Krim
Krim (kwa Kirusi Крым Krym; kwa Kiukraina Крим Krim; kwa Kitartari Qırım; kwa Kiingereza Crimea) ni rasi upande wa kaskazini wa Bahari Nyeusi yenye eneo la km² 26.100.
Kisiasa ni jimbo la kujitawala ndani ya nchi ya Ukraine na jina rasmi ni "Jamhuri ya kujitawala ya Krim". Tangu mwaka 2014 ilivamiwa na kutekwa na jeshi la Urusi na kutangazwa kuwa sehemu ya Urusi, hatua isiyotambuliwa na umma wa kimataifa. Zaidi ya nusu ya wakazi 1.994.300 (mwaka 2005) ni Warusi (58,5 %), takriban robo Waukraine (24,4 %) halafu kuna pia Watartari 243.400 (12,1 %).
Historia
[hariri | hariri chanzo]Rasi hii ina historia ndefu iliyoona mabadiliko mengi kiasi kwamba haiwezekani kusema ni nani wanaoweza kuitwa "wakazi asilia" wa nchi hii.
Katika historia inayojulikana Krim ilitawaliwa na Waskithi, Wagiriki wa Kale, Roma ya Kale, Wagothi, Bizanti, Wahunni, Wakhazari, Wamongolia, Waitalia kutoka Venezia na Genua, Watartari, Waosmani, Urusi na tangu 1991 nchi huru ya Ukraine.
Kwa muda mrefu lugha ya mawasiliano ilikuwa Kigiriki hadi kuingia kwa Watartari Waislamu mnamo karne ya 15 walioleta lugha yao ya Kiturki.
Tangu mwaka 1783 Krim ilikuwa sehemu ya Milki ya Urusi na Warusi walileta walowezi wengi kutoka kwao. Sehemu ya Watartari walihamia Uturuki. Chini ya utawala wa Kirusi muundo wa wakazi ulibadilika hadi Warusi walikuwa kundi kubwa.
Katika miaka 1853 hadi 1856 rasi iliathiriwa vibaya na vita ya Krim ambako jeshi la Waturuki Waosmani pamoja na Uingereza na Ufaransa lilishambulia ngome ya Kirusi ya Sevastopol.
Baada ya kuporomoka kwa Milki ya Urusi mwaka 1917 Watartari walitangaza jamhuri ya kujitegemea kwa muda mfupi. Tangu 1918 Krim ilirudishwa Urusi kwa nguvu ya kijeshi na kuwa sehemu ya Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi ndani ya Umoja wa Kisovyeti. Hapo Krim ilikuwa eneo la kujitawala chini ya Urusi. Mwaka 1944, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia Watartari wote walifukuzwa katika Krim kwa amri ya Stalin na kupelekwa sehemu za Asia ya Kati, hasa Uzbekistan.
Mwaka 1954 serikali ya Umoja wa Kisovyieti iliamua kuhamisha eneo lote la Krim kutoka jamhuri ya Urusi kwenda Jamhuri ya Kisovyeti ya Kijamii ya Kiukraine. Tangu miaka ya 1980 Watartari walianza kurudi Krim kutoka sehemu za Asia ya Kati. Leo hii wako tena, na lugha yao inakubalika kama lugha rasmi kimkoa pamoja na Kirusi.
Wakati Umoja wa Kisovyeti ulipoporomoka na Ukraine kuwa nchi huru mwaka 1991 rasi ya Krim ilikuwa ndani ya Ukraine kwa hali ya "Jamhuri ya kujitawala ya Krim".
Baada ya mapinduzi ya Ukraine ya mwaka 2014 sehemu ya wakazi wa Krim walikataa mwelekeo mpya wa serikali ya Kiev. Rais wa Urusi Vladimir Putin alitumia nafasi hiyo kutuma wanajeshi wa Urusi wasiovaa sare rasmi ndani ya Krim na baada ya kura ya maoni wananchi wengi walipiga kura ya kujiunga na Urusi. Mwezi wa Machi Urusi ilitangaya eneo la Krim kuwa sehemu ya Shirikisho la Urusi.
Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Krim kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |