerinae) hubeba mayai mgongoni. Spishi za Lethocerus zinaweza kufikia zaidi ya sm 10 na ni miongoni mwa wadudu wakubwa kabisa duniani[1]. Wadudu hawa wanatokea maeneo yote yenye maji ya tropiki na nusutropiki, spishi nyingi sana huko Amerika ya Kusini na 26 tu hapa Afrika[2].

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Kunguni-maji wakubwa wana urefu wa sm 1-12. Mwili wao ni bapa na una umbo la duaradufu[3]. Miguu yao ya mbele ni imara sana na ina ukucha mmoja tu na hutumiwa kukamata mbuawa. Walakini, spishi za Limnogeton zina miguu ya mbele ya kawaida, kwa sababu zinakula konokono tu. Miguu ya kati na ya nyuma hutumiwa kwa kuogelea, ingawa haijatoholewa sana kwa hiyo. Sehemu za kinywa ni imara na kama sindano. Spishi nyingi zina mabawa yaliyokuzwa vizuri na huruka vizuri, lakini nyingine haiwezi kuruka kwa sababu mabawa yao yamepunguka[2]. Kama nge-maji wana mrija wa kupumua mwishoni mwa fumbatio yao, lakini ni fupi zaidi. Kwa kawaida hauonekani, kwa sababu umerudishwa ndani wakati hawapumui.

Biolojia[hariri | hariri chanzo]

Wadudu hao huwa wanakaa kwenye sakafu ya maji au kati ya uoto wa maji. Wengi sana hutokea katika maji yasiyotiririka, lakini wengine hutokea kwenye vijito na mito yenye mimea. Wanaogelea kwa shida na ili kukimbia tu au kwenda kwa uso wa maji ili kupumua kwa mrija wao wa kupumulia. Mbuawa anapokaribia wanamshika kwa miguu yao imara ya mbele[4]. Kisha wanamtoboa kwa kinywa chao na kuingiza mate ambayo hufanya tishu kuwa kiowevu. Baada ya hayo wanafyonza yaliyomo. Mbuawa ni pamoja na wadudu wakubwa, samaki wadogo, ndubwi, vyura wadogo, salamanda na nyoka wachanga wa maji. Spishi kubwa zaidi zinaweza hata kukamata ndege wadogo.

Kunguni wakubwa wa maji wanajulikana sana kunyakua vidole vya miguu vya watu[5]. Ikiwa mguu haujaondolewa haraka vya kutosha, kinywa kinaweza kutoboa kidole, ambacho ni chungu sana. Kwa watu wengine inaweza kusababisha uvimbe, homa na ugumu wa kupumua.

Miongoni mwa wadudu hao, madume hutunza mayai, wakati mwingine wale wa majike kadhaa. Majike wa Lethocerinae hutaga mayai yao kati ya mimea, lakini wale wa jamii nyingine hubandika mayai yao kwenye migongo ya madume, ambao huyabeba mpaka yanapoanguliwa.

Spishi zinazoweza kuruka mara nyingi huonekana usiku karibu na taa za umeme. Kwa watu wengi, ni fursa pekee ya kuona wadudu hao.

Kama chakula[hariri | hariri chanzo]

Katika Asia ya Kusini na ya Kusini-Mashariki kunguni-maji wakubwa huliwa sana, hasa Lethocerus indicus[6]. Watu huwavutia usiku kwa taa katika mitego. Hukaangwa kabla ya kuliwa.

Spishi za Afrika[hariri | hariri chanzo]

  • Appasus ampliatus
  • Appasus capensis
  • Appasus grassei
  • Appasus major
  • Appasus nepoides
  • Appasus procerus
  • Appasus quadrivittatus
  • Appasus severini
  • Appasus stappersi
  • Appasus urinator
  • Appasus wittei
  • Diplonychus eques
  • Diplonychus esakii
  • Diplonychus eques
  • Hydrocyrius colombiae
  • Hydrocyrius longifemoratus
  • Hydrocyrius nanus
  • Hydrocyrius punctatus
  • Diplonychus rectus
  • Lethocerus cordofanus
  • Lethocerus edentulus
  • Lethocerus oculatus
  • Limnogeton expansum
  • Limnogeton fieberi
  • Limnogeton hedenborgi
  • Limnogeton scutellatum

Picha[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. P. J. Perez-Goodwyn (2006). "Taxonomic revision of the subfamily Lethocerinae Lauck & Menke (Heteroptera: Belostomatidae)". Stuttgarter Beiträge zur Naturkunde. Serie A (Biologie) 695: 1–71. 
  2. 2.0 2.1 J.H. Thorp; D.C. Rogers, wahariri (2015). Thorp and Covich's Freshwater Invertebrates: Ecology and General Biology 1 (toleo la 4). Elsevier. ku. 954–955. ISBN 978-0-12-385026-3. 
  3. Randall T. Schuh; James Alexander Slater (1996). True Bugs of the World (Hemiptera:Heteroptera): Classification and Natural History (toleo la 2). Cornell University Press. ku. 111–114. ISBN 978-0801420665. 
  4. Merritt, R.W. (2008). An Introduction to the Aquatic Insects of North America. Dubuque, Iowa: Kendall/Hunt Company. 
  5. A. C. Huntley (1998). "Lethocerus americanus, the "toe biter"". Dermatology Online Journal 4 (2): 6. PMID 10328676. 
  6. Mitsuhashi, J. (2017). Edible Insects of the World. CRC Press. ISBN 978-1-4987-5657-0.